unaoletwa na lehemu kuganda ndani ya viungo na mishipa ya damu.
Dawa hiyo inazalishwa kutoka kwa kuku wa GM ambaye mayai yake ndiyo yanayotengeneze tiba hiyo, ripoti ya hali ya biashara ya mazao ya GMO duniani iliyotolewa wiki hii, imeeleza. Inaongeza kuwa pamoja na kupata dawa hizo, bidhaa nyingi za GMO zimekubalika na wataalam wa lishe na afya na vibali vimetolewa kuuzwa sokoni bila kipingimizi. Mazao hayo ni pamoja na kitoweo cha samaki au nguruwe , viazi pomoja na matunda.
Marekani ambayo ni kitovu cha teknolojia ya uhandisi jeni unaozalisha bidhaa za GM, imepata mafanikio mengi ya kujivunia kuanzia ugunduzi na uidhinishaji wa matumizi ya mayai hayo ya GM kutengeneza dawa za kutibu taka sumu za lehemu zinazosababisha magonjwa ya figo na moyo, hadi kupata jamii ya ‘nguruwe wasioshambuliwa na maradhi.’
Wiki hii, jukwaa la kimataifa la upatikanaji na utumiaji wa bayoteknolojia katika kilimo, (International Service for the Acquisition of Agri-Biotech Application- ISAAA), liliwasilisha ripoti inayohusu mafanikio na biashara ya mazao yanayozalishwa kwa kutumia bayoteknolojia au uhandisi jeni.
Ripoti hiyo ambayo Nipashe ina nakala yake imezungumzia mafanikio yanayopatikana kwenye ugunduzi na uboreshaji wa mazao ya chakula na wanyama ambayo sasa yanaanza kuuzwa sokoni na kuliwa huko Marekani, baada ya tafiti kuthibitisha kuwa binadamu.hakuna athari kwa
MAFANIKIO KITIBA
Mamlaka ya udhibiti wa chakula na dawa ya Marekani ( FDA imeruhusu uzalishaji wa kuku wa GM ambao mayai yake yanatumika kutengeneza tiba ya ugonjwa ambao haujapata tiba muafaka wa lysosomal acid lipase deficiency (LALD).
Haya ni maradhi yanayotokana na ukosefu ama matatizo ya kimeng’enya, au mwili kushindwa kuchakata vyakula vya mafuta na matokeo yake mafuta kujikusanya kwenye viungo hasa ini na wengu na kusababisha maradhi yanayoambatana na saratani kwenye viungo hivyo, kwa mujibu wa taarifa.
Inaeleza zaidi kuwa kwa upande mwingine lysosome humeng’enya kolestro ama lehemu na iwapo inapungua mafuta hayo mabaya hujazana kwenye mishipa ya damu na viungo kama moyo na kusababisha vifo kutokana na moyo kusimama ghafla hali inayoitwa (cardiac arrest), huleta pia sarati za ini na figo kufa.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa huko Marekani ulaji wa vyakula vya GMO ikiwamo nyama, matunda na mazao mengine ni ruksa na tayari taasisi ya kudhibiti ubora wa vyakula na Dawa ya nchi hiyo imeruhusu kuingizwa sokoni na kutumiwa.
Bidhaa hizo ni viazi mvirongo vyenye nasaba kadhaa ambavyo kitaalamu vimeitwa ‘multi trait potatoes’ ambavyo vinaruhusiwa kuliwa na kuuzwa sokoni. Viazi hivi havishambuliwi na ‘fangas’ kwa kuwa tangu mwanzo maradhi makubwa ya mazao hayo ni magonjwa yanayosababishwa na fangas zinazoleta kuoza, kuwa vigumu na kuharibika ama viazi au majani na shina.
Kadhalika yapo ‘maepo’ au matufaa ‘arctic apples’ ambayo hayana vidonda na pia hayabadiliki rangi na kuwa ya kahawia yanapokatwa ama kung’atwa yakiliwa, sasa mbegu zake zinaruhusiwa kuoteshwa Marekani na Canada.Wateja wataanza kunufaika na matunda hayo mwakani.
“Kampuni iliyozalisha matunda hayo ya GM ya Okanagan Specialty Fruits ya Canada, inaendelea kutafiti na kutengeneza piches na peasi za GM na kuongeza orodha ya matunda bora yasiyoharibika.”
Taarifa inasema pamoja na hayo taasisi ya kudhibiti ubora wa vyakula na dawa FDA , Novemba mwaka jana imeruhusu Wamarekani kula kitoweo cha samaki wa salmon ‘jodari’ waliozalishwa kwa teknolojia ya GMO.
Samaki hao watavunwa haraka kwa muda wa mwaka 1.5 ikilinganishwa na wale wasiobadilishwa nasaba wanaotumia miaka mitatu kukomaa na kuliwa.“Hii ni kama nusu ya muda uliozoeleka wa kukuza samaki hawa mabwawani,” inaongeza ripoti.
Aidha inaongeza kuwa teknolojia ya uhandisi jeni, imewezesha uboreshaji wa nasaba za nguruwe wa GM ambaye hashambuliwi na maradhi hatari ya virusi ambayo pia yanawaathiri wanadamu.
Kadhalika huko Marekani chakula cha mifugo majani ya ‘alfalfa’ ambayo yana viini lishe vingi na bora zaidi na yanayoyeyuka kwa wepesi tumboni na mwilini, kiligunduliwa na kuruhusiwa kutumika kuanzia mwaka 2014.
Marekani kwa mujibu wa ripoti hiyo inayotoa taarifa kuanzia mwaka 1996 hadi 2015 , inaonyesha kuwa ndilo taifa linaloongoza kwa mazao ya GM inayolima soya, pamba, alfafa, mapapai na viazi mviringo.
Brazil pia iko juu ikilima soya, pamba na mahindi, China imo, inazalisha zaidi pamba, wakati Afrika Kusini inalima pamba, mahindi na soya . Burkina Faso inazalisha pamba kwa wingi na wakulima wake wameuaga umaskini. Kwa ujumla mataifa yote huzalisha zaidi mahindi na pamba.
Taarifa hiyo ambayo kwa Tanzania inaratibiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ilizinduliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuki, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), ambachoo ni mdau mkuu wa taaluma , tafiti na uendeleza wa kilimo nchini.
Taarifa inataja tafiti za kudhibiti magonjwa, kuboresha nasaba za mimea na wanyama na kupata viumbe wenye sifa madhubuti ambazo ni pamoja na kukomaa haraka, kutokushambuliwa magonjwa ya virusi na bacteria.
TANZANIA INAHITAJI GMO?
Kwa ujumla inaonekana kuwa japo bidhaa za GM ama zinaogopwa au kupingwa vita na serikali nyingi za Afrika ukweli ni kwamba viongozi na raia wa mataifa haya wakizuru Marekani au Canada watakula vyakula na kuvaa nguo za GM.
Lakini kikubwa kinachojitokeza ni tiba mpya ya mayai ya GM yatakayotumiwa kuzalisha dawa za kuondoa lehemu, kutibu ini na figo ni kitu kisichokwepeka maana dawa ni uhai na maisha hayana mbadala, hayupo atakayaweza kukwepa dawa hii hata kama nchi yake hairuhusu GM.
Japo baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wanahamasisha ubaya wa mazao ya GM , wanasahau kuwa sindano ya insulin anayochomwa mgonjwa wa kisukari inatokana na teknolojia ya GMO ya kutumia insulin ya wanyama wakiwamo nguruwe,mbwa au ng’ombe.
Lakini kabla ya ugunduzi huo ni kwamba watu waliokuwa wakiugua kisukari aina ya kwanza (Type I) walikufa kwa sababu mwili haukuweza kutumia sukari kutengeneza nishati na nguvu ili kufanya kazi.
Historia ya tiba hii kwenye mitandao inaeleza kuwa mwaka 1921, mtafiti wa Canada alichuja insulin kutoka kongosho ya mbwa na kuanza kupata tiba za kusaidia kisukari hicho ambacho mtu huzaliwa akiwa hana inslun mwilini. Tafiti ziliendelea kwa kutumia kichocheo hicho kutoka kwenye kongosho za ng’ombe na nguruwe.
Lakini pia katika miaka ya 1980 watafiti wa bayoteknolojia walitambua jeni za insluni kwenye seli za binadamu na kwa kutumia teknolojia hiyo waliingiza jeni za insulin ya panya kwenye jamiii ya bacteria na kuzalisha insulin inayotumiwa sasa.
Kwa kulingana na tafiti na mabadiliko ya kitekinolojia huenda kabla ya kufikia miaka ya 2050 teknolojia hiyo itakuwa inatumiwa duniani bila kipingamizi, kama ilivyotokea kubadili mfumo wa analojia na kuingia dijitali. GM italenga kupata ufumbuzi wa matatizo mengi ya kiafya , kilimo na lishe, kupata tiba , chanjo na kwa ujumla kukabiliana na changamoto za kuwezesha wanadamu kupata mahitaji ya kila siku.
Kwa Tanzania mabadiliko ya tabianchi yanaashiria uhaba wa chakula na malisho ya wanyama, ukosefu wa maji, misitu ya kuchoma mkaa na kuni lakini pia kitisho kikubwa kinakuwa ongezeko la wadudu waharibifu na maradhi yote haya yanakutana na ongezeko la watu lisiloweza kuhudumiwa na rasilimali zilizopo.
Ndiyo maana kuna haja ya kutumia tafiti za GM kwa kutumia watafiti wa ndani ili kujibu maswali yanayoikabili jamii kwa kuanza ni vyema kuelekea kwenye maeneo yaliyotafitiwa kama pamba, mahindi, mapapai, vyakula vya mifugo na wanyama ili kuwa na na mahitaji ya Tanzania.
Watafiti wa Costech na Jukwaa la Bayoteknolojia wanasema licha ya tafiti na gunduzi nyingi kufanyika sehemu nyingine duniani, siyo rahisi kustawisha mbegu za taifa jingine bila kuzifanyia utafiti na kuziboresha kulingana na mazingira na mahitaji ya nchi husika.
Wanasayansi hawa wanasema mbegu za GM za China haziweza kupandwa Tanzania bila kuboreshwa kuendana na mahitaji. Mathalani, ugunduzi ulilenga kupata mbegu zinazokomaa mapema, kwa Tanzania utatafiti mbegu za mahindi zinazotumia maji kidogo na kuhimili ukame. Hivyo,utaziwekea mbegu hizo nasaba zinazoweza kupandwa popote hata kama ni mikoa yenye ukame.
Kadhalika kama ni kuokoa misitu jitihada za teknolojia ya GM inalenga kupata miti inayokomaa na kuvunwa haraka, inayohimili ukame ili kuipanda nchi nzima kwa lengo la kuhifadhi mazingira, kupata nishati na kuongeza uoto wa asili.










