11 bora timu za mikoani 2015/16

23May 2016
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
11 bora timu za mikoani 2015/16

WIKI iliyopita kulikuwa na makala ya wachezaji 11 bora wa kigeni waliosajiliwa na klabu mbalimbali kwa ajili ya kucheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2015/2016 iliyomalizika jana kwenye viwanja nane tofauti hapa nchini.

Beno Kakolanya - Prisons

Kabla ya kutoa kikosi bora kwa msimu uliomalizika wa ligi, leo tutakuwa na kikosi bora cha timu zilizoshiriki ligi hiyo kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam.

Mara nyingi kinapotangazwa kikosi bora cha msimu wachezaji wengi bora kutoka klabu mbalimbali ndogo au za mikoani hawapati nafasi.

Mara nyingi nafasi hupata wachezaji wa klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC kwa sababu timu hizi ndizo hucheza ligi moja kwa moja zikisaka ubingwa na hufukuzana kwenye msimamo.

Hata hivyo, kwenye timu zingine huwa kuna wachezaji walioonyesha viwango vya juu, lakini huwa vinafichwa na umaarufu wa timu kubwa.

Kwa kufuatilia viwango vya wachezaji wa timu za mikoani, hawa ni wachezaji 11 bora kabisa kwa mujibu wa mwandishi wa makala haya.

1. Beno Kakolanya - Prisons
Ni mmoja wa makipa waliotia fora katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara. Mbali na urefu wake akiwa kipa pekee mrefu kuliko wote kwenye ligi, lakini pia ana uwezo mkubwa wa kukokoa michomo.

Ameifanya Tanzania Prisons kuwa ya kutisha hapo ilipofikia, ikiwa kwenye nafasi za tano bora, tofauti na msimu uliopita iliponusurika kushuka daraja.

Wengi watamkumbuka jinsi alivyowahenyesha washambuliaji wa Simba kwenye mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, ilipopata bao zikiwa zimebaki dakika tatu mechi kumalizika.

Hapana shaka kuwa ndiye kipa namba moja wa timu zilizo nje ya Dar es Salaam. Na kwa kuthibitisha hilo, ameitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars).

2. Salum Kimenya - Prisons
Ni beki namba mbili sahihi kuchaguliwa kwenye kikosi hiki kutokana na kazi kubwa anayoifanya.

Ana uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi, kupiga krosi, kufunga na pia kuwazuia mawinga machachari.

Ameifanya Prisons kuwa moja ya timu ngumu kufungika msimu huu, lakini pia ikiwa haijafungwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Sokoine mjini Mbeya.

3. Hassan Mwasapili - Mbeya City
Anafahamika kuwa moja ya mabeki machachari kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ana mbio, chenga na uwezo wa kusaidia mashambulizi. Pia ni mkakamavu na mbishi, kitu ambacho kinamfanya kumtofautisha na mabeki wengine wa kushoto. Beki huyu wa Mbeya City anastahili kuwemo kwenye kikosi hiki.

4. Andrew Vicent -Mtibwa Sugar
Wenyewe mashabiki wa soka Morogoro wanamwita 'Dante'. Ni mmoja wa mabeki ving'ang'anizi wa Mtibwa Sugar, anayetumia nguvu inapobidi na akili inapohitajika.

Mashabiki wa soka walishuhudia burudani safi pale walipopambana na mshambuliaji hatari wa Yanga, Donald Ngoma kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu kwenye Uwanja wa Taifa.

Ni beki pekee ambaye alionekana kumudu kumzuia kwa maarifa zaidi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.

5. David Ossuman- Stand United
Ndiye mchezaji pekee wa kigeni kwenye kikosi hiki. Ni beki wa kati ya Stand United aliyeifanya timu hiyo kuwa na ukuta mgumu kupenyeka.

Kuna taarifa kuwa klabu ya Simba imeanza kumnyemelea. Alisajili wa klabu hiyo kutoka Olympique Sports Abobo ya Ivory Coast. Kwenye kikosi hiki anasimama kama beki wa kati.

6. Abadallah Seseme -Toto Africans
Ni mchezaji wa zamani wa timu ya Simba. Kwa sasa anaichezea Toto Africans. Amekuwa na msimu mzuri kiasi cha kuwa mmoja ya wachezaji wanaowaniwa na Mbeya City.

Pamoja na kwamba timu yake haikufanya vizuri sana, lakini kiwango chake binafsi kimeonekana kupanda, tofauti na alivyokuwa Simba.

7. Shiza Kichuya - Mtibwa Sugar
Huyu ni winga machachari na msumbufu. Anaichezea Mtibwa Sugar na tayari ameshafunga magoli nane kabla ya mechi ya jana.

Uwezo wake, kasi, chenga za maudhi na uwezo wa kupachika mabao umemfanya kuanza kuhitajika na baadhi ya timu kubwa na kongwe za Ligi Kuu.

Simba, Yanga na Azam zimeshaanza kuitaka saini yake. Yumo kwenye kikosi hiki.

8. Miraji Athumani- Toto Africans
Ni mchezaji wa kikosi cha pili cha Simba anayechezea kwa mkopo Toto Africans. Klabu hiyo imepanga kumrejesha ili acheze kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.

Ni mmoja kati ya wachezaji wa timu za mikoani waliofanya vizuri sana msimu huu kwenye ligi.

Pamoja na uchanga wake kwenye soka, lakini ameonyesha kuwa kiungo mwenye uwezo wa kufunga magoli, kitu kinachowashinda wachezaji wengi wa kizazi cha sasa kwenye nafasi hiyo, hasa wa Kibongo. Ameshafunga magoli matano mpaka sasa kwenye Ligi Kuu.

9. Elius Maguri- Stand United
Kwenye kikosi hiki anasimama kama namba tisa. Ni mshambuliaji ambaye amefanya vizuri zaidi msimu huu kuliko wowote ule mwingine.

Amefunga jumla ya magoli 14 na kuwa mmoja wa washambuliaji wa Kitanzania waliofunga magoli mengi msimu huu akiwa na Stand United.

Kama angecheza mechi nyingi zaidi idadi ya magoli ingeweza kuongezeka, lakini kuna wakati alisimamishwa na kocha Patrick Liewig kutokana na utovu wa nidhamu, pia kutoroka kwenda kwenye majaribio nje ya nchi bila baraka za Mfaransa huyo.

10. Atupele Green- Ndanda FC
Ameotokea kuwa mshambuliaji hatari wa Kibongo kwa sasa. Ana uwezo wa kukaa na mpira, pia kupambana na mabeki wakorofi kutokana na nguvu alizojaaliwa kuwa nazo.

Beki mtukutu wa Yanga Kelvin Yondani amekiri kupata shida kila anapokutana na mshambuliaji huyo wa Ndanda. Zipo taarifa za kutakiwa na klabu ya Simba. Naye anastahili kuwa kwenye kikosi hiki.

11. Jeremiah Juma- Prisons
Kwa mfumo wa 4-3-3, ambao hutumika washambuliaji watatu mbele, Jeremiah Juma atasaidiana na Maguri na Atupele.

Mshambuliaji huyu wa Prisons amekuwa kwenye msimu mzuri kwa kupachika magoli 14. Uwezo wake mbali na kuifanya Prisons kuwa timu tishio msimu huu, lakini pia umemfanya kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars.