Morogoro yajitutumua kumaliza tatizo la madawati

10May 2016
Ashton Balaigwa
Nipashe
Morogoro yajitutumua kumaliza tatizo la madawati

MKOA wa unakabiliwa na tatizo kubwa la upungufu wa madawati.Karibu wilaya zote baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi na Sekondari wanakaa chini.

Takwimu zinaonyesha kuwa, mkoa wa Morogoro licha ya kuwa na misitu inayotoa mbao lakini ina upungufu wa madawati 73,972 katika shule za msingi na sekondari 11,038.

Wilaya ya Ulanga, ni mojawapo katika Mkoa wa Morogoro ambayo imebarikiwa kuwa na misitu mikubwa lakini ni miongoni mwa wilaya zenye tatizo la wanafunzi wake kukaa chini kutokana na upungufu wa madawati.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ulanga, Isabela Chilumba, anakiri baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari katika wilaya hiyo wanasoma wakiwa wamekaa chini kutokana na upungufu wa madawati.

Hali hiyo anasema kuwa inatokana na ufinyu wa bajeti inayoletewa wilaya hiyo katika sekta ya elimu pamoja na mwamko mdogo wa wazazi katika kuchangia masuala ya elimu ikiwemo madawati na vifaa vingine.

Mkurugenzi anasema kuwa, pamoja na wilaya hiyo kuwa na misitu mingi, lakini walikuwa wanashindwa kuitumia kutengeneza madawati kutokana na sheria za misitu na mazingira zimekuwa zikiwabana na kukosa vibari vya kuvuna miti hiyo.

Hata hivyo anasema kuwa, tayari Serikali imetoa miongozo mbalimbali kwa kila kijiji kuanza kuvuna miti hiyo, baada ya kupata kibali kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutengeneza madawati kulingana na upungufu uliopo katika eneo hilo.

Wakati haiyo ipo hivyo, tayari wilaya imeanza kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa inamaliza tatizo hilo la upungufu wa madawati kwa kutumia rasilimali za misitu zilizowazunguka na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo makampuni ya uchimbaji wa madini.

Wilaya hiyo ambayo imekuwa ikielezwa kuwa ipo pembezoni kabisa ya mkoa wa Morogoro inakabiliwa na changamoto kubwa ya barabara, ina upungufu wa madawati kwa shule ya msingi 6,272 wakati shule za Sekondari zina upungufu wa viti na meza 1,200.

Wananchi wazungumzia upungufu

Mariam Said ni mkazi wa wilaya hiyo, anashangazwa wanafunzi wa wilaya hiyo kukaa chini kutokana na upungufu wa madawati wakati ina raslimali nyingi ikiwemo ya miti kwa ajili ya mbao na magogo.

“ Wingi wa miti wilayani kumesababisha kujengwa kiwanda cha mitiki kinachopasua mbao zinazoenda kutengenezwa vitu vya thamani nchi za nje huko Ulaya. Lakini sisi wenye miti hiyo watoto wetu wanakaa chini. Hali hii inatushangaza sana,” alisema Said.

Licha ya mitiki wilaya hiyo ina miti ya mbao mingi sana ambayo imekuwa ikivunwa kiholela na kunufaisha baadhi ya watu wachache wakiwemo viongozi wanaovuna mbao na kusafirisha nje ya wilaya na mkoa .

Naye Shomari Mkulunge, mkazi wa kijiji cha Makanga, anasema kuwa anashangazwa kuwepo tatizo la madawati katika wilaya hiyo kwa shule za sekondari huku kila kijiji kina msitu wa hifadhi ambao umesheheni miti ya mbao inayowezwa kuvunwa kwa utaratibu na kutengenezwa madawati na viti vya kukalia.

Anasema ni lazima Serikali ya wilaya ijipange katika hili ili kuhakikisha kuwa inatumia rasilimali hiyo ya miti kwa ajili ya kutatua changamoto ya tatizo la madawati ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kukaa kwenye madawati na kufanya vizuri.

Mkuu wa wilaya.
Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Christina Mndeme, anasema kuwa wilaya hiyo imejitazama upya na kuanza kutatua changamoto ya madawati kwa shule zote za msingi na sekondari kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka ikiwemo misitu katika kila kijiji.

Mndeme anasema, tayari wilaya hiyo imepata vibali kwa kila kijiji kwa ajili ya kukata miti ya mbao na kutumia nguvu za wananchi kutengeneza madawati katika kila kijiji chenye upungufu pamoja na viti na meza kwa shule za sekondari.

Mkuu huyo wa Wilaya, anasema miti ya mbao inapokatwa ni lazima ishirikishe kamati maalumu iliyoundwa na kijiji ili kuhakikisha kuwa inatumika kwa ajili ya utengenezaji wa madawati tu na sio kufanyia shughuli nyingine.

Kutokana na mipango hiyo, wafanikiwa kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwa asilimia 80 katika shule zote za msingi na sekondari na kwamba wamejiwekea lengo la kukamilisha utengenezaji huo kabla ya muda uliowekwa na mkoa Mei 30, mwaka huu na wa kitaifa Juni 30, mwaka huu.

Alipongeza wadau wa maendeleo katika Wilaya hiyo kwa kuchangia madawati kwa baadhi ya shule kwamba imesaidia kuwapunguzia wanafunzi tatizo la kukaa chini na kushindwa kufanya vizuri katika masomo.

Changamoto

Mkuu huyo wa wilaya amesema kuna changamoto mbalimbali baada ya serikali kuruhusu uvunaji wa mbao kwa ajili ya utengenezaji wa madawati, viti na meza kutokana na baadhi ya viongozi wa vijiji na watendaji wasio waaminifu kuuza mbao hizo kwa wafanyabiashara.

Aliwataja baadhi ya viongozi wa vijiji vya Kichangani, Mzelezi na Makanga walihusishwa na wizi wa mbao na tayari wamefikishwa mahakamani kwa kukiuka maagizo yaliyotolewa na Serikali.

Mkuu huyo wa Wilaya amewataja viongozi waliokamatwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Makange, Victorian Kamkwenela na mtendaji wake, Nestory Uhaju wanatuhumiwa kuiba mbao 94 kati ya 120 zilizoandaliwa kwa ajili ya kutengeneza madawati.

Viongozi wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Mzelezi, Hassan Itambiko na mtendaji wake, Salutian Likasi wanatuhumiwa kwa wizi wa mbao 17.

Katika Kijiji cha Kichangani, wanaotuhumiwa kwa wizi wa mbao za madawati ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mahogeli, Erick Kitumbuizi na mjumbe wa Serikali ya kitongoji, Faustine Mbanda, wanadaiwa kuiba mbao 22.

Mbao hizo anasema zilikutwa katika kiwanda cha kutengeneza samani kilichopo tarafa ya Lupiro, wilayani humo.
“ Vyombo vya dola vitaendelea kuwashughulikia viongozi wenye tamaa binafsi ya kutaka kukwamisha, kuwatakisha tamaa wananchi ambao tayari wamejitokeza kwa wingi kuchangia utengenezaji wa madawati,” anasema Mndeme.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro azungumza

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe, anasema kuwa, atahakikisha kuwa analisimamia kwa vitendo agizo la Rais Dk John Magufuli kwa kila wilaya kumaliza tatizo la upungufu wa madawati.

Kimkoa alisema kuwa ulishaweka mikakati na malengo mbalimbali ikiwemo kila wilaya kupewa kibali cha kukata miti ya mbao na kutumia rasilimali zilizowazunguka pamoja na wadau wa maendeleo kuhakikisha kuwa azma hiyo inatimia.

“ Hivi karibuni nitaanza kuzungumza na wilaya zote za Mkoa wa Morogoro, ili kuangalia utekelezaji wa agizo la Rais Dk Magufuli. Atakayezembea kabla sijawajibishwa tayari nitakuwa nimewatumbua watu majipu kwenye hili la madawati kwa sababu tulishapeana maagizo na majukumu, “ anasema Dk Kebwe.

Kauli ya Waziri wa TAMISEMI.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene akizungumza na viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote za mkoa wa Morogoro amesema, wakaoshindwa kutekeleza agizo la kujitosheleza kwa madawati katika shule ya msingi na sekondari hadi Juni mwaka huu, wajitambue wameshindwa kazi.

Pia wakurugenzi wa halmashauri watakaozalisha madeni ya watumishi na ya wazabuni wa vyakula katika shule za serikali, watakuwemo kwenye kundi la kuwajibishwa.

Alisema Viongozi wa Serikali ya mkoa wa Morogoro wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri (Ma-DED), makatibu tawala wa wilaya, na wakuu wa Idara za halmashauri zote watambue hilo ni agizo la rais na wanapaswa kulitekeleza.

“ Tumieni vyema nafasi zenu kuwa wenyeviti wa kutoa vibali vya uvunaji wa rasilimali za misitu ili madawati yaweze kutengenezwa na utekelezaji wa vibali hivyo ufuatiliwe ili visitumiwe vibaya na waliopewa kazi hizo,”alisema Waziri huyo
Serikali iliyopo madaraka ya awamu ya tano ya Rais Dk John Pombe Magufuli, imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa inamaliza kabisa, tatizo la ukosefu wa madawati ili kuhakikisha kuwa mpango wake wa kutoa elimu bure unapata mafanikio.

Katika kutekeleza mpango huo,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,alisema kuwa, zipo wilaya na mikoa yenye matatizo ya madawati na kusababisha watoto wao kukaa chini na kuwataka kuanza kujitathimini wenyewe.

Majaliwa alielekeza kuwa wilaya hizo zinaweza kulimaliza tatizo hilo la madawati kwa kutenga fedha kutoka katika vyanzo vyao vya ndani vya mapato au kutumia wadau mbalimbali kuhakikisha watoto hao wanasomea katika madawati. na kwamba, Rais Dk. John Magufuli, alishatoa maelekezo na kuwataka viongozi watakaoshindwa kutengeneza madawati ya kutosha katika shule zao wajipime.

Tatizo la Ukosefu wa madawati lilishazungumzwa na Serikali ya awamu ya nne kupitia kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wake mstaafu Mizengo Pinda aliyetoa takwimu za upungufu wa madawati na mikakati ya kumaliza tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Pinda wakati huo, takwimu zinaonyesha Tanzania ina mahitaji ya madawati 3,303,678.Yaliyokuwepo ni 1,837,783 hivyo kuwa na upungufu wa madawati 1,464,895 katika shule za msingi nchini.