Chimbuko la mpasuko wa kisiasa ni hatua ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi huo, kwa maelezo mengine kama wapinzani kujitangazia matokeo.
Kitendo cha kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu kilisababisha chama cha CUF kususia kushiriki uchaguzi wa marudio kwa madai uchaguzi uliotangulia ulikuwa huru na wa haki na kusababisha mkwamo wa kuundwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pamoja na vyama vingine kushiriki katika uchaguzi huo vilishindwa kufikia mashariti ya katiba ya kupata asilimia 10 ya kura za urais ya kuunda SUK.
Hata hivyo, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, ameamua kuwakaribisha viongozi wakuu wa vyama vya upinzani vyama Tadea akimteua Juma Ali Khatib , kadhalika Said Soud Said wa AFP na Hamad Rashid Mohamed wa ADC kuwa mawaziri katika serikali yake.
Lakini pamoja na kufanyika kwa uteuzi huo bado mapasuko wa kisiasa umeendelea kujichimbia mizizi na kubakia kama ulivyokuwa kutokana na vyama vya CCM na CUF kuwa na uwakilishi mkubwa.
Msimamo wa CUF wa kutomtambua Rais wa Zanzibar Dk Shein na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar umerejesha chuki ya kisiasa na watu kuanza kubaguana kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kabla ya maridhiano na kuzaliwa SUK mwaka 2010.
Wananchi katika Kisiwa cha Pemba wanabaguana katika nyumba za ibada, maziko, harusi, kuoana pamoja na utoaji wa huduma madukani, usafiri na kuwafanya wanachama wa CCM kuwa katika wakati mgumu.
Kutokana na hali hiyo serikali imeanza kuchukua hatua kama kufuta leseni za biashara kwa magari matano ya abiria yanayodaiwa kutoa huduma kwa ubaguzi kwa sababu ni kinyume na masharti ya biashara.
Mbali na vitendo vya kubaguana pia mashamba manne ya viongozi CCM na serikali yameripotiwa kuhujumiwa baada ya watuhumiwa kukata mikarafuu, migomba na kufyeka mpunga kwa sababu za kisiasa.
Bahati mbaya wananchi wanaobaguana ni watu wanaofahamiana na wanaishi katika kijiji kimoja au mtaa mmoja lakini chuki za kisiasa zimewafanya kususiana hata misiba.
Wanachama wa CCM ndiyo wamekuwa wathirika wakubwa ikiwamo kususiwa misikiti kunyimwa huduma ya usafiri wa daladala na wakati mwingine wananchi kugoma kula chakula harusini mpaka wanachama wa CCM waondoke katika shughuli hizo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud, anasema serikali haitawafutia leseni wafanyabiashara wote ambao watabainika kutoa huduma kwa ubaguzi kinyume na mashariti ya lesseni.
Anasema vitendo hivyo vya ubaguzi vilivyojitokeza vinakwenda kinyume na utu na misingi ya haki za binadamu na kuwataka wananchi kudumisha amani na umoja wa kitaifa.
Pamoja na vitendo vya ubaguzi kuendelea kushika kasi hasa Pemba viongozi wa dini, vyama vya siasa, asasi za kiraia vimeshindwa kuvikeme.
Kwanini asasi za kiraia zimekaa kimya na kuachia vitendo vya ubaguzi vikiendelea kufanyika kwa sababu tu ya chuki za kisiasa na kutesa watu wasiokuwa na hatia Zanzibar.
Kama Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ulifutwa na Mwenyekiti wa Zec kwa sababu mbali mbali kwanini wateseke watu wengine wasiokuwa na hatia mpaka kufikia kunyimwa mahitaji muhimu madukani kama dawa na vyakula.
Zanzibar kuna asasi nyingi za kiraia ikiwamo Jumuiya ya Maimamu Zanzibar(Jumaza) (Chama cha Wanasheria Zanzibar(ZLS) Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLCS) Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) pamoja na Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar (ZAFELA). Wote ni watazamaji.
Wakati umefika kwa asasi za kiraia na viongozi wa dini kukemea vitendo vya ubaguzi vinavyoendelea kufanyika kutokana na chuki za kisiasa bila ya kuangalia madhara yake.
Hakuna njia ya kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar zaidi ya kuwapo maridhiano baina ya pande mbili zinazovutana CUF na CCM.
Kama Rais mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, aliweza kufanya maridhiano na kuzaliwa SUK viongozi wengine wansshindwa vipi kumaliza mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar? Mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar hauwezi kumalizika bila ya kuwapo kwa Srikali ya Umoja na shirikishi kutokana na vyama vya CCM na CUF kuwa ndiyo vinavyoungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi.
Bila ya viongozi wa vyama kutumia busara na hekima uchumi wa Zanzibar utatetereka kutokana na matatizo ya kisiasa na migomo kama itaendelea kufanyika katika sekta ya biashara na huduma.










