Hoja ya matumizi ya makao hayo, imebadilika katika miaka ya karibuni baada ya kushamiri matukio ya mauaji ya vikongwe wanaotuhumiwa uchawi, mahali hapo panatumika kuwahifadhi wanaonusurika kuuawa.
Kambi hiyo imekuwa ikihudumiwa na serikali kwa kutengewa bajeti maalumu ya chakula na matibabu. Tangu mwaka 2006, huduma ya matibabu ilisitishwa, ingawaje haijawa bayana juu ya sababu za hatua hiyo na mbadala wa maamuzi hayo.
Hali iliyopo sasa, kuna mtihani mkubwa juu ya hatima ya afya ya wazee hao ambao kwa sasa wako 40, pindi wanapougua, kwani hakuna mfumo rasmi wa kusimamia matibabu yao.
Katika idadi hiyo, baadhi ni wanandoa kwa maana ya mume na mke na baadhi wana watoto.
Janga jingine linalokabili majengo hayo ya kambi katika umri wake wa miaka 102, ni kwamba yameshaanza kuporomoka.
Awali, kambi ilipokuwa ikianzishwa, ilikuwa na majengo sita, lakini sasa yamebaki majengo mawili pekee ndiyo yanayotumika, kwani mengine ama yameanguka au yana hali mbaya na yamejaa nyufa.
Evodia Ndaka ni Msimamizi Msaidizi wa kituo hicho, anayesema wazee wanaolelewa kwenye kambi hiyo hawana tatizo la njaa, bali hali ngumu wanayokutana nayo ni katika kupata huduma ya umeme, majengo wanamoishi na uzio wake.
Anasema hofu ya usalama iko katika hatari ya majengo kubomoka na kuingiliwa na wahalifu.
Msimamizi huyo wa kituo anasema kuwa, mvua zinapoanza kunyesha kama ilivyo sasa, wazee hao wanaishi kwa hofu ya kuangukiwa na majengo yaliyochakaa na wanaamua kukaa nje na huwa wanafanya hivyo kwa kumtaarifu msimamizi afike hapo hata ikiwa usiku, wakimuomba awasaidie.
“Kweli kuchakaa kwa majengo kwenye kambi hii kunanitesa sana, hasa pale mvua zinaponyesha na kuvuma kwa upepo, wazee hukimbilia nje huku wakinyeshewa na kulundikana kwenye jengo moja ambalo ndio imara.
“Mvua inapokatika, wanarudi kwenye vyumba vyao na kulala usingizi wa hofu ya kupondwa na nyumba,” anaeleza Evodia.
“Pia kulikuwa na utolewaji wa pesa kwa ajili ya matibabu ya wazee hawa, lakini zilisitishwa tangu mwaka 2006,” anadokeza Evodia na kuongeza:
“Nimeandika barua nyingi za kuziomba, lakini hazijibiwi na kufikia hatua ya kutoa pesa zangu mkononi, maana vikongwe hawa ni kama wazazi wangu kwa sasa”
WAELEZA KILIO CHAO
Mwenyekiti wa wazee kwenye kambi hiyo, Samwel Maganga, anaiomba serikali itatue kilio hicho cha majengo na uzio ambayo yana muda mrefu, ili kuwahakikishia usalama wa maisha yao.
Maganga anasema adha hiyo imefikisha hatua kwamba, baadhi ya wazee wenye uwezo wa kutembea, hutoroka kambini na wanaenda kuomba mitaani.
Anaeleza imani yake kwa serikali na Rais Dk. John Magufuli, kwamba atakapolifahamu hilo ataingilia kati kuwatatulia kero hizo, akitoa mfano wa mafundi Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) wamekuwa wakifika na kupima kisha wanatokomea pasipo kutoa majibu yoyote.
Anna Malongo, ambaye ni mkazi wa Manispaa ya Shinyanga na mdau aliyezoea kutembelea kambi hiyo ya wazee, kwa kuwapatia misaada mbalimbali ikiwamo chakula na mavazi, anaishauri serikali ichukue hatua kwa kutatua kilio cha wazee hao.
Mdau huyo wa haki za wazee, anasema katika miaka ya nyuma, wazee walikuwa wakiishi maisha bora kutokana na kupatikana huduma zote muhimu kambini hapo, ikiwamo matibabu.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Mkoa wa Shinyanga, Selena Mapula, anasema matatizo yanaendelea kuwaandama wazee, kwa sababu hayatafutiwi ufumbuzi mapema.
Anazitaja kambi za Kolandoto na Usanda, kwamba zina hali mbaya, kutokana na wawakilishi wa wazee kutoshirikishwa kwenye mabaraza ya maamuzi katika ngazi za maeneo yanayowahusu, akiataja baadhi ni Kijiji, Kitongoji, Kata, Halmshauri, Wilaya na Mkoa.
Selena anasema kwamba ushirikishwaji wa wahusika kutoka ngazi hizo ulikuwa na nafaso kubwa katika kutatua matatizo hayo yanayojitokeza sasa katika ngazi tofauti, akivitaja vyombo vya habari kwamba ndiyo nyenzo pekee zinazoonekana kufanya kazi ta kuwasemea.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee waa Wilaya ya Shinyanga, Edward Lupimo, anasema kuna baadhi ya matatizo ya wazee yanayoweza kutatuliwa kwenye ngazi za chini, ikiwamo kukomesha mauaji ya vikongwe kwa kuunda jeshi la jadi la Sungusungu.
Anataja jingine kuwa ni kwa wazee hao kupatiwa vitambulisho vya matibabu bure, kupitia halmashauri wanakotoka.
Helena Maleza ni Katibu wa asasi ya kiraia iitwayo (TAWLAE) mkoani hapa ambayo inajihusisha na kutetea haki za wazee, anasema kwa miaka mingi wamekuwa wakipaza sauti kuwapigania wazee, lakini utatuzi wa suala hilo ulikuwa mtihani mkubwa.
Anasema asasi yake inampongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuwaingiza wazee kwenye wizara, kilio walichokuwa wakikipigania kwa muda mrefu na wanaamini wazee sasa wako katika nafasi nzuri kupata haki zao.
Anataja sehemu ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwakabili wazee kwa muda mrefu ni yanayohusu haki za Pensheni.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi, aliyefika kwenye kambi hiyo ya wazee kwa ajili ya kutoa zawadi ya Sikukuu ya Pasaka akimwakilisha Rais Dk. Magufuli, alikiri hali mbaya ya majengo na kuahidi kufanyika juhudi za kunusuru usalama wa wazee hao.
Dachi anaahidi kwamba serikali mkoa wa Shinyanga, itatenga bajeti ya kuyakarabati majengo hayo na kusimamia utekelezaji wa sera ya matibabu kwa wazee kwa kuwa na madirisha maalumu ya kuwatibu kuanzia ngazi ya zahanati.
“Suala la kusitishwa fedha za matibabu kwa wazee hawa kambi ya Kolandoto, nadhani inatokana na sera ya kutibiwa bure kwa wazee, maana na mimi mgeni hivyo sifahamu kwa undani zaidi suala hili.
“Lakini, cha msingi nitasimamia utekelezaji wa Sera ya Matibabu Bure kwa Wazee na hiyo ndiyo itakuwa mwisho wa tatizo hilo." anasema Dachi










