Lianzishwe dawati la jinsia bungeni

08May 2016
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Lianzishwe dawati la jinsia bungeni

WANAWAKE wapinzani bungeni wameonyesha kukerwa na udhalilishaji wa kijinsia na kupuuzwa kinamama unaofanywa na baadhi ya watu wakiwao wabunge wanaotumia utaratibu wa ‘stereo typing’ au ‘kuwagandisha’ wanawake kwenye mawazo ya kiunyanyasaji iliyoota mizizi ndani ya jamii inayotawaliwa na mfumo dume.

Kugandisha wanawake kunaendana na kauli za mbunge Goodluck Mlinga wa CCM anayedai kuwa wabunge wa viti maalum wapinzani wamenapata fursa hiyo kwa njia ya ngono au kuitwa baby.

Udhalilisha kwa kauli umezoelekea utasikia wanawake ni wambea, watu tegemezi na wakati mwingine wanasema mwanamke ni mswaki wa mti unauvunja, kuutumia ukiuchoka unautupa.

Tukio la bungeni juzi si la kawaida kwani wanawake wameendelea kutukanwa hadi kwenye chombo cha maamuzi. Sehemu ya kuwakilisha na kuzungumza masuala ya kuiwajibisha na kuishauri serikali, kuchambua matatizo ya umma, kutunga sheria na kupitisha bajeti.

Mbunge Mlinga anayekashifu wanawake hadharini hakuzingatia heshima na utu wa mwanamke, kiongozi kama huyu huenda hatakuwa na muda wa kuzungumzia hoja za kuinua usawa wa kijinsia na kuhakikisha kuwa wanawake wanasoma, wanakombolewa kifikra , wanajitegemea ili kuhudumia familia kwa weledi zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ukatili wa kijinsia, kuanzia kashfa na dharua kama za mbunge huyo zinawaathiri mamilioni ya wanawake barani Afrika.

Utafiti uliofanyika mwaka 2005ukihusisha afya za wanawake na ukatili wa kijinsia, WHO iliripoti kuwa asilimia 50 ya wanawake wa Tanzania na asilimia 71 huko Ethiopia wanaishi kwa vipigo na aina nyingine nyingi za manyanyaso kutoka kwa wenza, wapenzi na hata viongozi wao.

Lakini ukweli ni kwamba ukatili dhidi ya wanawake unakwenda mbali ni zaidi ya vipigo kuna mambo mengi WHO inazungumza. Udhalilishaji kama huo wa bungeni ambao huitwa ‘intimidation’ ni sehemu ya vitisho kudharauliwa, kupuuzwa tena wanawake wakiwa kazini.

Hayo hufanyika kwenye taaluma, maofisini na hata kama ilivyoonekana bungeni.

Madai kama hayo yanasababisha fikra, huumiza na hata kusababisha watu wengine wazidi kupuuza wanawake. Ni wazi kuwa jamaa wa wabunge hao wanaoambiwa wanapata ubunge kwa njia ya zinaa wanaweza kuwapuuza.

Kadhalika madai hayo yanaweza kutumiwa kuwatukana wanawake wanasiasa ambao huingia bungeni kwa njia ya kuchaguliwa.

Pamoja na vitisho na kauli za kuudhi manyanyaso mengine ni ndoa za utotoni, kuozwa kwa mahari kubwa ikihusisha fedha ama ng’ombe wanaolipwa kwa binti. Mume humnyanyasa na kumdhalilisha apendavyo kutokana na mahari aliyomlipia.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (Tamwa) na Shirika la Mpango wa Maendeleo ya Watu (UNFPA), tatizo hilo liko kwenye mikoa ya Mara, Manyara na sehemu nyingine zenye wafugaji.

Mahari kubwa huwa chambo cha kumnyanyasa mwanamke anayelazimishwa kuzalisha zaidi, kuzaa watoto wengi, kutumikia familia ya mumewe na kuwa mtumwa na iwapo atataka kuachika wazazi hawampokei kwani hawako tayari kurudisha mahari kwa wake zao.

Tukirejea bungeni, kashfa na unyanyasaji kama huo unawafanya wanawake kudharaulika kuwa ni watu wa madaraja ya chini. Kushushwa hadhi huko kunaongeza kupuuzana na unyanyasaji zaidi kutoka kwa wanaume.

Aliyekuwa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake, Radhika Coomaraswamy, wakati wa uongozi wake aliwahi kueleza kuwa mazoea na utamaduni wa kuwadhalilisha na kuwadhihaki wanawake unaofanywa na wanaume, ukichanganyikana na tofauti za kiuchumi na kisiasa unasababisha wanawake wengi kuwa na hali duni.

Pamoja na kwamba wanawake wapinzani wamekuwa mstari wa mbele bungeni kukosoa na kuihoji serikali masuala mengi yanayohusu udhalilishaji kuanzia watoto , wazee hadi mauaji ya albino, kinachojitokeza ni tuhuma kuwa wanachaguliwa ‘kingono’. Michango yao haithaminiki bali kinachotizamwa ni mambo hasi.

Wabunge hawa wamekuwa mstari wa mbele kutafuta na kuhimiza kuweka mifumo na taratibu zakulinda rasilimali za nchi na kuondoa umaskini na daima wamepinga ufisadi.

Kauli ya Mliga ifungue njia ili serikali itunge sheria za kutekelezwa mkataba wa UN wa mwaka 1979 unaoagiza kutokomezwa kwa aina zote za unyanyasaji wa wanawake (CEDAW).

Mkataba huu unaziagiza serikali zibadilishe sheria kandamizi, sera na mila za kishenzi na kutumika kauli za kudhalilisha kama hizo zinazoelezwa kuwa ili upate ubunge unatakiwa kutoa rushwa ya ngono.

Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayohalalisha binti kuolewa na chini ya miaka 15 nayo ifanyiwe marekebisho.
Kwa kurejea kashfa hiyo iliyotokea bungeni ni wazi kuna haja ya kuwahamasisha wanaodhalilisha ili wakubali usawa ni vyema kuwe na dawati la kijinsia bungeni.

Ili kuleta usawa unaotazamiwa ni wakati wa viongozi kusaidia kubadilisha mitizamo na fikra inayowarudisha wanawake nyuma na kusaidia juhudi za kuwaongeza zaidi bungeni na kwenye taasisi za umma.

Pia ni wakati wa kuwafundisha Watanzania umuhimu wa kuwalinda na kuwathamini wanawake kwenye jamii.