Baba anapotaka kumaliza hasira zake kwa muuaji wa binti yake

04Jun 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Baba anapotaka kumaliza hasira zake kwa muuaji wa binti yake

NI kama sinema, lakini ni kweli,Baba wa binti aliyeuliwa na mtu mwenye rekodi ya makosa ya ngono alijikuta akipaa juu ya meza kwa ghadhabu na kujaribu kumshambulia muuaji huyo wa mlolongo aliyekuwa akimkejeli kwa kicheko mahakamani baada ya kuwa amehukumiwa adhabu ya kifo juzi.

Van Terry ‘akipaa’ juu ya meza ndani ya mahakama kumvaa muuaji wa binti yake, Michael Madison, dakika chache baada ya jaji kutangaza kutolewa kwa adhabu ya kifo.

Michael Madison alihukumiwa adhabu ya kifo kufuatia kupatikana na hatia ya kumuua binti mwenye umri wa miaka 18, Shirelda Terry, na wengine Angela Deskins, 38, na Shetisha Sheele, 28, mjini Ohio, Marekani mnamo Julai 2013.

Hiyo juzi, baba yake Shirelda, Van Terry, alikuwa akizungumzia machungu yanayomkabili kuhusiana na kumkosa binti yake huyo baada ya Madison kuwa ameshahukumiwa kifo wakati alipojikuta akishindwa kujizuia na ghafla akaondoka mbio na ‘kupaa angani’ kumvaa muuaji huyo. Hali iliyozua sekeseke mahakamani hapo.

Madison, 38, alionekana akicheka tu wakati wasaidizi kwenye chumba cha mahakama hiyo ya Kaunti ya Cuyahoga wakijitahidi kumshika na kumdhibiti ili kumzuia na baadaye kumtoa nje baba huyo aliyekuwa amejawa na ghadhabu.

Terry aligeuka, akasita na kuanza kumvaa Madison huku maofisa wa polisi wakihaha kumrudisha nyuma.
Usikilizaji wa kesi hiyo uliendelea baada ya Terry kuwa ameshaondolewa ndani ya chumba hicho cha mahakama.
Na Madison hakuonekana kuumia kwenye songombingo hilo.

Sakata hilo lilianza dakika chache tu baada ya Madison kuhukumiwa kifo kwa mauaji hayo ya mwaka 2013.
Miili ya Shirelda, Angela na Shetisha ilipatikana imefungwa kwenye mifuko ya kuwekea uchafu karibu na makazi kwenye jengo moja huko East Cleveland ambapo Madison alikuwa anaishi Julai 2013.

Mfanyakazi mmoja wa kituo cha televisheni aliripoti kuwepo kwa harufu ya kitu kilichooza iliyokuwa ikitokea kwenye sehemu moja ya kuegeshea magari ambayo ilikuwa pia inatumiwa na Madison kwenye jengo hilo.

Ndani ya gereji hiyo, polisi waligundua mwili uliooza wa mwanamke mmoja uliokuwa umewekwa ndani ya mifuko ya uchafu iliyofungwa.

Siku iliyofuata, wachunguzi walikuta miili mingine ikiwa sehemu ya chini ya nyumba moja iliyokuwa tupu na kwenye sehemu ya nyuma ya nyumba moja jirani.

Baada ya kukamatwa, Madison aliwaeleza polisi kwamba aliwanyonga wawili kati ya wanawake hao lakini alikuwa hakumbuki kumuua huyo wa tatu.

Jaji kwenye mahakama hiyo ya Cuyahoga, Nancy McDonnell, alikubaliana na pendekezo la jopo la washauri wa mahakama hiyo kwamba Madison ahukumiwe adhabu ya kifo.

Mwanamama huyo badala yake angeweza kuchagua kumhukumu Madison kifungo cha maisha gerezani bila msamaha, lakini aliona hiyo adhabu stahili.

Jaji McDonnell alisema hali ya kutisha ya uhalifu uliofanywa na Madison ilikuwa haiwezi kupozwa na ushahidi ulitolewa kwenye jitihada za kumuokoa adhabu hiyo ya kifo, ikiwemo kutolewa kwa madai ya kunyanyaswa na malezi mabovu wakati wa utoto wake.

Madison pia alipatikana na hatia mwezi uliopita kwa matukio kadhaa ya mauaji na utekaji nyara.

Hata hivyo, utekelezaji wowote wa adhabu hiyo ya kifo unaweza kuchukuliwa miaka kadhaa baadaye kwa sababu ya mlolongo mrefu wa rufaa. Mbali na hilo, mji huo wa Ohio pia una ukosefu wa madawa yanayotumika kwenye kwenye utekelezaji wa dhabu hiyo.

Wanasheria wa Madison hawakusumbuka kumtetea mteja wao kwamba hakuwa na hatia, badala yake walijitahidi kukoa maisha yake kwa kuwasilisha ushahidi kwamba muuaji huyo alipata madhara ya kudumu ya kisaikolojia kutokana na manyanyaso aliyoyapata akiwa bado mdogo.

Kulikuwepo na ushahidi kwamba Madison alinyanyaswa na mama yake mtumiaji wa dawa za kulevya, baba yake wa kambo, baadhi ya marafiki wa kiume wa mama yake na watu wengine wa familia yake.

Mwanasheria wa utetezi David Grant alimueleza jaji juzi kwamba historia ya unyanyaswaji na malezi yake mabovu haviwezi kuwa sababu ya kile kilichotokea lakini vilikuwa vinatoa msingi wa kuelewa aina ya mambo ambayo Madison alijikuta akizungukwa nayo.

Hata hivyo, upande wa waendesha mashtaka walipinga wakati wote wa kesi hiyo kwamba Madison alikuwa anastahili kufa kwa sababu ya mazingira yaliyokuwa yanazunguka mauaji hayo.

Adhabu ya kifo ‘itatuma ujumbe kwa jamii kwamba hukumu kali sana itatolewa kama utatokea uhalifu kama huo,' Christopher Schroeder, mwendesha mashtaka msaidizi wa Kaunti ya Cuyahoga, alimueleza jaji huyo.

Madison aliwekwa kwenye orodha ya wahalifu wa ngono mwaka 2002 wakati alipohukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani kwa jaribio la kubaka.

Kugundulika kwa miili ya wanawake hao watatu mwaka 2013 kulishtua taifa juu ya uwezekano kwamba muuaji mwingine wa mlolongo kama Anthony Sowell alikuwa akiua wanawake ndani na kando kando ya mji ya Cleveland.

Sowell alipatikana na hatia mwaka 2011 na kuhukumiwa kifo kwa mauaji ya wanawake 11 ambao miili yao ilipatikana kwenye nyumba yake huko Cleveland. Mahakama ya Juu ya Ohio inatafakari kama iendelee na hukumu hiyo.