kadhalika, klabu imetangaza itafanya uchaguzi Juni 11, huku Kamati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yenyewe ikisema uchaguzi ni Juni 25.
TFF ilipewa agizo na Serikali kuitisha na kusimamia uchaguzi wa Yanga baada ya klabu hiyo kushindw akufanya hivyo kwa muda refu.
Hata hivyo, wiki iliyopita sekretarieti ya Yanga ilitangaza kutoutambua uchaguzi huo na kutangaza utaratibu wake.
Jambo hilo linawafanya wanachama wa Yanga wachanganyikiwe na kutofahamu upande upi uko sahihi hadi baadhi kufikia kusema hawajui mustakabali wa uchaguzi huo.
Mmoja wa wanachama wa klabu hiyo ambaye alikuwepo kwenye uongozi uliomaliza muda wake (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema kuwa mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo utawagawa wanachama.
"Sasa kama mamlaka mbili zote zinaendesha mchakato huu unategemea nini, huku ni kuwagawa wanachama, ni vyema busara ikatumika," alisema mwanachama huyo.
Aliongeza kuwa si sahihi kwa TFF kuendesha mchakato wa klabu hiyo na badala yake walitakiwa kuliacha jukumu hilo mikononi mwa klabu husika kwa kutumia kamati yake ya uchaguzi.
"Mimi nafikiri TFF wao walitakiwa kuwa wasimamizi, mchakato mzima tuuendeshe wenyewe," aliongeza mwanachama huyo.
Hata hivyo, wakati TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa ikisisitiza kuwa uchaguzi wa Yanga utafanyika Juni 25 na shirikisho hilo litausimamia, kwa sasa ni kama hakuna kinachoendelea kwa upande wao.
Wanachama hawaendelei kujitokea kuchukua fomu katika shirikisho hilo na badala yake walienda kuchukua fomu zinazotolewa na klabu yao.
Awali, wanachama tisa walijitokeza kuchukua fomu TFF, lakini baada ya Yanga kutangaza kuendesha uchaguzi wao, hakuna wanachama waliojitokeza kuchukua fomu TFF huku wale waliokwenda kuchukua awali wakikutana na rungu la adhabu ya kusimamishwa uanachama wa klabu hiyo.
Kusimamishwa kwa wenzao, kuliwafanya wanachama wengine wawe na hofu.
Adhabu hiyo ilielezwa na uongozi wa Yanga kuwa ni fundisho kwa wanachama wote wanaotaka kuhujumu uchaguzi wa klabu hiyo, na kusisitiza uchaguzi wao utasimamiwa na klabu.
Wakati mchakato unaoendeshwa na TFF ukiwa kama 'umesimama', tayari wanachama 19 wamepitishwa kuwania nafasi mbalimbali zilizotajwa huku wawili wakikatwa.
Jambo ambalo mashabiki wa soka wanasubiri kuona mwisho wake, ni uchaguzi gani utakuwa halali baada ya malumbano hayo yanayoendelea kati ya Yanga na TFF.
Kwa lugha nyingine ni nani 'ataufyata' kwa mwenzake, je ni TFF itaiachia Yanga iendeshe uchaguzi wake au Yanga watakubalina na uamuzi ya TFF kusimamia uchaguzi wao kama ilivyofanywa kwa wanachama wake wengine mwaka jana?










