Wanasheria watendeeni haki wananchi

08May 2016
Ibrahim Mkamba
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wanasheria watendeeni haki wananchi

KWA kiwango kikubwa, wanasheria kadhaa wa Tanzania wamekuwa hawaitendei haki nchi kutokana na kuendekeza maslahi binafsi, yao na ya wengine wanaowahusu, ushabiki wa watu,wa kiitikadi na kupenda kuwafurahisha baadhi ya watu hasa wenye mamlaka.

waziri wa katiba na sheria, dk. harrison mwakyembe.

Mwanasheria halisi popote duniani anaposhughulikia jambo lenye maslahi kwa umma husimamia lililo la kweli tena mwanasheria si mtu wa kutetemeka ni jasiri na asiyekubali kushawishiwa kupindisha ukweli.

Nani atanishawishi kwamba kwenye kesi hizi za uchaguzi hakuna hata moja yenye ukiukwaji wa kustahili kubatilisha ushindi wa mbunge wa chama chochote? Zote zinashindwa! Siyo mkakati huu?

Wanasheria wetu ndiyo wanahusika na mikataba mibovu ya kuitesa nchi. Mara kadhaa pia wamekuwa upande wa pili dhidi ya maslahi ya umma kama ilivyotokea wanasheria wenye mamlaka makubwa kuwa upande wa kampuni ya kufua umeme ya Dowans ilipodai kulipwa pesa yote ambapo Watanzania wenzetu hawa walipaswa wapambane ili tusilipe au tulipe kiasi pungufu lakini tuliwasikia wakisema.

“Hapa hakuna namnalazima tulipe pesa yote”.Waligeuka vipi kuwa watetezi wa Dowans dhidi ya Watanzania tunaowalipa mishahara?

Ni wanasheria wetu walioshiriki kuvuruga mchakato wa katiba kuanzia walipotoa tafsiri mbovu na iliyokosewa mno ya kifungu cha 25 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (sura ya 83 toleo la mwaka 2012) kuhusu uwezo wa Bunge Maalum la Katiba, jinsi mmoja alivyoliendesha bunge hilo kwa kulazimisha kuingizwa mambo mengi yasiyo maoni ya wananchi, alivyosimamia kupitishwa kiutata kwa katiba inayopendekezwa, isiyo ya wananchi, iliyosimamiwa kuandikwa na mwanasheria mwingine.

Tukiendelea nayo, katiba inayopendekeza itatoa katiba batili kwa mujibu wa utangulizi (preamble) wa sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Utangulizi huo unaainisha msingi mkuu wa kuandika katiba yetu kuwa maoni ya wananchi.

Mwanasheria anapotafsiri kwamba Bunge Maalum la Katiba lina uwezo wa hata kubadili rasimu yote anamaanisha linaweza kutengeneza kitu kipya nje ya maoni ya wananchi!

Tujiulize, tume ya kukusanya na kuratibu maoni iliundwa kwa sababu zipi? Maoni yalikusanywa ili yafanyiwe kini na nani alipaswa kutoa hoja za kuomba namna ya kuishi kama taifa ni wananchi wote au wajumbe tu wa Bunge Maalum la Katiba?Hii ndiyo iliyofanya tushindwe kuandika katiba hiyo.

Kwa usahihi, Bunge Maalum limepewa uwezo wa kubadili maoni kwenye rasimu kuyafanya yawe na uhalisia na kutekelezeka. Kwa mfano ukomo wa mbunge uliopendekezwa miaka 15, ungeweza kufanywa miaka 35 na si kuuondoa.

Badala ya kuondoa mawaziri kutokuwa wabunge ilivyopendekezwa na wananchi, wangepewa uwezo na katiba kuingia bungeni kujibu hoja na kufanya kazi nyingine za serikali lakini bila kuwa wabunge.

Leo hii wanasheria wetu wanataka kulazimisha kupigwa, kinyume cha sheria, kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa.

Wao wanajua kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, namba 11 ya 2013 ikisomwa pamoja na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,kwa katiba hii iliyopendekezwa, kisheria, kura ya maoni haipigiki.

Wanasheria, akiwemo mbobevu Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, wanajua hivyo lakini wanatumia kutojua sheria kwa wananchi kuwapumbaza kwamba kura ya maoni inapigika.

Kwa mujibu wa sheria hizo, kila hatua imepewa muda maalum kisheria tangu siku ya kuchapishwa kwa katiba inayopendekezwa mpaka kupigwa kwa kura ya maoni.

Kwa sasa tukio hilo limepitwa na wakati na kura hiyo ikipigwa ni kinyume cha sheria.Tatizo ni tarehe za kuanza mchakato baada ya katiba inayopendekezwa kuchapishwa ambayo inavuruga vipindi vyote vinavyofuata .

Tusome vifungu 32(1), 33(1) na 33(3) vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na 4(1),5(1) na 5(3) vya Sheria ya Kura ya Maoni.

Tungekuwa na wanasheria makini wenye mamlaka, wenye uchungu na nchi hii wangemshauri Rais yafanywe mambo mawili; kurekebisha kifungu cha 22 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwaondoa wajumbe wanaoingia wote toka Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi na badala yake nao waingie kwenye Bunge Maalum la Katiba kwa idadi ndogo ya uwakilishi kutoka vyama tofauti kwa idadi inayolingana kama asasi mojawapo.

Kwa maana hiyo vifungu vya 22(1) (a) na (b) vifutwe na kifungu cha 22 (1) (c) kirekebishwe kiwe 22(1) tu kwa kuongeza kundi la bunge na baraza la wawakilishi na hivyo kuwa na vifungu vidogo (i) mpaka (xi).

Pili, wamshauri aitishe upya bunge hilo maalum lenye marekebisho ya wajumbe kuandika katiba itakayoenda sawa na “Hapa Kazi Tu” na utumbuaji majipu, vinavyokosekana kwenye katiba inayopendekezwa ingawa yalikuwamo kwenye rasimu ya pili iliyotokana na maoni ya wananchi.

Anayo nguvu ya kufanya hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 28 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Naomba wanasheria wa Tanzania muwe wazalendo, mpiganie maslahi ya nchi dhidi ya yale ya mabepari wa kimataifa na msipotoshe wananchi kwa maslahi yenu na ya tabaka la watawala.