Falsafa za Makonda kuhusu afya inakubalika

12May 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Falsafa za Makonda kuhusu afya inakubalika

Nimefuatilia falsafa ya Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar e s Salaam, Paul Makonda na kubaini ni ya kisasa katika eneo la afya na hasa kipengele cha kujitolea fedha Sh. billion 50 kwa mshindi wa wilaya itakayoongoza kwa usafi.

Mkuu mpya wa Mkoa wa Dar e s Salaam, Paul Makonda.

Hiyo inawafanya wakazi wa jiji wawajibike katika usafi kwa moyo wa kizalendo. Ni falsafa ya kipekee na adimu sana serikalini.

Wazo hilo la Makonda bila shaka limepokewa na wananchi na wakurugenzi wote wa Manispaa kwa mikononi miwili. Ni bora serikali kutumia mamilioni ya fedha, kuliko kuendekeza magonjwa huku ikibaki na fedha hizo.

Mtu akitanguliza afya, maana yake anatanguliza usalama wa uhai wake. Tujiulize, ni lini imewahi kutolewa fedha kiasi cha mabilioni ya shilingi katika shindano la afya? Mkuu wa Mkoa usilegeze!

Ni vyema wakuu wa mikoa kitaifa wakawa wabunifu kama vile Makonda ambaye tunamuombea abuni lingine zuri la Dar es Salaam.

Hiyo nayo ni changamoto kwa wafanyabiashara kuwa wasafi. Serikali iwatoze kodi ndogo hata kama ni Sh. 200, lakini kunakuwapo mipango mizuri ya afya.

Rais Dk. John Magufuli alichukua hatua ya maana kwa kuahirisha baadhi ya sherehe za kitaifa, ili zitumike kufanya usafi wa jamii na hiyo ilianzia siku ya Desemba 9 mwaka jana na tukaona kilichofanyika.

Usafi ni jambo la msingi, kwani linahitajika sana katika maeneo yenye huduma za jamii kama vile hospitali, ambako unahitajika kwa kiwango cha juu.

Hilo ndilo linaenda katika maeneo kama sokoni, ambako baada ya tukio la hivi karibuni tulishuhudia uzalishaji mkubwa wa taka kwa kiwango cha malundo.

Operesheni hiyo ambayo ni ya kitaifa, imepangwa kuwa endelevu, lakini Mkuu wa Mkoa - Makonda, ameipanga ifanyike kila wiki jijini Dar es Salaam.

Ni wazo zuri sana ambalo likifanyika kwa namna ya kuhamasisha jamii kwa mashindano, matunda yake yanaweza kuwa na sura nzuri zaidi ya kuijenga Dar es Salaam katika sura mpya na safi zaidi.

Hapo inanifanya niguse katika suala la uboreshaji wa dampo la Pugu Kinyamwezi, ambalo linaonekana kuelemewa sasa.
Hii inaipa jiji ujumbe kwamba, inahitajika dampo mpya mahali fulani, kukidhi kasi ya uzalishaji wa taka, jijini Dar es Salaam.

Nitafurahi kuona kasi ya maendeleo ya Dar es Salaam inayopanuka kila kukicha, inaendana na mabadiliko ya maboresho katika vigezo vya afya.

Huwa nafurahi kushuhudia serikali ikiisaidia jamii kwa kukusanya jumuiya ya wajasirimali pamoja na kisha waulizane wanachopenda kufanya.

Hapo wanaopendelea wanaweza kukusanyana kwa utaratibu maalum na kisha wanapatiwa eneo na nyenzo za kazi kama trekta la kilimi na kisha wanajiinua kiuchumi.

L Mwandishi wa makala hii anajitambulisha msomaji na Nipashe na mtunzi wa vitabu na anapatikana kwa namba ya simu: (+255) 0712 – 946671.