Hujafa hujaumbika, mtoto akiugua analemaa akili…

28Apr 2016
Nebart Msokwa
Mbalizi
Nipashe
Hujafa hujaumbika, mtoto akiugua analemaa akili…

VERONICA Agripa, anayeishi katika Mtaa wa Mlima Reli, ulioko katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, ni mama wa familia ya watoto watatu, ambaye anakabiliwa na mtihani mkubwa wa malezi.

Kushoto kabisa ni Fromena Mwampashe (Mlemavu), wa pili kushoto ni Veronica Agripa ambaye ni mama wa familia, anayefuata ni Stanslaus Mwampashe (Mlemavu) na Kulia ni Agripa Mwampashe ambaye ni baba wa familia. Picha na NEBART MSOKWA.

Mtihani huo ni kwamba, katika watoto hao wawili ni walemavu na anaamini kwamba, iwapo uchumi wake ungekuwa mzuri, alikuwa na nafasi ya kuwanusuru na tatizo hilo.

Veronica, ambaye ni mke wa Agripa Mwampashe, anawataja watoto hao kuwa ni Fromena (17) ambaye ndiye mtoto wa kike pekee, Romado (13) na Stanslaus ambaye ana miaka tisa.

Mama huyo analalamika kuwa, kati ya watoto hao, ni mmoja pekee, Romado, ndiye aliyepata bahati ya kusoma Shule na kwa sasa yuko darasa la sita katika Shule ya Msingi Mbalizi One.

Anasema watoto wengine ambao ni Fromena na Stanslaus, hawajawahi kwenda shule, licha ya kuwa na umri unaopaswa kuwa shuleni. Kikwazo kikuu anachokitaja Verionica, ni ulemavu wa ubongo walio nao tangu umri mdogo.

Fromena na Stanslaus, ukiwakuta nyumbani kwa hisia ni watoto wazuri na wanafurahia kila mgeni anayeingia kwenye nyumba yao, lakini hakuna wanachoweza kueleza, pia hawana uwezo wa kumuelewa mtu zaidi ya kucheka na kumpa mkono mara kwa mara.

Kwa mujibu wa maelezo ya mama yao, udhaifu huo wa kushindwa kuwasiliana unaenda mbali kwamba hawana hata uwezo wa kutamka neno moja tu katika maisha yao, isipokuwa ‘mama.’

Veronica anasema, kwa watoto hao takriban kila kitu wanahitaji msaada wa mama, ikiwamo huduma ya kujisaidia

WALIVYOANZA KUUGUA

Veronica anasema watoto wake wote walizaliwa katika kijiji cha Isansa
wilayani Mbozi. Fromena alizaliwa mwaka 1999 na Stanslaus alizaliwa mwaka 2007. Wote walizaliwa wakiwa na afya nzuri.

Anasema kifungua mimba wake (Fromena) alianza kupata matatizo akiwa na umri wa mwaka mmoja alipougua kwa muda mrefu na akapata homa na kuharisha,hali iliyomfanya mtoto huyo adhoofike.

Mama huyo anasimulia kwamba aliwahi kumpeleka kutibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi (Vwawa), lakini alipewa jibu la kitabibu kwamba alikuwa na malaria.

Anaongeza kwamba licha ya kutibiwa, bado hali haikuwa nzuri na ilimfanya amhamishie katika Hospitali ya Rufani Mbeya, ndiko kulikogundulika bintiye ana matatizo ya ubongo.

Madaktari walisema kwamba, hakuna namna nyingine ya kufanya, bali kurejea naye nyumbani.

Veronica anasema hali hiyo ilimuathiri mwanawe achelewe kuanza kutembea na alipata uwezo huo wa kutembea akiwa na umri wa miaka minne, lakini hakuweza kuongoea zaidi ya kutamka neno ‘mama’.

“Mtoto wangu wa kwanza (Fromena) alizaliwa vizuri na alikuwa na afya, lakini akiwa na mwaka mmoja aliugua kwa muda mrefu. Alikuwa anatapika na kuchemka, hali hiyo ilifanya mifupa kuchelewa kukomaa na kumfanya aanze kutembea akiwa na miaka minne na tangy hapo, hata matatizo ya ubongo yalianza,” anasimulia.

“Kuhusu mtoto Stanslaus, alianza matatizo akiwa na umri wa miezi minne na haikujulikana kilichokuwa kikimsumbua, lakini alikuwa analia sana hasa nyakati za kuanzia jioni mpaka alfajiri. Jioni alikuwa mzima,” anasema Veronica.

Anafafanua kwamba, aliaza safari ya matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi (Vwawa) alikoambiwa hakuna tatizo lililogundulika.

Veronica anaeleza zaidi kuwa, baada ya kuona hali si ya kuridhisha, alihama Mbozi na kwenda kuishi
Sumbawanga kati ya mwaka 2007 na 2013. Katika kipindi hicho wanawawe hawakuwahi
kulia tena.

Anasema katika kipindi hicho, alijifariji kuwa mwanawe amepona, lakini baada ya muda mfupi, aligundua mwanawe alianza kuonyesha dalili za tatizo kama la dada yake, yaani kushindwa kujitambua na kujieleza, zaidi ya kutamka ‘mama’.

“Stanslaus alianza akiwa na miezi minne kuugua, alikuwa analia kiasi kwamba tulikuwa hatulali. Nilienda naye katika Hospitali ya Vwawa, ambako walimpima na wakasema ugonjwa hauonekani.

“Lakini nikakuta mtoto habadiliki, tukaamua kuhama tukaenda Sumbawanga na tangu hapo hakulia tena lakini ikajitokeza hali kama ya dada yake,” anasema mama huyo.

MITIHANI YA MALEZI

Mama wa Fromena anasema malezi ya wanawe ni magumu kutokana na kumzuia asiende kufanya shughuli nyingine za kiuchumi na anaishia kushinda nyumbani kuwaangalia watoto, hali inayomfanya aishie kumtegemea mume ambaye ni fundi cherehani.

Veronica anataja shughuli zinazomuweka nyumbani kuwahudumia wanawe ni kuandaa chakula na kuhakikisha wamekula, kuwasindikiza chooni na kuwahudumia huko pamoja na kuwalinda wasidhurike na magari yanayopita jirani.

Anasema kuna baadhi ya wasamaria wema ambao wamwekuwa wakimsaidia kwa baadhi ya mahitaji kama vile chakula na hata fedha.

Veronica anasema hata makazi anayoishi sasa wamehifadhiwa kwa baadhi ya vyumba walivyopewa na msamaria mwema, katika makazi ambayo walipaswa kulipa kodi.

Kuhusu shule ya watoto, Veronica anadai kwamba awali wakati wanaishi Sumbawanga, walikuwa hawajawahi kuwapeleka watoto hao shuleni, kutokana na hali zao kuwa hawajiwezi.

Anasema baadaye, alipata ushauri kutoka kwa mtu aliyekuwa amewahifadhi kwamba, zipo shule maalumu kwa ajili ya watoto walemavu, jambo lililomfanya ahamie Mbalizi na kuzitafuta.

Veronica anasema alifanya juhudi za kuzunguka mkoani Mbeya kusaka shule za watoto hao bila ya mafanikio na mara nyingi alipata majibu ambayo si ya kuridhisha.

Anataja baadhi ya maeneo alikopita ni Kituo cha Iwindi kilichopo katika Mji Mdogo wa Mbalizi, alikoahidiwa angetafutiwa shule, lakini mpaka sasa hajajibiwa.

Kwingine ni shule maalum ya watoto walemavu iliyopo wilayani Rungwe, alikoambiwa inapokea watoto walemavu wa viungo na sio wa akili, ikawa imeshindikana katika mawanda ya uwezo wake.

Anasema mara ya mwisho alienda katika Shule ya Itigi iliyopo jijini Mbeya, ambayo inapokea wanafunzi mchanganyiko na anasema alikubaliwa, lakini tatizo likawa uchumi, kwa sababu alitakiwa kuwapeleka na kuwachukua kila siku.

Veronica anaomba msaada kwa serikali, asasi na watu binafsi wenye uwezo wa kumsaidia katika malezi ya watoto hao, ikiwa ni pamoja na kuwasomesha angalau waweze kupata elimu ndogo ya kujitambua.

Anasema familia yake haina kitega uchumi chochote na hofu yake kubwa ni iwapo watafariki, itakuwa shida kubwa kwao.

BABA ANENA

Agripa Mwampashe, ambaye ni baba wa familia hiyo, anasema awali alikuwa anamudu kutafuta riziki ya familia yake kutokana na kwamba alikuwa anajishughulisha na kilimo ambacho kilikuwa kinaipatia familia chakula na kipato.

Anasema kwa sasa kazi hiyo haiwezi, kutokana na sababu kwamba amekuwa akiugua mara kwa mara, hali iliyomfanya aanze kutegemea kazi ya ufundi Cherehani.

Mwampashe anasema amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Atha kwa kipindi cha miaka tisa, hali inayomfanya sasa ashindwe kufanya shughuli za kilimo.

Anasema, hata kazi yake hiyo ya ufundi cherehani anashindwa kuipanua, kutokana na kwamba mzigo wa familia ameubeba mwenyewe kwa sababu mkewe hawezi kujishughulisha.

Mkuu huyo familia anaiomba serikali imsaidie katika malezi ya watoto wake, ili angalau baadaye wawe na uwezo wa kujitegemea watakapokuwa wakubwa zaidi.