Pamoja na kuujua ukweli huo,hatupambani na rushwa bali tunaongea tu kulinda nafasi zetu kwa kuonyesha eti sisi ni wapambanaji wa adui huyo.
Rushwa haichukuliwi kuwa jambo la aibu. Wanaojihusisha nayo huheshimika kwani ni aghalabu huwa na uwezo mkubwa kifedha zaidi ya ilivyopaswa na mara nyingi watu hao wamekuwa wakisifiwa kuwa na akili nyingi kwa kutumia ofisi zao kutajirika haraka lakini wanaoishi kwa vipato halali na kufanikiwa kwa kasi ndogo huonekana wajinga wasioweza kuitumia nafasi vizuri!
Ukifanya uchunguzi wa kina, sehemu mbalimbali za utumishi wa umma wanaopata kashkash kubwa ni wale wanaodai kwamba wenzao ni wala rushwa.
Hawa huonekana kuwa wapika majungu, vinaa, watu hatari katika ofisi wa kuhamishwa au ikibidi wa kuundia zengwe wafukuzwe kazi! Wanaonekana wana wivu wa kichawi kwa wenzao wanaondelea kwa rushwa.
Washirika wa rushwa maofisini hujisifu kwamba wao ni wachapa kazi wakubwa na kuwatangaza wasio washirika wao kwenye rushwa kwamba si watenda kazi.
Mapambano ya kweli ya rushwa yatafanikiwa kama jamii yetu itaichukulia rushwa kwamba ni jambo baya, ovu,chafu, la aibu, la hatari na kuwaona watu wanaofanikiwa kwa pesa ya rushwa ni wabaya, waovu, wachafu, wanaotia aibu na wa hatari.
Huko maofisini watu wanaoona rushwa ikitembea wajengewe ujasiri wa kufichua vitendo hivyo kwa mamlaka husika.
Na mamlaka hizo zipambane kikamilifu na rushwa. Halafu, watu wanaojihusisha na rushwa watiwe kashkash ya nguvu mpaka jamii izoee kwamba rushwa ni adui na uadilifu ni rafiki.
Hatuwezi kupambana na rushwa kikamilifu bila kuiweka hiyo rushwa kwenye upande hasi. Lakini kwa sasa, hapana ni siasa tu. Hebu tuache unafiki.
Kiongozi anaongea kwa nguvu kukemea rushwa lakini kuna watendaji chini yake wanaishi kirushwarushwa hawafanyi chochote! Akitokea mtu kuwabana, mtu huyo anaundiwa zengwe kuondolewa kwa kutumbuliwa kama jipu! Hapo ndipo ninapoamini kwamba kamwe hatupambani na rushwa bali tunaongea siasa tu.
Inawezekana hata baadhi ya majipu yanatangazwa hivyo kwa sababu ni wapambanaji wa rushwa kikweli kweli. Hebu ona hii.Nimeshatumia usafiri wa daladala Dar, Tanga, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Morogoro.
Ukiondoa Morogoro, kwingine kote daladala (kwa majina tofauti mji na mji), huogopa sana kuvunja sheria na wakivunja sheria huchukuliwa hatua mara moja na mamlaka zinazohusika.
Daladala nyingi za Morogoro zinaishi kwenye dunia yake ya pekee! Wengi wao wanaweza kupandisha abiria popote pale tena katikati ya barabara. Wanakwenda safari yote mlango ukiwa wazi wakiita abiria njia nzima.
Wanapotoka stendi kuu ya mabasi ya Msamvu, kwenda mjini au Kihonda, wanagombania abiria baadhi wakiwa ndani ya barabara ya Morogoro-Dodoma! Mengi wanayafanya wengi wao huku askari wa usalama barabarani wakiona! Ikitokea wachache wakachukuliwa hatua, wote wanagoma na suluhisho la wao kurudi barabarani ni ahadi ya kwamba “hawatasumbuliwa tena”!
Mwaka huu alihamishiwa Morogoro ofisa mmoja wa Mamlaka ya Usimaizi wa Usafirishaji Majini na Nchikavu (Sumatra).
Alipopambana kisheria kudhibiti uvunjanji sheria wa dalalala za mji huo kwa makosa ya ukiukaji wa ruti, daladala zikagoma na suluhu ikawa viongozi wa kisiasa kumtangaza ofisa aliyetimiza wajibu wake vizuri kisheria kwamba ni jipu!
Waliofanya hivyo ni viongozi hao wa kisiasa wanaohimiza watu kutii sheria na kuepuka rushwa! Ofisa huyu ametangazwa kuwa jipu kwa sababu hakuuchekea uvunjifu wa sheria. Naamini angeweza kujiunga kufanya hivyo kama angekubali kuwekwa sawa kwa rushwa.
Nilivutiwa sana na swali alilouliza mkuu wake kwamba ofisa wake ametangazwa kuwa jipu kwa kuachia uvunjifu wa sheria au amepokea rushwa? Sijui kama mkuu huyu hajui kwamba angefanya hayo, kwa mfumo wetu, asingeonekana jipu na angeonekana kuwa mtu wa watu. Hakuna tuliyemsikia akimlalamikia ofisa huyo kwa kubambikia kesi wala kukiuka sheria.
Tulisikia watu wa daladala wakikiri kukamatwa kwa makosa waliyodai waliyafanya kusaidia watu. Walilalamika kutozwa faini na waliposhindwa magari yalizuiliwa kwa kutozwa gharama za kuyatunza.
Hayo yote yako kisheria ila kwa sababu watu hawa wanalelewa kufanya makosa waliona si haki kuadhibiwa. Kinachosikitisha ni kwamba waliokosa na kuchukuliwa hatua walikuwa wachache lakini waliogoma walikuwa karibu wote!
Ukweli ni kwamba wadau wa daladala wa mji wa Morogoro, uliokosa bahari, wanaishi katika himaya yao ya kipekee! Nguvu gani imewapa jeuri hiyo? Uchawi gani umewalaza fofofo watu wenye mamlaka ya kuwadhibiti? Kwa nini aliyejitokeza kuwadhibiti katangazwa kuwa jipu? Sina majibu kwa kweli. Uchunguzi ndiyo utatoa majibu.
Rushwa ni ya kutokomezwa kwani kama ilivyoelezwa kwenye utangulizi wa kwanza wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Sura ya 329) rushwa ni kikwazo cha utekelezaji wa misingi ya demokrasia,utawala bora, haki za binadamu na inahatarisha amani, utulivu na usalama ndani ya jamii.










