Kishapu yaanzisha kampeni ya kudhibiti mimba shuleni

10May 2016
Marco Maduhu
Nipashe
Kishapu yaanzisha kampeni ya kudhibiti mimba shuleni
  • *Wanafunzi 500 hupachikwa mimba kila mwaka

KISHAPU ni miongoni mwa wilaya inayokabiliwa na changamoto kubwa ya wanafunzi wake kukatishiwa masomo kwa sababu ya kupachikwa ujauzito. Baadhi yao wanaozeshwa wakiwa na umri mdogo kwa sababu ya tamaa ya wazazi kulipwa mahari.

Hawa Ng’humbi akizungumza na wanafunzi

Asilimia kubwa ya wakazi wa wilaya hiyo ni wafugaji, ambao baadhi yao hawajali kabisa wanapoona mtoto wao ana ujauzito na kutimuliwa Shule. Hushindwa kumchukulia hatua mtu aliyemkatisha ndoto za kielimu binti yao. Matokeo yake wamekuwa wakikaa na mtuhumiwa kisha kukubaliana kutoa mahali ama faini ya mifugo kama hataki kumuoa msichana.

Hali ya watuhumiwa wanaowapatia ujauzito wanafunzi kutochukuliwa hatua kali za sheria kwa sababu ya wazazi wa binti huyo kumalizana kimyakimya, imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wilayani humo kuendelea kubebeshwa mimba shuleni kama kwamba hakuna sheria inayowabana wahalifu.

Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Hawa Ng’humbi baada ya kuona tatizo hilo limeendelea kuathiri wanafunzi kwa kupachikwa ujauzito huku wazazi wao wakiona jambo hilo kuwa kama ni la kawaida kwa kile wanachodhani kuwa ni neema kwao ya kupata mifugo kwa urahisi na kulaani tabia hiyo.

Ng’humbi amesema, baada ya kuhamia wilayani humo kikazi, amekuta wananchi wengi hawana mwamuko wa elimu huku wakishindwa kuwaelimisha watoto wao kuhusu madhara ya kufanya mapenzi wakiwa shuleni.Hali hiyo, imemfanya azindue Kampeni ya Kupinga Mimba Mashuleni akishirikiana na shirika lisilo la kiserikali la AGAPE.

Halmashauri hiyo ya wilaya ya Kishapu ina jumla ya Shule za sekondari 27, 26 za serikali na moja ya binafsi.Mwaka Mwaka (2015) wanafunzi 21 walipewa ujauzito na mwaka huu(2016) tayari wanafunzi watano (5) wamepachikwa ujauzito hali inayoashiria kuwepo uwezekano mkubwa wa wanafunzi wengi kukatiza masomo.

Ng’humbi anasema, katika Kampeni yake hiyo atazunguka Shule zote 26 za serikali na kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu madhara ya kufanya mapenzi shuleni na kuwaonya wanafunzi kwamba atakayebainika kuwa na ujauzito atapelekwa mahabusu na bwana yake ili liwe fundisho.

“ Hii ni aibu kila mwaka wilaya ya Kishapu inanyooshewa vidole kuwa, kinara kwa wanafunzi kubebeshwa ujauzito. Hali hii nimeikuta, lakini naona inaendelea kushamili na baadhi ya watendaji wa serikali wamekuwa wakilifanyia mzaha kwa kutowajibika kulimaliza tatizo hili,” amesema Ng’humbi

Anaongeza” Hata nyie walimu nimepata taarifa kuwa, baadhi yenu mmekuwa mkijihusisha kimapenzi na wanafunzi wenu, hivyo atakayebainika ndio itakuwa mwisho wa ajira yake na kuishia kufunguliwa mashtaka.Serikali ya awamu hii ya tano haina mchezo na suala la elimu hivyo kuweni chonjo.”

Pia mkuu huyo wa wilaya alivitaka vyombo vya maamuzi kuwajibika ipasavyo wanapopelekewa kesi hizo na kutozichezea kwa kutoa hukumu haraka kwa watuhumiwa, hali ambayo itasaidia kuondoa tatizo hilo.Aliwaonya watendaji wa kijiji, mitaa na kata kuacha kushirikiana na wazazi kumaliza kesi hizo kimyakimya.

John Myola ni mkurugenzi wa Shirika linalotetea Haki za Watoto (AGAPE) mkoani Shinyanga, ni miongoni wa mtoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa sekondari wilayani Kishapu kuhusu tabia ya kujihusisha na mapenzi wakiwa na umri mdogo, hali ambayo imekuwa ikilitia hasara taifa kwa kukosa wataalamu wake wenyewe.

Myola anasema, mwanafunzi anapopata ujauzito shuleni na kukatishwa masomo yake ni hasara kwa taifa, kwani alikuwa tegemeo la baadaye kuja kuwa mtaalamu, hivyo kufanya taifa liendelee kuishi kwa kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi ambao hulipwa mabilioni ya fedha jambo ambalo ni hasara kwa nchi yetu.

Hata hivyo amewataka wanafunzi hao kuwa wanatoa taarifa mapema kwa mkuu wa shule, wazazi wao hata viongozi wa serikali mtu yeyote anayemtongoza, ili apate kuonywa pamoja na kuwataja wanaowapachika ujauzito na siyo kuficha siri hiyo ili wapate kuwajibishwa kwa kufungwa jela.

Aidha Myola anasema takwimu za mwaka (2012) zinaonyesha kuwa, kila mwaka mkoani Shinyanga karibu wanafunzi 500 wa shule za sekondari wanapachikwa ujauzito, na watoto 16 kila siku wanabakwa mkoani humo, lakini watuhumiwa wa matukio hayo ambao wamekuwa wakikamatwa hawachukuliwi hatua na kuendelea kurandaranda uraiani.

“Mkuu wa wilaya kama unataka tufanye kazi pamoja na kukomesha vitendo hivi nakuomba usimame kidete usiwe na huruma.Nitakuletea watuhumiwa wote wa vitendo hivi, maana Shirika langu limekuwa likiwakamata, lakini serikali kupitia baadhi ya vyombo vyake vya maamuzi imekuwa ikitetea wahalifu hao,” amesema Myola na kuongeza kuwa
“Imefikia mahali vyombo hivyo likiwamo dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi kuanza kunitishia, maana kesi hizo zinapofika sehemu hizo zinageuzwa kuwa dili na kukaa na watuhumiwa kuwapatia vitu vidogo na kuifuta kesi hiyo, na ninapoonekana kuishupalia naanza kupewa vitisho.”

Pili Misungwi ni mkuu wa dawati la jinsia la Jeshi la Polisi Shinyanga anasema, kesi hizo kufutwa sio kwamba wanapewa vitu vidogo, bali wamekuwa wakikosa ushahidi wa kutosha wanapoanza kufanya upelelezi watendewa wa vitendo hivyo wamekuwa hawatoi ushirikiano mara baada ya wazazi wao kumalizana kimyakimya.

Anasema tabia hiyo ya kumalizana kimyakimya na wao kunyooshewa vidole kuwa, hawawajibiki ipasavyo, wao hawapo tayari kuwajibishwa bali wataanza kuwakamata na wazazi ambao wamekuwa wakikaa na watuhumiwa kuelewana na kupeana mifugo huku tayari wameharibu maisha ya mtoto na kumpotezea uelekeo.

Naye Ofisa Elimu Sekondari wa wilaya hiyo ya Kishapu Charels Stephano, amesema vitendo hivyo vya wanafunzi kupachikwa ujauzito, pia vimekuwa vikichangiwa na wazazi wenyewe kwa kushindwa kuwatimizia mahitaji ya shule watoto wao, hali ambayo imekuwa ikiwafanya kuingia kwenye vishawishi.

Nao baadhi ya wanafunzi wa sekondari wanaosoma wilayani humo Khadija Mikidadi anayesoma Shule ya Kishapu na Victoria Shida anayesoma Mwataga wamesema kwa nyakati tofauti kuwa, tatizo linalosababisha wanafunzi kupewa ujauzito ni umaskini kutoka majumbani kwao kwa kukosa mahitaji muhimu ya shule.

Shida anasema pia umbali nao umekuwa ukichangia wanafunzi kupewa Mimba, ambapo njiani wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali vya kutongozwa, na hivyo kuwafanya kujikuta wakitumbukia kwenye mapenzi na kuambulia ujauzito, na kutoa wito kwa serikali kuwajengea hosteli wanafunzi wa kike.

Naye Mikidadi hakusita kuwataja watu, ambao wamekuwa vikwazo kwao kwa kutongoza wanafunzi, kuwa ni askari polisi, waendesha bodaboda kwa kutumia mbinu za usafiri, walimu wao pamoja na wafanyabiashara kwenye mnada wa Mhunze wilayani humo, ambao umekuwa ukifanyika kila Alhamisi wakiwamo na wafugaji.