Kuifuta CUF si ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi Z’bar

05Jun 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Kuifuta CUF si ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi Z’bar

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), wamepitisha hoja binafsi wakitaka Chama cha Wananchi (CUF), kichunguzwe na kikibainika kinahusika na vitendo vya ubaguzi uliojitokeza Zanzibar kifutwe.

Spika wa BLW Zuberi Ali Mouludi

Hawajaishia hapo wanataka Katibu Mkuu wake Seif Sharif Hamad, almaarufu Maalimu Seif, achukuliwe hatua za kisheria.

Hoja hiyo imewasilishwa barazani kwa dharura na Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohamed said Bimwa, na kuungwa mkono na wajumbe baada ya kujadiliwa.

Mbele ya Spika wa BLW Zuberi Ali Mouludi, hoja ziliibuliwa za kutakiwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuchunguza vitendo vinavyodaiwa kufanywa na viongozi wa CUF baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio ambao waliususa.

Hatua ya CUF kususia uchaguzi wa marudio kwa madai haukuwa halali kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar na sheria ya uchaguzi namba 11 ya mwaka 1984, imesababisha kukwama kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).

Wajumbe watano walichagia hoja hiyo na kueleza kuwa hali ya kisiasa ya Zanzibar si shwari kutokana na kasi ya wananchi kubaguana katika nyumba za ibada, misiba, harusi, maulidi na kunyimana huduma za jamii madukani na ndani ya vyombo vya usafiri kwa sababu ya chuki za kisiasa.

Chimbuko la ubaguzi huo pamoja na kuhujumiwa mali za serikali na wananchi kama utekelezaji wa mpango wa kutomtabua Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, na viongozi wote, lilidaiwa ni wana CUF wakiongozwa na Katibu Mkuu Hamad.

Wawakilishi hao wanataka Hamad achukuliwe hatua za kisheria kwa kuhatarisha amani na umoja wa Wazanzibari kutokana na kampeni zake za kuwataka wananchi kugoma kulipa kodi pamoja na kutoshirikiana na serikali na wana CCM.

Hoja binafsi imesema waathirika wakubwa ni wana CCM ambao wanatengwa katika nyumba za ibada, maziko, harusi pamoja na kupata huduma nyingine za kijamii kama usafiri wa daladala.

Kuelekea Mwezi wa Ramadhani, unaoanza sasa, waumini wanahitajika kufanya ibada pamoja lakini, hali imekuwa tofauti hasa katika kisiwa cha Pemba ambayo ni ngome kuu ya kisiasa ya CUF.

Madhara ya mpasuko wa kisiasa yameanza pia kuathiri Watanzania Bara ambao pia wameanza kutengwa hasa wanaoishi katika nyumba za kupanga wakionekana kama ni sehemu ya wana CCM Zanzibar.

Lakini SMZ katika kupambana na tatizo hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Mohamed Aboud Mohamed, anasema hawatanyang’anya leseni za biashara wafanyabiashara watakaopatikana na hatia ya kutoa huduma kwa ubaguzi au kujaribu kufanya mgomo kwa sababu za kisiasa visiwani hapo.

Aliwambia wajumbe wa BL kuwa, SMZ imempiga marufuku Maalim Seif kuzunguka na misafara mirefu ya magari na kufanya mikusanyiko ya watu katika matawi au sehemu anazopita bila ya polisi kuwa na taarifa au kuwa na kibali.

Tayari watu watatu wameripotiwa kujeruhiwa katika vurugu zilizotokea vijiji vya Kivunge, Mkwajuni na Bumbwini baada ya askari wa kutuliza ghasia kutumia mabomu ya kutoa machozi, kuwatawanya wafuasi wa CUF waliojitokeza kumpokea Maalim Sefu akiwa katika ziara yake ya kwanza tangu kufanyika uchaguzi wa marudio.

Mpasuko huo uliibuka baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana kwa madai ulikuwa na udaganyifu pamoja na waangalizi wa ndani na nje kudai ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.

Baadhi yao ni Umoja wa Ulaya(EU) Jumuiya ya Madola Marekani na Uingereza.

Uamuzi wa ZEC unapigwa na CUF ambao walisusia uchaguzi wa marudio.

Tunajiuliza kwanini wananchi wateswe kwa maamuzi yaliyofanywa na Jecha na kufikia kunyimwa huduma muhimu za kijamii pamoja na kuhujumiwa mali zao yakiwamo majengo na mashamba ya mazao?

Lazima tukumbuke kwamba vitendo vya ubaguzi vinavyoendelea kufanyika Zanzibar hasa kisiwani Pemba havikubaliki katika misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana hakuharibiwa au kufutwa na wananchi wa Zanzibar tangazo la kuubatilisha lilitolewa na Mwenyekiti wa ZEC kwanini waadhibiwe Wazanzibari au Wabara wasiokuwa na hatia?

Pamoja na wawakilishi kutaka CUF ichunguzwe na Katibu Mkuu achukuliwe hatua za kisheria si ufumbuzi wa kumaliza mpasuko wa uchaguz mkuu wa Zanzibar.

Unaweza kuifuta CUF lakini watu wanaoiunga mkono huwezi kuwafuta wataendelea kuwepo na kubakia na misimamo cha muhimu ni kutafuta maelewano kwa njia za kidiplomasia na amani badala ya nguvu za dola.

Maridhiano bado njambo la muhimu katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar kwa vyama vya CCM na CUF pamoja na kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa marudio na kuundwa kwa serikali ya awamu ya saba Zanzibar.

Kuwataka wahisani kuongeza vikwazo au wananchi wasilipe kodi lazima hakusaidii , wanyonge Zanzibar ndiyo wataumia kwa ugumu wa maisha kwa kukosa na wala si viongozi wakuu.