Ni kweli, msaliti mkubwa wa chama hicho ni Bunge linaloundwa na wabunge wa CCM wanaozidi idadi ya upinzani. Kwa ‘usaliti huo’, idadi hizo hukaribiana kadri miaka inavyokwenda, kutoka 206 kwa 26 mwaka 2005 mpaka 156 kwa 116 mwaka 2015!
Chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi, miaka yote kimekuwa kikiongozwa na viongozi kutoka CCM, wengi wao wanaochangia sana ‘kukisaliti’ chama chao kwa wapiga kura kwa uendeshaji mbaya wa bunge kwa kubagua pande, kuwabana wapinzani na kuwaachia wabunge wa CCM kwa mambo yale yale.
Hayo yanawapa wapinzani kura nyingi za huruma. Kinachosahaulika hapa, zaidi ya wapinzani kubeba sana agenda za kitaifa, kwenye majimbo yao wanaishi watu wa itikadi mbali mbali wakiwamo wana CCM.
Wapinzani wanapoteswa na uongozi wa Bunge kwa kupigania yale yanayoonekana kuwa na maslahi kwa wananchi, ushabiki wa watu kwa upinzani na chuki kwa CCM vinaongezeka.
Wabunge wa upinzani wanaonekana wako na wananchi na wa CCM wako na serikali yao inayotenda yale ya yanayojadiliwa bungeni, mengine yakiwa yanayokosewa. Matokeo ya uchaguzi yakiwa si mazuri kutokana na matukio hayo ya bungeni, viongozi wa CCM wanadai kuna wasaliti nje ya Bunge wakati wasaliti wao wamo bungeni.
Tazama hili suala la wanafunzi zaidi ya 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliokuwa wanaosomea shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi walikosa masomo baada ya walimu kugoma kuwafundisha kutokana na mipango ya utoaji wa elimu ya masomo ya sayansi kutokamilika.
Mipango hiyo ni kuongezwa kwa idadi ya walimu kulingana na wingi wa wanafunzi, kuwapo kwa maabara za kutosha na wataalam wa kuzisimamia maabara au laboratory technicians).
Hatua walizochukua wanafunzi kuonyesha kukerwa kwao na kukosa masomo zilisababisha wafukuzwe chuo bila kujali utu kwa kutozingatia wangenunuaje chakula, wangelala wapi mjini Dodoma na wangesafirije kurudi makwao.
Wabunge waliomba mwongozo wa kusimamishwa kwa muda kujadili hoja iliyokuwa mezani ili watumie wajadili tukio hilo zito. Naibu Spika alikataa. Kilichofuatia ni kikao kuvurugika.
Kwa sababu agenda hiyo ilibebwa zaidi na wabunge wa upinzani licha ya kuanzishwa na mbunge wa CCM, ni wazi ushabiki wa watu kwa wabunge wa upinzani uliongezeka.
Wanafunzi waliofukuzwa wanatoka Tanzania nzima na kila mmoja ana kadri ya ndugu, jamaa na marafiki 30 wanaoamini wabunge wa upinzani walikuwa nao.
Kwa hesabu hiyo, kwa tukio hili tu, tayari watu 217,000 (wakiwamo vijana wenyewe) wameshaingia kwenye kundi la kuichukia CCM! Hao 217,000 nao wakimwaga sumu kwa wengine 10 tu kila mmoja na sumu kuwakolea,tayari wanafika watu 2,170,000. Hawa ni wengi sana ikizingatia wapigakura wa nchi hii huwa hawafiki milioni 10.
Hili swali linapaswa kuulizwa ndani ya vikao vyovyote vya CCM kikiwamo cha wabunge wa CCM na vikao vingine vya chama hicho.
Hivi kuna tija gani kwa CCM na serikali kulifanya Bunge kuwa chombo cha kuitetea serikali hata kwa mambo ambayo ni kero kwa wananchi?
Hivi wabunge hawa wanaenda sawa na falsafa inayoelezwa sana ya kujali maslahi ya wanyonge wa nchi hii? Kuna wanyonge kama wanafunzi wanaofukuzwa bila msaada wowote wa chakula, maji, malazi na nauli ya kwenda makwao?
Hivi kujadili namna ya kuwasaidia vijana hao wa kiume na wa kike kulikuwa na madhara gani kwa mtu yeyote yule zaidi ya faida kwa wanafunzi hao wa nchi hii? Kama ni suala la kuumbuana akilengwa mwenye mamlaka aliyekosea kwenye hili (kama kosa lipo), kukosolewa kwa mtu huyo si ndio kujipanga vizuri ili tusiharibu siku zijazo?
Na kama ni kuepuka kuumbuana, kuzuia mjadala kuna maana huyo wa kuumbuliwa hana majibu? Kwa nini mjadala usingefanywa na wa kujibu ajibu? Tukirudi nyuma, sura ya mjadala huo ilikuwa si ya kumuumbua mtu bali ya kutafuta ufumbuzi. Uongozi wa Bunge umekataa lakini kesho tunatarajia vijana hao wawe wazalendo.
Hawatakuwa, wataichukia CCM na wataichukia nchi yao. Wataenda upinzani si kwa sababu yoyote zaidi ya sababu ya kuichukia CCM.
Halafu hawa wanasomea taaluma ya ualimu. Wakifanikiwa kumaliza masomo, watafundisha. Wataingiza misimamo gani kwa watakaowafundisha hata kama watakuwa wanawafundisha sayansi?
Bunge lazima lijikumbushe kwamba lenyewe ni chombo kinachowawakilisha wananchi kuisimamia serikali na kutunga sheria. Inakuwaje leo linageuzwa kuwa wakili wa serikali? Bila kuisimamia sawasawa serikali, tutafanikiwa vipi kupata maendeleo?
Kwa ufupi, hakuna mwana CCM nje ya Bunge anayekisaliti chama hicho kwenye uchaguzi bali mwenendo wa wanachama wanaoongoza chombo hicho na baadhi ya wabunge wake ndiyo wasaliti hasa wa chama hicho. Asitafutwe mchawi mwingine wa kupanda kwa wapinzani na kushuka kwa CCM kwenye kila uchaguzi. Wachawi ni hao.










