Ameongezewa wiki moja nyingine ya majaribio.Winga huyo machachari wa Azam FC na timu ya taifa (Taifa Stars) ameonekana kulivutia benchi la ufundi la timu hiyo na wanataka kumsajili kwa mkopo wa miaka miwili.
Mkurugenzi wa Azam, Yussuf Bakhresa, anayefuatilia majaribio ya mchezaji huyo Hispania, anasema Tenerife itaanza mazungumzo na uongozi wa Azam FC juu ya kumnunua mchezaji huyo.
“Tunatarajia kuanza mazungumzo nao juu ya suala la Farid, ingawa wazo lao la awali ni kumchukua kwa mkopo wa miaka miwili, sasa tunasubiri ofa yao rasmi, kisha Bodi ya Ukurugenzi itajadili na kutoa maamuzi,” anasema Bakhresa.
Awali, alikuwa apelekwe katika moja ya klabu za Ligi Kuu ya Hispania, kati ya Las Palmas na Athletic ya Bilbao kwa majaribio, lakini wakala wake akashauri mchezaji huyo aanzie timu ya Daraja la Kwanza Hispania ili kupata nafasi ya kucheza, kukomaa na kuzoea soka la Ulaya taratibu.
Kama atafanikiwa kucheza soka la kulipwa nchini Hispania, basi atakuwa ameungana na Mtanzania Mbwana Samatta ambaye yuko nchini Ubelgiji akikipiga na klabu ya Ligi Kuu, KRC Genk.
Farid aliyezaliwa Mei 21, 1995, ilianza kung'aa kwenye michuano ya Kombe la Kagame hasa katika mechi ya nusu fainali dhidi ya KCCA ya Uganda.
Alifunga bao pekee kwenye mechi hiyo ngumu katika dakika ya 78.
Lilikuwa ni bao lililoipeleka fainali na hatimaye Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza tangu ipande kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara 2007.
Azam ilimnasa Farid kwenye kikosi cha timu ya Mkoa wa Kilimanjaro kilichoshiriki mashindano ya Copa Coca Cola 2011. Tangu hapo alifanya vizuri kwenye kikosi chao cha vijana chini ya miaka 20 na msimu uliopita alipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa.
Tangu kupandishwa amekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo, huku pia aking'ara kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Kiungo huyo ndiye aliyefunga bao la kwanza kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Esperance ya Tunisia, mchezo uliofanyika jijini Dar es Salaam na Azam kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, akitoa pasi ya mwisho la goli la pili lililofungwa na Ramadhani Singano 'Messi'.
Farid ameonyesha uwezo mkubwa kasi yake, uwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga, na akili ya kumfanya awe na maamuzi sahihi wakati wote.Si winga wa kukimbia tu kama baadhi ya mawinga wa Kibongo. Anapomtoroka beki anafahamu anakwenda wapi na akifika hapo atafanya nini.
Ana uwezo wa kuinua shingo na kuangalia wenzake wamekaa vipi, na si kujipigia tu.
Ndiyo sababu krosi zake nyingi husaidia Azam.
Amefunga magoli mawili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, akiwa ameifungia Azam magoli manne kwenye ligi tangu alipoanza kucheza ligi 2013/14.










