Lengo la kuanzisha elimu hiyo ni kuwahifadhi wanafunzi hao na kuwapunguzia adha ya usafiri.
Watoto hao wanaotoka sehemu mbalimbali za Shinyanga, jumla yao wakiwa 41, walitengewa makazi maalumu, hatua ilioyoendana na kutengewa bajeti ya chakula kwa kila mwaka wa fedha, kwa mujibu wa ratiba za masomo na likizo zao.
Mwaka 2008, iliposhamiri mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, maarufu kama Albino, serikali katika ngazi ya mkoa iliamua kuwa watoto albino wapelekwe kuhifadhiwa kwenye kituo hicho na kupewa ulinzi mkali, ili kuwahakikisha usalama.
Albino wanaopelekwa na kulelewa kwenye kituo hicho wanatoka katika maeneo tofauti jirani, ikiwamo mkoa wa Shinyanga, Simiyu na wilaya ya Nzega iliyoko mkoani Tabora.
Kumiminika kwa watu kituoni hapo, kulitokana na kuwapo sifa kwamba kituo kipo katika hali nzuri ya kuhifadhi watoto hao katika hali ya usalama.
Licha ya kituo hicho kuwa chini ya serikali, bajeti ya chakula kwa watoto hao albino haikutengwa na iliyokuwepo ni kwa ajili ya watoto 41 wasiosikia.
Hiyo imewafanya watoto wenye ulemavu wa ngozi waishi kwa kutegemea msaada hadi sasa wakipelekewa na wazazi na wasamaria kituoni hapo.
Mazingira hayo yanawafanya watoto kuwa na lishe duni na uhalisia wa mazingira yao, umewafanya wanyemelewe na maradhi kama kuharibika ngozi, utapiamlo na meno kuoza.
Mwaka jana, Chama cha Madaktari Bingwa wa Kinywa na Meno Tanzania (TDA), walifika kwenye kituo hicho cha kulea watoto wenye ulemavu wa ngozi kutoa huduma za elimu ya kinywa matibabu ya kuziba na kung’oa meno.
Aidha, mwaka huu madaktari hao wakiadhimisha Wiki ya Kinywa na Meno, walitembelea kituo hicho cha watoto na kutoa elimu na tiba ili kuhakikisha afya zao zinaimarika na kuishi maisha bora.
Arnold Mtenga ni daktari bingwa wa meno kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), aliyeambatana na mabingwa wenzake kutoka TDA, anasema:
“Tumeamua kutembelea kituo hiki tena kufanya uchunguzi wa Meno kwa watoto albino, kundi ambalo limekuwa likisahaulika kutokana na kuishi kwa kutegemea wahisani.
“Baada ya kufanya ukaguzi wa kinywa, tumebaini watoto hawa wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa meno,” anasema Dk. Mtenga na kuongeza:
“Wana matatizo ya kuharibika fizi, meno kutoboka, kuoza. Tumeyang’oa na wengine kuyaziba, pamoja na kuwapatia dawa za meno, miswaki na mafunzo ya kujua namna ya kusukutua ili kukabiliana na kuharibika meno yao.”
Dk. Bakari Lembati, aliyeshiriki mwaka jana katika utoaji tiba na elimu ya kinywa kwa watoto hao albino, anasema mwaka huu watoto waliowapatia tiba mwaka jana, hawajangudulika kuwa na matatizo.
Anasema kuna tofauti kubwa sana, lakini kutokana na ukweli kwamba kila siku kuna watoto wapya wanaojiunga na kambi hiyo, kuna changamoto katika kufikia malengo ya kumaliza tatizo hilo.
Gustav Rwekaza, ni daktari wa meno anayehusika na kutunza takwimu. Anasema kituo hicho kina watoto 409 na kati yao, waliofanyiwa uchunguzi ni 250 ambao ni sawa na asilimia 61.
Rwekaza anatoa sababu ya uchunguzi huo kutofanyika ni muda mfupi waliokuwa nao kulingana na ratiba yao.
Anasema katika orodha hiyo ya uchunguzi kuna watoto 34 ambao ni sawa na asilimia 13.6 ndio waliogundulika kuwa na meno yaliyotoboka, baadhi yamezibwa na mengine yameng’olewa.
Dk. Rwekaza anafafanua kwamba, kuna watoto watano waliobainika kuwa na matatizo makubwa ya meno na wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Shinyanga, kutokana ukweli, jopo la madaktari bingwa waliokuwepo hawakuwa na muda wa kutosha.
“Mbali na meno kutoboka, pia fizi zao ni mbovu, zinatoa damu, meno yamebadilika rangi na kuashiria kuwa huwa hawapigi mswaki mara kwa mara.
“Pia napenda kutoa wito kwa walezi, hili liwe endelevu, elimu izidi kutolewa ili kulinda vinywa vyao,” anasema Dk. Rwekaza
MGANGA MKUU & WALENGWA
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Nuru Mpuya, anawashukuru madaktari hao bingwa kwa kutembelea kituo hicho cha watoto albino na kuwapa matibabu na aliahidi itakuwa endelevu kwa kupeleka wataalamu mara kwa mara kutoa elimu na tiba ya meno.
Dk. Mpuya anafafanua kuwa, hali ya maradhi ya meno mkoani Shinyanga si ya kuridhisha, kwani wananchi wamekuwa wagumu kuzingatia elimu na kutunza vinywa vyao kwa kupiga miswaki.
Anasema kuna mazoea ya wananchi kuendekeza kutunza vinywa vyao kwa njia za kienyeji, jambo linaloishia na kuharibika meno na matatizo ya vinywa.
Kaimu Mganga Mkuu huyo anasema, takwimu za mwaka jana zinaonyesha mkoa wa Shinyanga umetoa matibabu ya meno kwa watu 2,500 ama kwa kung’oa au kuziba, ikijumuisha watu wa rika zote na mkakati walioupanga wa mwaka huu, ni kutembelea shule kutoa elimu ya usafi wa kinywa na meno.
Nao watoto walengwa walionufaika na huduma hiyo, Mariam Peter na Tatu Moses, wanasema tatizo linalowakabili kituoni kwao katika suala la kutunza vinywa, ni kukosa miswaki na dawa, huduma wanazozipata kutoka kwa wasamaria wema.
Wanatahadharisha kuwa, endapo wasamaria hao watasitisha misaada hiyo, maisha yao yatakuwa magumu na ndio maana hata utunzaji wa meno yao unakuwa mgumu, hasa katika upatikanaji wa vifaa vya kutunza kinywa, pindi iliyopo inapokwisha.
Mtoto Mwashi Balongo, anapaza sauti kwa Rais Dk. John Magufuli, awatengee bajeti mahsusi ya kuwatunza, ili waondokane na kadhia iliyopo ya kuishi kwa kuwategemea wasamaria.
Kwa upande wake, Mlezi Mkuu wa Kituo hicho, Mwalimu Peter Ajali, anatoa wito kwa wataalamu wa afya na magonjwa mbalimbali wajitokeze kila mara kuwasaidia watoto hao, kama walivyofanya mabingwa wa tiba ya kinywa
MWISHO










