Marais wa zamani, vigogo Republican na kizungumkuti cha Trump

07May 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Marais wa zamani, vigogo Republican na kizungumkuti cha Trump

HUKU akionekana dhahiri kuwa mgombea anayesubiri kuteuliwa rasmi kupeperusha bendera ya chama cha Republican kwenye kinyang’anyiro cha urais wa Marekani baadaye mwaka huu, Donald Trump,

Rais wa zamani wa Marekani, George Bush, akiwa na Bush (baba yake) na kaka yake Jeb ambao wametangaza kumkataa Trump, kutinga White House.

bado anakutana na vihunzi vya hapa na pale vinavyoonyesha bayana kwamba safari yake ya kwenda White House si nyepesi.

Pamoja na kuwa ndiye pekee aliyebakia amesimama kwenye kinyang’anyiro cha kuiwakilisha Republican baada ya wagombea wenzake kujitoa mmoja baada ya mwingine, bilionea huyo ana wakati mgumu kukubalika na vigogo ndani ya chama ambao wanamuona kama asiyefaa kukabidhiwa jukumu la kuliongoza taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.

Na hali hiyo imezidi kujianika baada ya marais wawili wa zamani wa nchi hiyo ambao wanatoka familia moja ambao ni Baba George Walk Bush na mwanae George Bush kuweka bayana kupitia wasemaji wao kwamba hawatamuunga mkono Trump.

Marais hao wa 41 na 43 wa nchi hiyo walisema dhahiri kwamba hawatamuunga mkono pamoja na kuwa mteule mtarajiwa baada ya mahasimu wake wawili waliokuwa wamebakia kwenye kinyang’anyiro hicho cha ndani ya Republican kuamua kubwaga manyanga wiki iliyopita.

Maamiri jeshi wakuu hao wa zamani wote wawili wameungana kwenye orodha inayozidi kuongezeka ya watu maarufu ndani ya Republican ambao wamekataa kuunga mkono harakati za Trump kuwania kutinga White House akiwa kama rais wa Marekani.

Rais wa zamani George W. Bush, ambaye mdogo wake Jeb alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho Februari mwaka huu baada ya mlolongo wa matokeo yasiyo mazuri kwake, ameweka bayana kwamba hatashiriki kabisa kwenye kampeni za bilionea huyo mtata.

Alipoulizwa kama rais huyo wa karibuni zaidi kutoka Republican atatumia umaarufu wake kuongeza nguvu kwenye kampeni ya Trump, msemaji wake Freddy Ford alisema: 'Rais Bush hana mpango wa kushiriki wala kuzungumzia chochote kuhusiana na kampeni hiyo ya urais.'

Msemaji wa rais wa zamani George H. W. Bush, Jim McGrath, yeye alisema: 'Kwa umri wake wa miaka 91, Rais Bush amestaafu kuachana na siasa.'

Trump ni kama tayari ameshakamilisha kinachotakiwa kuteuliwa kuwa mgombea wa Republican baada ya seneta wa Jimbo la Texas, Ted Cruz, na gavana wa Jimbo la Ohio, John Kasich, kuachia ngazi kwenye kinyang’anyiro hicho kufuatia uchaguzi wa mchujo wa Jimbo la Indiana wiki iliyopita.

Hata hivyo, baadhi ya vigogo ndani ya Republican bado wana matumaini ya kuwepo ushindani kwenye mkutano wa uteuzi, kitu ambacho kinaweza kutokea iwapo tu kama Trump hatafanikiwa kupata jumla ya idadi ya wajumbe 1,237 inayotakiwa.

Kwa hivi sasa tajiri huyo tayari ana wajumbe 1,053, lakini ana uwezekano mkubwa wa kupata sehemu kubwa ya wajumbe 514 ambayo bado imebakia kwa vile hana ushindani.

Mbali na marais hao wawili wa zamani, Seneta Ben Sasse wa Republican kwenye Jimbo la Nebraska yeye alisisitizia tena taarifa zake kwamba hatamuunga mkono Trump na kusema ataangalia mgombea mbadala kama bilionea huyo atateuliwa.
Vile vile kumekuwepo ukimya kutoka kwa Spika wa Bunge, Paul Ryan, ambaye amekuwa akimkosoa sana Trump lakini ameshakataa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kama mgombea mbadala.

Tim Miller, msemaji wa zamani wa Jeb Bush, yeye aliandika kwenye Twitter kumpinga kabisa Trump akieleza kama kupitishwa kwake ni kitu kisichowezekana.

Seneta Deb Fischer wa Republican yeye aliweka wazi alipofanya mahojiano kwenye Nebraska Radio Network kwamba atamuunga mkono mteule wa chama hicho lakini alikuwa hafurahishwi na Trump.'Bw. Trump atakuwa na kazi ngumu kukiweka chama pamoja,' mwanamke huyo alisema.

Gavana Nikki Haley wa Republican kwenye Jimbo la Carolina Kusini alitoa taarifa akisema atamuunga mkono mteule wa chama hicho lakini alikuwa ‘hana mpango’ kuwa mgombea mwenza na makamu wa rais wa chama hicho baada ya kuwepo uvumi kwamba Trump anaweza kumchagua yeye.

Lakini kwa upande mwingine, Gavana wa Oklahoma, Mary Fallin, alimuidhinisha Trump kwa furaha na alikaribisha uvumi wa uwezekano wa yeye kuwa mgombea mwenza wake.

Mitch McConnell, kiongozi wa wajumbe walio wengi kwenye Seneti, alisema Trump alikuwa na 'fursa na jukumu’ la kukiunganisha chama hicho.

Alisema chama hicho kilikuwa kimepania 'kurudisha uchumi na usalama wa taifa' na kuzuia 'awamu ya tatu ya Barack Obama' kama mgombea anayeongoza ndani ya Democratic, Hillary Clinton atashinda kutinga White House.
McConnell alitoa wito kwa Trump kukiunganisha chama hicho kufikia 'malengo yetu'.

Hali hiyo ilitokea wakati mamia ya wafuasi wa Republican walipochoma moto kadi zao za kupigia kura na kutangaza kuunga mkono kampeni ya kumpinga inayojulikana kama #nevertrump, ambayo inalenga kumzuia bilionea huyo kuingia White House.

Mwelekeo kama huo kwa upande wa Trump, unafanya wengi waonekane kuwa tayari kupigia kura Democratic pamoja na kuwa wafuasi wa muda mrefu wa Republican.

Dennis Jordan aliandika kwenye Twitter: 'Nimekuwa mtiifu wa maisha yangu yote wa @GOP, tangu siku nilipoweza kupiga kura. Usiku wa leo, nimejiondoa kwenye usajili na hivi sasa niko Huru.'

Lachlan Markay yeye aliweka kwenye Twitter picha ya kadi yake ya kupigia kura ya District of Columbia ikiungua moto.
Ben Howe kwa upande wake alisema: 'Kama wewe ni #nevertrump basi nashauri ukubali matokeo ya kile inachomaanisha. Usijidanganye. Mimi hapana.'