Wakunga wahamasishe tiba ya fistula kulinda utu wa mwanamke

07May 2016
Gaudensia Mngumi
Nipashe
Wakunga wahamasishe tiba ya fistula kulinda utu wa mwanamke

HALI ya kuvuja haja ndogo au choo na wakati mwingine vyote kwa pamoja ambayo kitaalamu huitwa fistula, zama hizi inazuilika na inatibika.

wakunga

Lakini ukosefu wa taarifa za jinsi ya kujiepusha na tatizo ama namna ya kulitibu, umesababisha mamia ya wanawake kuendelea kunyanyapaliwa na kudhalilishwa utu wao baada ya kuwa waathirika wa matatizo yanayotokea baada ya kujifungua.

Kukosa habari za uzazi salama kunamaanisha kuwa watu ama waathirika ambao ni wanawake ni ‘mambumbumbu’ hawafahamu kikamilifu masuala ya msingi ya kitaalamu kuhusu, ujauzito, ulezi wa mimba, uzazi na hawajui kuwa fistula inatokana na uchungu mkali na wa muda mrefu.

Ni vyema kuuleta ujumbe wa fistula wakati wa kuadhimisha siku hii ya wakunga kwa vile ni jambo linalohusiana na uzazi, ili wazalishaji hawa wanapotafakari yaliyo mbele yao wakumbuke na tatizo hili. Chanzo cha fistula ni kichwa cha mtoto kukwama ndani ya njia ya uzazi hivyo kuongeza ‘presha’ inayotokana na kusugua kibofu ama njia ya haja kubwa na kusababisha kuchanika kunakomletea mama tundu.

Shimo hilo ndilo linalosababisha wanawake kushindwa kujizuia kuvuja mkojo ama haja kubwa au vyote kwa pamoja muda wote na kama hawatafanyiwa ukarabati tatizo hilo hudumu na kuwadhalilisha wanawake wanaotengwa na jamii.

Kadhalika huwa mwanzo wa kunyanyapaliwa.Kina mama wanatengwa na jamii, wanaitwa wachafu, wanakimbiwa kutokana na harufu, hawana wateja wa bidhaa zao, watu hukataa vyakula walivyopika. Hata hivyo, waathirika hawa huwa wanyonge na wapweke waliokata tamaa. Kila mmoja amhurumuie mwanamke hivi kuzaa mtoto ndiko kunakosababisha adhalilike utu wake?

SIKU YA WAKUNGA

Mei 05 ni Siku ya Wakunga, niunganishe maadhimisho ya siku hiyo na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazozungumzia fistula kuwa , wanawake zaidi ya 2,000,000 wanateswa na hali hiyo. Kwa Tanzania, wanawake kati ya 25,000 hadi 30,000 wanaathirika kila mwaka.

WHO inaeleza kuwa 1,000 wanafanyiwa ukarabati wa kuziba matundu ya fistula, na hapa nchini huduma hizo hutolewa bure na wadau mbalimbali ikiwamo Hospitali ya CCBRT Dar es Salaam.

Ukarabati hutolewa hospitali za Bugando mkoani Mwanza, KCMC mkoani Kilimanjaro, Selian mjini Arusha na Peramiho huko Ruvuma, kwa mujibu wa taarifa za mtandaoni za CCBRT, hivyo waathirika wachangamke wasiendelee kuteseka na kuchanganyikiwa kisaikolojia.

Wakunga wanapoadhimisha siku hii muhimu wana mtihani wa kupunguza vifo vya wazazi vinavyohusiana na matatizo ya ujauzito hivyo wanachangamoto ya kuifanya Tanzania kuwa salama kwa wajawazito. Leo katika wanawake 100,000 wanaojifungua 410 wanakufa japo vifo vyao vingeweza kuzuilika.

Wakunga wanafahamu kuwa licha ya kupata fistula wazazi wengine wanaathirika na kulemaa miguu (foot drop) kunakotokana na mimba kusababisha tatizo kwenye mishipa ya fahamu, baadhi hupata maambukizi makubwa ya kizazi, kifafa cha mimba na hata kuchanika na kuondolewa mfuko wa uzazi.

Kwa kuona mambo mengi yanayohatarisha maisha ya wanawake , wakunga wanawajibika kuwahimiza na kuwakumbusha kujifungulia hospitalini na kuhudhuria kliniki ili kujiepusha na fistula na vifo vinavyoletwa na ujauzito.

Lakini hiyo pekee haitoshi serikali iongeze na kuboresha huduma za uzazi ili kuwe na uhakika wa afya ya mama na mwana na masalahi bora ya mkunga ambaye ndiye anayesaidia kupatikana watoto hao.
SABABU ZA FISTULA

Mtandao wa WHO unaonyesha kuwa wanawake wanaweza kuteseka kwa uchungu wa muda mrefu kutokana na kukosa madaktari , wakunga na hospitali za kuwahudumia, hasa wanapooanza uchungu huo.

Tatizo la miundombinu mibovu huathiri pia wajawazito kama kukosa gari la wagonjwa ‘ambulensi,’ barabara mbaya zisizopitika muda wote hasa vijijini ni miongoni mwa mambo yasababishayo hali hii, kwani inasababisha mama ateseke na uchungu.

Ndoa na mimba za utotoni zinaleta hatari ya kupata fistula, hii inatokea kwa sababu binti anabeba ujauzito mapema hata kabla ya viungo vya uzazi kukomaa na kuhimili mikiki ya mimba. Wakati mwingine hupata uchungu mkali lakini kutokana na umri na uchanga wa viungo anapata tatizo hilo.

Kwa Tanzania tatizo la mimba za utotoni linachochewa na kuendeleza mila na utamaduni unaomuoza binti mapema hasa miongoni mwa jamii za wafugaji. Kadhalika ni matokeo ya ukosefu wa shule zenye miundombinu rafiki kwa mabinti hasa ukosefu wa maji , mabweni na chakula.

Utafiti uliofanywa mwaka jana na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) mkoani Tabora ulibaini tatizo la ukosefu wa mabweni, maji na chakula kwenye shule za sekondari za kata pamoja na nyumbani pia huchochea mimba na ndoa za utotoni.

Ulibaini kuwa ukosefu wa maji hasa vijiji unawalazimisha mabinti kusaka huduma hiyo usiku wa manane, halikadhalika kukosa mabweni kunawaingiza kwenye vishawishi vinavyotokana na kutembea umbali mrefu kwenda shuleni ama kupangisha nyumba mitaani.

Huko wanalaghaiwa na waendesha bodaboda, wafanyabiashara na vijana wanaoishi nao wanaotumia fedha kuwahadaa ili kuwatumia kingono. Bila kusahau umaskini wa familia unasababisha kuooza mabinti ili kupata fedha na ng’ombe za mahari.

Ushirikina unaohusishwa na fistula kwa sababu wenye hali hiyo wanadaiwa kuwa ni wachawi ama wamerogwa hivyo hawatibiwi na kuendelea kukuza tatizo. Wengine hutuhumiwa kuwa wameharibu mimba, wanadaiwa kuwa wamelaaniwa na mama au jamaa zao, huku wengine wanatuhumiwa kuwa ni wazinzi ndiyo maana wametoboka sehemu za ndani zinazosababisha kuvuja mkojo.

Ubakaji nao unachanjia kwa vile wanawake wanaobakwa na kundi la wanaume wengi (gang rape) wanaweza kupata fistula.

Kukwepa huduma za kliniki na kuzalia kwa wakunga wa jadi au waganga wa kienyeji kunaweza kuleta fistula kwa vile mzazi anakosa msaada anapozidiwa na uchungu mkali wakati mtotto amekwama kwenye njia ya uzazi.

SHUHUDA

Mwanamkuu Jumbe ni mama wa miaka 81 ambaye ameishi na fistuala kwa miaka zaidi ya 60 anasema alipata tatizo hilo alipojifungua watoto mapacha mwaka 1950.“Sikufahamu kuwa tatizo linaweza kutibiwa hospitalini nimejua mwaka juzi.

Pia niliaminishwa na wanawake na wakunga wa jadi kuwa kuvuja haja ndogo ni kawaida baada ya kujifungua” anasema Mwanamkuu ambaye hayuko tayari kufanyiwa ukarabati, akiamini kuwa umri wake ni mkubwa hana sababu ya kuhangaika tena.

Mama huyu ni mfano wa wanawake wengi ambao wanaaminishwa uongo hivyo kusita kutafuta huduma za matibabu ya fistula. Anaamini kuwa kama taarifa hizi zingepatikana miongoni mwa wakunga, kanisani, misikitini na kwenye mikusanyiko ya watu kama sokoni huenda wanawake wasingeteseka na kufedheheka kwa fistula.

Hata hivyo, Mwanamkuu anasema wakati mwingine alipokwenda hospitalini akiwa na maradhi mengine aliwaeleza madaktari kuhusu tatizo hilo lakini aliambiwa kuwa halina dawa.

Anaamini kuwa hata madaktari wengine huenda hawafahamu kuhusu ukarabati hasa vijijini hivyo anashauri wapewe taarifa mara kwa mara ili wawasaidie wanawake.

“Naamini hata kei kuna madaktari na wakunga ambao hawafahamu kuwa fistula inatibika kwa hiyo hawakuwasaidia wanawake wenye shida hii. Kama wangekuwa wanafahamu wangewapa rufani mapema..”

UNYANYAPAA

Mwanamkuu anasema alinyanyapaliwa na mumewe aliyemuacha na kuoa mke mwingine huku akimuachia watoto saba aliozaa naye licha ya kwamba alikuwa ana tatizo la kuvuja mkojo.Kadhalika wakwe zake na familia ya mumewe ilimtenga na kulazimika kurudi kwa kaka zake waliowasomesha wanae na kumtunza pia.

Anasema licha ya kuishi na ugonjwa huo watoto wake wanamtunza na wamemshauri kwenda hospitalini lakini anaona kuwa siku za kuishi zimekwisha hana haja ya kusumbuka.

KUSHINDWA KULA

Anasema madhara ya kupata fistula ni pamoja na kushindwa kula vyakula bora. Anamaanisha kuwa wataalamu feki mitaani walimkataza kutafuna miwa, kutumia vimiminika kama uji, chai, maziwa, matunda hasa mapapai na machungwa hata maji kisa walidai vinaongeza hali hiyo. Hivyo akawa anatumia vyakula vikavu zaidi.

Analalamikia ukosefu wa taarifa sahihi kuwa fistula inatibika na inapona tena mwanamke kurudia hali ya kawaida, ndiko kunakowakwamisha wanawake wa vijijini kutafuta huduma hiyo kwa vile wengi hawajaelimika na ni vigumu kupata habari za ujauzito na uzazi salama kama watu wanavyojua.

Kwa mujibu wa maelezo yake fistula ni mzigo kwa wanawake maskini ambao hawawezi kununua vifaa vya kujisitiri hasa pedi, sabuni za manukato na marashi kwa ajili ya kupunguza harufu.

Kwa sababu huduma za kukarabati fistula zinapatikana tena bure wakunga wawafahamishe wanawake kufuatilia huduma za uzazi salama ili kujiepusha na vifo na maambukizi ya kizazi yanayotokana na tatizo hili. Lakini pia, wakemee mila mbaya kama kuoza mabinti kwa vile kunaongeza ukubwa wa tatizo.

Mambo yasiishe hapo ni lazima serikali iboreshe huduma za uzazi, ifunze wakunga wa kutosha, iwalipe mishahara minono, ikibidi kuwaboreshea maslahi kila wakati na kuwapa vitendea kazi muhimu ili wawahudumie wajawazito, wazazi na watoto kwa lengo la kupunguza vifo vya wanawake na watoto na fistula ambayo inadhalilisha utu na heshima ya mwanamke.