Mamilioni TRA yaanza kuibadili shule iliyoezekwa nyasi Magu

05Jun 2016
Neema Emmanuel
Magu
Nipashe Jumapili
Mamilioni TRA yaanza kuibadili shule iliyoezekwa nyasi Magu

HATIMAYE michango ya wadau wa elimu zikiwamo Sh. milioni 45 zilizotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwenye Shule ya Msingi Lupemba iliyopo wilayani Magu, Mwanza imeanza kuipa muonekano mzuri shule hiyo ya Kijiji cha Bubinza.

Baadhi ya wanafunzi Shule ya Msingi Lupemba wakiwa kwenye darasa mojawapo lililojengwa kwa miti na nyasi kabla shule hiyo haijafungwa kupisha ujenzi. Hii ilikuwa Februari, 2016. (PICHA: Maktaba)

Shule hiyo iliyoanza kuripotiwa na gazeti hili Februari 7 mwaka huu ikiwa na utitiri wa changamoto ikiwamo wanafunzi wake wote (isipokuwa wa madarasa ya nne na saba) kusomea kwenye madarasa yaliyojengwa kwa miti na nyasi, imeanza kubadilika muonekano kutokana na shughuli za ujenzi zinazoendelea kufanyika kila uchao kwa ajili ya kuiboresha, shukrani zikienda kwa uongozi wa wilaya pamoja na wadau mbalimbali wakiwamo TRA.

Juzi, mwandishi wa Nipashe aliyefika shuleni hapo aliwashuhudia mafundi wakiendelea kwa kasi na harakati za ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu.

Awali, shule hiyo ilikuwa na vyumba viwili tu vya madarasa vilivyokuwa vikitumiwa na wanafunzi wa madarasa ya nne na saba wanaokabiliwa na mitihani ya taifa huku wengine wote wakisomea kwenye madarasa yaliyojengwa kwa miti na nyasi.

Hata hivyo, matunda yatokanayo na jitihada za kuboresha shule hiyo yameanza kuonekana baada ya kukamilika kwa vyumba viwili vya madarasa, kuendelea kujengwa kwa kasi kwa majengo mengine yenye vyumba vinne vya madarasa na pia kuanza kujengwa kwa ofisi ya walimu.

Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa kazi zinazoendelea kufanyika sasa shuleni hapo zimetokana na jitihada za pamoja za Mkuu wa Wilaya Karen Yunus, uongozi wa halmashauri ya wilaya na pia wadau wa elimu, hasa TRA waliochangia Sh. milioni 45.

“Tunaendelea vizuri… kwa kasi hii, naamini watoto wetu sasa watakuwa ni miongoni mwa wale waliobahatika kusomea katika shule bora zaidi za msingi zinazomilikiwa na serikali mkoani kwetu (Mwanza),” mmoja wa wazazi aliiambia Nipashe.

“Tunaomba Mungu usiku na mchana jitihada hizi za kuboresha shule hii zifanikiwe… madarasa yakamilike kwa asilimia mia moja na watoto wetu wapate madawati.

Tunasubiri wakati wa kuona watoto wetu wakisoma kwa amani na yale masuala ya kukalia matofali kwenye madarasa ya miti na nyasi yabaki historia,” aliongeza mzazi mwingine mwenye watoto wawili wanaosoma kwenye shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2006.

Mwalimu mkuu mpya wa shule hiyo, Paulo Mabiti, ambaye ametwaa nafasi hiyo kutoka kwa Daniel Matemi aliyehamishwa, alisema fedha walizopata kwa wadau wakiwamo TRA zimeelekezwa kujengea jengo moja lenye vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja.

Mabiti alisema walifanya mabadiliko ya mpango kazi kwa nia ya kuboresha zaidi shule hiyo, wakianza kwa kujenga jengo jingine la vyumba vya madarasa na baada ya kukamilisha watatumia fedha zitakazobaki kumalizia majengo yaliyokuwapo awali na ambayo ujenzi wake umefikia mahala pazuri.

Aliongeza kuwa harakati zote hizo zinafanyika baada ya kupokea ushauri kutoka kwa mhandisi wa wilaya, ofisi ya elimu pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya inayoongozwa na mkuu wa wilaya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Lupemba, Teleza Dotto, alisema kamati yao imepewa jukumu la kusimamia ujenzi huo na hadi sasa, wanaamini watakamilisha kazi hiyo vizuri kwa sababu wamejipanga vyema na pia huwa makini zaidi katika kusimamia miradi hiyo.

Alisema lengo lao ni kuona kuwa majengo yanakamilika kwa wakati ili hatimaye kumaliza kabisa kero ya kukosekana kwa vyumba vya kutosha vya madarasa.

Mjumbe mmojawapo wa kamati ya shule hiyo, Mashaka Fumbuka, alisema wanawashukuru wafadhili kwa kuwaunga mkono kwa hali na mali katika kushughulikia kero zilizopo na pia gazeti la Nipashe kwa kuwafikishia kilio chao kwa wadau wa elimu.

Alisema hadi sasa, tayari wana matumaini ya kuwa na madarasa sita na ofisi mbili za walimu na hivyo kuondoa uwezekano wa watoto wao kusomea tena kwenye madarasa yaliyojengwa kwa miti na nyasi.

OFISA ELIMU MAGU
Ofisa Elimu ya Msingi wa Wilaya ya Magu, Saryankanga Mageta, alisema wanatarajia kuwa kufikia Julai 30 mwaka huu, ujenzi wanaoendelea nao utakuwa umekamilika na wanafunzi kuanza kuyatumia madarasa hayo.

Alisema ijapokuwa fedha ilitolewa kwa ajili ya kumalizia majengo yaliokuwapo awali, lakini waliona haitakuwa bora kuchomeka fedha hizo kwenye majengo yaliyoanza na badala yake kuwaenzi TRA kwa kuanza majengo mapya wanayotarajia kuyakamilisha kwa fedha zitokanazo na mamlaka hiyo.

“Ujenzi utaenda kwa kasi kubwa kwa sababu fedha zipo, watu wakitoa pesa zao wanataka washuhudie kile kinachofanyika… ujenzi ukikamilika, kwa ujumla shule hii itakuwa na jumla ya madarasa nane na ofisi tatu,” alisema Mageta.

Alisema kuwa awali, shule hiyo ilikuwa na madarasa mawili yaliyojengwa kwa matofali na ofisi moja, lakini mchakato uliofanywa na gazeti lenu (Nipashe Jumapili), ulisaidia kupatikana kwa madarasa sita zaidi na ofisi mbili za walimu... nanyi tunawashukuru sana,” alisema Mageta.

ILIVYOKUWA
Awali, baada ya taarifa kuhusu hali mbaya ya miundombinu ya madarasa kuripotiwa na gazeti hili Jumapili ya Februari 7 mwaka huu, siku iliyofuata (Februari 8, 2016), uongozi wa Wilaya ya Magu uliamuru kufungwa kwa shule hiyo hadi yatakapopatikana madarasa yatakayotumiwa na wanafunzi wote waliokuwa hatarini kwa kusomea kwenye vyumba vilivyojengwa kwa miti na nyasi.

Hali hiyo iliwalazimu watoto wote kubaki nyumbani kwa siku 45 na kuwaacha wenzao wa madarasa yanayokabiliwa na mitihani tu (la nne na la saba) kuendelea na masomo katika vyumba viwili rasmi vilivyokuwapo.

Wakati wakiwa nyumbani, baadhi ya watoto walijikuta wakijihusisha na shughuli mbalimbali zikiwamo za kuchunga ng’ombe, kufanya biashara ya kuuza bamia na wengine kwenda kujihusisha na uvuvi.

Hata hivyo, siku chache baada ya gazeti hili kuripoti zaidi kuhusu adha inayowakuta watoto wa shule hiyo baada ya kufungwa kwa shule yao kwa kukosa madarasa ikiwamo kushinda porini wakichunga ng’ombe (toleo la Februari 20, 2016), uongozi wa wilaya ya Magu uliongeza nguvu zaidi na mwishowe kufanikiwa kujenga vyumba vya madarasa mawili yaliyofikia hatua ya kuezekwa.

Aidha, wadau zaidi waliendelea kujitokeza wakiwamo TRA waliochangia Sh. milioni 45 ili kujenga madarasa imara na pia kuboresha miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ofisi ya walimu, lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya kujifunza shuleni hapo.

RIPOTI KUHUSU SHULE YA LUPEMBA
1. Februari 7, 206 – Nipashe ilifichua kuwapo kwa shule ya Lupemba ambayo wanafunzi wake (isipokuwa wa madarasa ya nne na saba) walikuwa wakisomea kwenye madarasa yaliyojengwa kwa miti na nyasi. Habari hii ilibebwa na kichwa kisemacho: “Elimu bure mtihani mzito”.

2. Februari 20, 2016 – Nipashe iliandika kuhusu watoto wa Shule ya Msingi Lupemba walivyolazimika kuchunga ng’ombe wakati waliporudishwa nyumbani kwa muda usiojulikana wakisubiri kujengwa madarasa. Kichwa cha habari kilikuwa: ”Wanafunzi Magu wachunga ngombe wakisubiri madarasa kujengwa”

3. Machi 26, 2016 – Mkuu wa Wilaya ya Magu, Karen Yunus, aliripotiwa kumtisha mwandishi Neema Emmanuel wa Nipashe kutokana na mfululizo wa taarifa zake kuhusu hali ya Shule ya Msingi Lupemba. Mkuu huyo alikuwa akimlalamikia mwandishi kuwa anataka kumharibia kazi hasa kutokana na namna anavyoiripoti shule hiyo. Habari hiyo ilibebwa na kichwa cha habari kisemacho: “DC amtisha mwandishi kufichua wanafunzi kuchunga ng’ombe Magu”.

4. Machi 27, 2016 – Nipashe iliripoti habari njema kuhusu kuanza kujengwa kwa vyumba vipya vya madarasa, ikiwa na kichwa cha habari kisemacho: “Hatimaye madarasa shule ya wanafunzi wachungao ng’ombe Magu yaanza kujengwa”

5. Aprili 3, 2016 – Nipashe iliripoti kuhusu kukamilika kwa kazi ya kuezeka vyumba viwili vipya vya madarasa na kurejea shuleni kwa wanafunzi waliokuwa wakichunga ng’ombe wakisubiri madarasa kujengwa. Hii ilibebwa na kichwa cha habari kisemacho: “Wanafunzi waliokuwa wakichunga ng’ombe Magu warudi darasani.

6. Aprili 10, 2016 – Habari ndani ya Nipashe katika siku hiyo ilieleza kuhusu matumaini ya wanafunzi wa Lupemba kununuliwa madawati. Kichwa ha habari kilisema: “Madawati yanukia shule ya wanafunzi waliokuwa wakichunga ng’ombe Magu

7. Mei 15, 2016 – Nipashe iliripoti kuhusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuichangia fedha Shule ya Lupemba kiasi cha Sh. milioni 45.