Mwanazuoni aliyegeuka lulu kwa kubobea kwenye sayansi ya udongo

12May 2016
Peter Orwa
Dar es Salaam
Nipashe
Mwanazuoni aliyegeuka lulu kwa kubobea kwenye sayansi ya udongo

Kuna dhana mahsusi inayotafsiri mahitaji ya ushiriki wa sayansi kwa wanafunzi wa sasa kuwa ni mdogo na hilo linaelezwa kuwa zaidi kwa wasichana.

Aneth David.

Dhana hiyo inapoelekezwa kwa Aneth David, inakuwa na jibu tofauti zaidi, kwani yuko katika jinsia hiyo na ni mpenzi kupindukia wa fani ya sayansi.

Akiwa kijana mdogo na kwa muonekano ni “mtu wa ‘kawaida,” wasifu wake katika utaalamu wa sayansi ya udongo na mbolea sasa umemfikisha katika kiwango cha juu. Ana sura zote za kitaaluma kuitwa mtaalamu mwandamizi.

Aneth ambaye kwa sasa ‘anashika chaki’ katika Idara ta Baiolojia ya Molekula ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mahali ambako kipindi kifupi kilichopita alipata mafunzo ya shahada zake za kwanza na pili, ana wasifu wa ziada.

Wasifu huo ni aliutoa katika mazungumzo maalum na Nipashe, kwamba ana kiwango cha ufaulu (GPA) ambayo ni wastani wa 4.8, ambacho kinafahamika ni kigumu sana kufikiwa na wanafunzi wengi katika vyuo mbalimbali.

Lakini kuna wasifu wa ziada ambao umempa utaalamu katika eneo la sayansi ya udongo hata hivi sasa kuingia katika mkataba na baadhi ya kampuni akiwa mtaalamu wao wa sayanasi ya udongo, ni namna alivyofanya mafunzo ya shahada yake ya pili, ambayo ni kwa njia ya utafiti (M.Sc by T0hesis).

Kwa mujibu wa Aneth, utafiti wake aliufanikisha ndani ya miaka miwili, tangu mwaka 2013, alijikita kutafiti changamoto za udongo na namna ynavyotunza tija ya kuotesha mimea.

Anataja kichwa cha habari kinachogusa eneo lake la utafiti kuwa: “Uwezo wa bakteria aina ya Bacillus kusaidia ukuaji wa mimea na kupambana na magonjwa ya mimea.”

Mtaalamu huyo wa udongo kijana anasema, changamoto iliyoko katika udongo unaotumia mbolea za kemikali ni kwamba inachakaa na kupoteza rutuba kwa wastani unaofikia asilimia 75.

Aneth anasema kuwa baada ya kupata utaalamu huo na kuchukuliwa na UDSM anakowajibika katika ngazi ya Mhadhiri Msaidizi. Pia, anashirikiana na asasi za CBN na CBA, zinajizohusisha na ufugaji nyuki na asali, pia ubora wa bidhaa zake.

Mbali na taasisi hizo, Aneth anaitaja taasisi ya EM Tech Foundation ya jijini Dar es Salaam, anayoshughulika nayo katika majukumu yanayoangukia kwenye taaluma yake, kama sehemu ya shughuli zake za ziada.

Anaeleza namna alivyopata udhamini wa masomo yake ya shahada ya uzamili, kwamba fursa zilitangazwa kwenye mtandao kwa ajili ya wanafunzi ambao wangechaguliwa mafunzo hayo kwa njia ya utafiti mwaka 2013, mfupi baada ya kumaliza shahada ya kwanza alipoibuka na matokeo yenye kishindo.

Msomi huyo wa sayansi – Aneth, anasema aliomba na kufanikiwa, ingawaje hawajui wenzake walioomba pamoja, hata vigezo vilivyotumika kumteua.

Anakumbuka ombi lake mtandaoni liliambatana na andiko binafsi la kujieleza kitaalamu sababu za kuomba nafasi hiyo namna anavyofaa kuteuliwa kwa fursa hiyo.

Msomi huyo mwanamke kijana, anaiambia Nipashe kuwa dhamira ya maisha yake kikazi yamelenga kuwa mwanataaluma mwandamizi, ikiwezekana kufikia ngazi ya profesa.

Anasema hadi sasa ameshapata nafasi nyingine ya kujiendeleza kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Sandwich, nchini Sweden kwa ajili ya mafunzo ya shahada ya uzamivu (PhD) anaeleza mfumo wa masomo hayo ni miezi minne katika mwaka anatarajia kuitumia darasani na kipindi kilichobaki, atarudi nyumbani kwa ajili ya kufanya utafiti.

Shahada ya kwanza ya Aneth, aliifanya katika eneo la Baiolojia ya Molekula na Baio Teknolojia (BSc. Molecular Biology and Bio- Technology) na Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Baio Teknolojia (M Sc. Bio –Technology).

Mhadhiri Msaidizi - Aneth, anataja masomo anayofundisha ni; Mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa mwaka wa tatu.

Pia kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili anafundisha masomo ya; Taarifa za Baiolojia (Bio- Informatics), Menejimenti ya Taarifa za Kompyuta (Computer Data Management)na Baio – Kemia (Bio Chemistry).

BALOZI WA SAYANSI

Mbali na utaalamu wake wa sasa, Aneth ni balozi maaalum nchini wa Umoja wa Wanasayansi wa Afrika uitwao Next Einstein Forum, wenye makao yake nchini Afrika Kusini, ambao msingi wake ni kusimamia nyendo na uwapo wa wanasayansi Waafrika katika nchi zao.

Aneth anaeleza namna alivyopata fursa hiyo kwamba, ni kufanya maombi maalum kupitia mitandao na ndipo alipoteuliwa, nafasi anayosema anadumu nayo kwa kipindi cha miaka miwili.

Je ni vigezo gani vilitumika kumteua Balozi wa Tanzania? Aneth ana maelezo kadhaa kwamba; Nafasi hutangazwa kupitia kwenye mitandao, fursa ikiwa mahsusi kwa wanasayansi vijana kutoka Tanzania.

Pia, kuna kigezo kingine kinachowekwa cha mwombaji anapimwa kama anakielewa vilivyo kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa nchi; uwezo wake wa kujieleza vyema mbele ya umma na kuna hatua ambazo ameshachukua katika kufanya hivyo; na ajirekodi kwenye kanda akijieleza namna gani anavyoweza kuwa balozi mzuri, ikiwa ni ishara dhahiri ya uwezo wake wa kujieleza.

Hata hivyo, ushiriki wa Watanzania katika nafasi hiyo, Aneth analalamika kuwa: “Tanzania bado iko nyuma, katika ushiriki (shindano lililomteua Aneth kuwa Balozi ) ni mdogo sana.”

ALIKOTOKEA

Kuna methali “usione kinaelea, kimeumbwa.” Ujumbe ulioko ni kwamba, kwenye jambo lolote linalong’ara huwa na mzizi wake.

Aneth anayeng’ara leo akiwa msomi aliyebobea katika teknolojia ya uhusiano baina ya baiolojia na kemia na ubobezi wa kipekee alio nao katika sayansi ya udongo, ni zao la msukumo fulani kutoka ngazi ya chini alikotoka.

Vivyo hivyo, ndivyo ilivyo kwa kazi yake nzuri katika taaluma hata akapata ufaulu wa ngazi ya juu kitaaluma, uliofanya abakishwe ‘kushika chaki’ UDSM nao una mzizi wake.

“Wazazi wana mchango wao katika kufanikisha katika masomo na sayansi. Kila nilichotaka kufanya waliniruhusu,” anasema Aneth na kuongeza:

”Kwanza mama alitaka niwe mnwalimu ili nipate kazi haraka, lakini mimi nikawa siupendi ualimu, lakini ndio sasa nimekuwa.”

Akirejea sababu ya kupenda somo la Baiolojia, ambalo anakiri liliongoza kutawala utashi wake katika masomo aliyosoma shuleni, huku akieleza chanzo cha kulihusudu somo hilo, lililomfikisha katika taaluma yake ya sasa.

“Mama Mwegela (Mwalimu wake wa Baiolojia) alinifundusha ndio alinipa ‘passion’ (mvuto) wa somo hilo. Alikuwa na sauti nzuri. Masomo ya Maths (Hesabu) na Cookery (Upishi) nayo niliyapenda,” anaeleza Aneth.

Mwanasayansi huyo anasema alizaliwa mwaka 1990 mkoani Mbeya na baada ya kupata elimu ya msingi mwaka 2003 alihamia katika Manispaa ya Moshi, ambako aliishi na mjomba wake, akianza masomo katika Shule ya Sekondari na kukiri alihamia shule tatu tofauti hadi alipomaliza kidato cha nne mwaka 2007, katika Shule ya Sekondari Mawenzi.

Baada ya matokeo kutangazwa mwanzoni mwa mwaka uliofuatwa, Aneth anasema alipata kiwango cha ufaulu cha darala la kwanza na ndipo alipojiunga na Shule ya Sekondari Majengo. Kabla ya hapo alikuwa katika Shule ya Sekondari Machame.

Anasema alikuwa mpenzi mkubwa wa kombinesheni ya Kemia, Baiolojia na Lishe ya Binadamnu, katika Shule ya Sekondari Majengo (CBN).

Hata hivyo, kujiunga na ‘kombinesheni’ hiyo ilikuwa matokeo ya juhudi binafsi baada ya kutafuta shule inayotoa masomo hayo mjini Moshi na mwaka 2010, katika matokeo ya mwisho ya mtihani wa kidato cha sita, alijikuta anapata tena ufaulu wa Daraja la Kwanza.

Aneth anasema pamoja na uelewa huo, hakuwa na ufahamu wa masomo yaliyokuwa yakitolewa kwenye vyuo vikuu na katika kutaptapa alikutana na rafiki yake anayemtaja kwa jina la Emmanuel.

Msomi huyo anaendeleza simulizi yake kwamba alifunguka macho zaidi akisema kuwa, rafiki huyo – Emmanuel, alimpatia kitabu chenye maelezo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University Prospectus) na ndipo akabaini kwa kina maudhui na mchanganuo wa kozi mbalimbali za UDSM.

Anasema hilo ndilo lililomvuta na kuchagua kozi ambayo yeye sasa ni mtaalamu anayetafiti na kufundisha darasani UDSM kwa miezi miwili sasa.

Katika kipindi hicho ambacho Aneth ni mwanazuoni katika Shule ya Sayansi ya UDSM, anaeleza mapungufu kadhaa anayobaini katika mfumo wa kujifunza na kufundisha sayansi.

Anataja mojawapo ni idadi kubwa ya wanafunzi kulinganisha na maabara na vifaa vilivyopo chuoni, pia sera zinazoongoza maendeleo ya elimu ya sayansi haijafikia kiwango bora kuoanishwa na mahitaji ya ufundishaji; na kiwango cha utafiti na matokeo yake kusambazwa, haijafikia kiwango kizuri.