Ilianza kwa kipigo cha mabao 3-0 Juni mwaka jana ikiwa na Mdachi Mart Nooij na juzi ikafungwa tena na 'kuzika' matumaini ya Stars kufuzu fainali hizo za Afrika ambazo mara ya mwisho kushiriki ilikuwa ni mwaka 1980.
Misri juzi ilifikisha pointi 10 ambazo haziwezi kufikiwa na Tanzania au Nigeria ambazo zimebaki kwenye kundi hilo kufuatia Chad kujitoa.
Stars na Nigeria kila moja ina pointi moja, hivyo mechi yao mwisho ya hatua ya makundi itakayochezwa Septemba mwaka huu itakuwa ni ya kukamilisha ratiba na kujenga heshima.
DAKIKA 15 ZA MAUAJI
Alikuwa ni Mohammed Salah anayecheza AS Roma ya Italia, aliyefunga mabao yote mawili katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Meye Bastrel aliyekuwa anasaidiwa na Mihundou Ganther na Vinga Theophile wote kutoka Gabon na kushuhudiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.
Dakika ya 43 straika huyo alifunga bao la kwanza kwa mkwaju wa adhabu baada ya beki Haji Mwinyi kufanya madhambi, huku lile la pili akimzidi nguvu na kumtoka Mwinyi na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Stars, Deogratius Munishi 'Dida' kudaka alilipachika wavuni dakika 15 baadaye.
Katika kuonyesha kuwa Stars haikuwa na bahati, nahodha wake na Mchezaji Bora wa Afrika, Mbwana Samatta alipiga juu penalti waliyopata dakika ya 53 na kumfanya mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon na Simba 'kuondoka' mchezoni.
MKWASA: PENALTI ILITUHARIBU
Kocha Mkuu wa Stars, Boniface Mkwasa alisema baada ya mechi hiyo kuwa kufutaia nahodha wake Samatta kupaisha penalti, kikosi kiliondoka mchezoni na kucheza chini ya kiwango zaidi.
Mkwasa alisema pia safu ya ulinzi ya timu yake haikuwa makini kwa kuruhusu wapinzani wao kuwatoka mara kwa mara na hatimaye kupata mabao hayo kirahisi.
Alisema bado wanajenga timu na kupoteza mechi hiyo, ni sehemu nyingine ya kuanza kwa mipango ya kukiimarisha kikosi hicho kwa ajili ya baadaye.
Aliongeza kuwa wapinzani wao Misri walistahili kupata ushindi katika mechi ya juzi, lakini amesikitika walifunga mabao kirahisi huku kiufundi waliizidi pia Stars.
CHAD ILIWARUVUGA
Kujitoa kwa Chad kwenye michuano hiyo ilichangia kuivuruga Stars, ambayo katika mechi ya kwanza iliyofanyika mjini N'Djamena walishinda mabao 2-1, kabla nchi hiyo haijatangaza kujiondoa kwenye michuano hiyo siku chache kabla ya mchezo wa marudiano uliotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam.
Baada ya Chad kujitoa, Misri ndiyo iliyoonekana kufaidika zaidi kutokana na yenyewe kufanikiwa kushinda katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Stars, kuifunga Nigeria na kutoka nayo sare waliporudiana na hivyo pointi ilizokatwa dhidi ya Chad, hazikuwaathiri.
Misri ilibaki na pointi saba na ushindi wa juzi uliwafanya wafikishe pointi 10, ambazo haziwezi kuwapeleka kokote.










