Kauli hiyo ilikuja siku moja baada ya Naibu Spika Dk. Tulia Ackson, kukataza Bunge kujadili sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliotumuliwa kwa maelezo kuwa hawafundishi kwa muda mrefu kutokana na walimu kugoma wakidai malimbilikizo ya stahili mbalimbali.
Sipendi kuingia kwa undani yaliyojiri huko chuoni kwani shabaha ya makala haya ni kujadili msimamo wa kambi rasmi hiyo kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika Dk. Ackson.
Kwa kile kinachoonekana kama ni kampeni baridi mithili ya vita baridi vya dunia inayooandaliwa na kambi ya upinzani dhidi ya CCM, “kutishia nyau”, Mbowe alinukuliwa akisema “kama Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti hatatuona bungeni hata kama ni leo au kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo.”
Sina tatizo na msimamo huo na wala sipingani na hatua hizo zilizochukuliwa kwani inafahamika kuwa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, uamuzi wa kambi ya upinzani kuamua kususia vikao vya Bunge na kutoka nje ni haki yao.
Hata hivyo, swali ambalo wadau wengi wanajiuliza, je, kumsusa Naibu Spika, katika vikao atakavyoongoza ndiyo itakuwa suluhisho la kudumu ama ndiyo itakuwa suluhu ya madhila mengine yanayogusa utekelezaji wa kila siku ndani ya Bunge?
Hiki ni kitendawili kinachohitaji kambi ya Mbowe wakae na wajadili kwa makini. Ni kweli Mbowe na kambi yake wanazo haki zote za kususia vikao vinavyoongozwa na Dk. Ackson isipokuwa wajaribu kuangalia athari zake kwani tendo la kususia mara nyingi halina tija kwa kuwa wametumwa na wananchi kuwawakilisha.
Kwa hiyo binafsi kama ningekuwa mmoja kati ya washauri wa Mbowe ningependekeza yafuatayo :-
Mosi, kuunda tume ya kambi rasmi nje ya Bunge ambayo itawasaidia kutanzua matatizo yanayojitokeza kila mara katika kipindi cha Bunge na kushauriana nini kifanyike haraka juu ya tukio la dharura kama hilo ili wananchi wasiwaelewe vibaya.
Pili, ikumbukwe kuwa uchaguzi mkuu uliopita, kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), iliwavuna wanasiasa mahiri na mashuhuri waliobobea katika shughuli za Bunge na masuala ya kisiasa za hapa nchini, watu hao ni mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Fredrick Sumaye, wapo pia wenyeviti wa CCM Mikoa amabo ni Mgana Msindai wa Singida, Hamis Mgeja wa Shinyanga na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, John Guninita.
Viongozi hawa ni watu muhimu wenye busara ndani ya Ukawa, wangetumiwa katika kutafuta majawabu ya matukio kama hayo ya dharura yanayowakuta wabunge wa upinzani. Siyo tu, watumiwe kusaka ufumbuzi kwenye matukio bali wangehusishwa kuandaa program mpya ya kupambana na “watani” wao CCM.
Hakuna jambo lenye thawabu kama kutumia “busara”. Watu wenye busara hawaikimbii hoja bali wanazikabili ili wafuatiliaji wapate fursa ya kuamua upande upi umesimamia kwenye ukweli. Kukimbia hoja ni sawa na kuonyesha udhaifu wako katika kuhimili vishindo vya kisiasa.
Busara inajenga fikra na muono imara. Mwenye busara haoni aibu pale anaposhindwa katika majaribio na kwamba mwenye anayapa umuhimu mambo yenye tija.
Ni Muhimu kambi rasmi ya upinzani bungeni ingejitambua na “kusoma” maono wa Lowassa ili wajue ukimya wake tangu uchaguzi umalizike ana malengo gani! je kukimbia vikao vya Bunge na kutoka nje ndiyo kipaumbele ya kuing’oa CCM madarakani?
Ushauri mwingine ni kwamba Mbowe na kambi yake ya upinzani watumie busara ya kukubali kuwa Naibu Spika hatoi maamuzi kutoka mfukoni mwake bali anatumia sheria na kanuni zilizotungwa na Bunge yenyewe.
Wapinzani wajitambue na wafanye utafiti wa kina kujua watu wa kawaida wanaisemaje serikali ya Rais John Magufuli. Wasidhani kumsusia Naibu Spika ndiyo kutawabatilisha kifkra wapiga kura haraka haraka na kuanza kukejeli serikali.
Jambo jingine, wabunge waliofukuzwa kutoka kambi ya upinzani wakubaliane na matokeo. Hakuna taasisi yeyote isiyoongozwa bila kufuata sheria, kanuni na taratibu. Kambi ya upinzani itambue kuwa hata wao wakibahatika kushinda uchaguzi, ni sharti waheshimu sheria kanuni na taratibu zilizowekwa.
Hivyo Mbowe na kambi yake wafikirie mara mbili juu ya msimamo wao huo. Vinginevyo wataendelea kuwakosa wale wapiga kura wastaarabu wasiopenda vurugu zinazoashiria utovu wa nidhamu.
Sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) lisitumiwe kisiasa, watumie busara za wazee wao na Lowasa na Sumaye pamoja na Kingunge Ngombale Mwiru katika kutanzua matatizo yao na wajenge utamaduni wa kushauriana nao mara kwa mara.










