Tatizo ambalo limekuwa likiwasumbua hasa wamiliki wa shule binafsi nchini ni madai ya kuwapo kwa asilimia kubwa ya walimu wanaozalishwa kutoka katika vyuo vilivyopo, wasio na viwango vinavyotakiwa.
Licha ya nidhamu na kuzingatia masomo wanayofundishwa watoto, bado ubora wa mwalimu katika kazi hiyo ni muhimu, ili kuziwezesha shule kupata watoto wenye uelewa mkubwa utakaowawezesha kufanya vizuri katika mitihani yao hasa ya taifa, na hatimaye kuwa na uwezo wa kulitumikia taifa.
Twaha Rashid ni miongoni mwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka jana, katika shule ya sekondari Kaizirege iliyoko katika manispaa ya Bukoba, ambayo ilishika nafasi ya kwanza kitaifa kufuatia matokeo ya mtihani huo, anasema walifanya vizuri kutokana na juhudi za walimu.
Rashid anasema kuwa, mtoto yeyote akifundishwa na mwalimu mwenye viwango vya juu na ujuzi unaokubalika, lazima atafanya vizuri kimasomo pia baada ya masomo atakuwa mtumishi aliyeelimika.
“Shule yetu ilishinda kwa sababu tunao walimu wenye viwango vya kufundisha vinavyokubalika, pia juhudi za wanafunzi katika masomo ni sababu iliyochangia ushindi huu,” anasema.
Anasema wakiwa shule wamekuwa wakitengeneza mahusiano mazuri na walimu wao na kuwa karibu nao kila mara, pia walipenda sana kusoma vitabu kutoka katika maktaba ya shule, ambavyo vimewaongezea uelewa na kuwasaidia kufaulu.
Eulogius Katiti ni meneja wa shule ya Kaizirege Boarding Nursery, Primary, Secondary and High School, anasema pamoja na shule binafsi ikiwamo ya kwake kufanya vizuri katika mitihani ya taifa, wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa walimu wa Tanzania wa kutosha wenye uwezo mzuri wa kufundisha
“Uwezo wa walimu unatokana na msingi, mfano mwalimu amemaliza chuo kikuu lakini je msingi wake ulikuwaje tangu alipoanza elimu ya msingi hadi anafikia hatua ya kwenda chuoni,” anasema.
Anasema pamoja na walimu kutokuwa na uwezo mkubwa wa kufundisha, pia waliopo hawatoshi, na kuwa kinachofanyika ni shule binafsi kunyang’anyana walimu na serikali, maana nayo inataka walimu kwa ajili ya shule zake, pia hata wao wanahitaji walimu kutoka katika vyuo vile vile.
Anasema kuwa, changamoto hiyo ni kubwa na ya kitaifa, na kuwa ndiyo maana wamekuwa wakiiomba serikali wakati inaendelea na kujipanga kwa ajili ya kuwa na idadi ya kutosha ya walimu, basi ipunguze baadhi ya vikwazo na kuruhusu walimu kutoka nje ya nchi kuja kufundisha nchini.
“Walimu wa nje wanakuja ili kuwasaidia Watanzania ambao wana upungufu wa walimu maana kwao wapo wa kutosha tena wenye uwezo, shule binafsi hatupangiwi walimu, tunachokifanya tunatafuta wenyewe na ndiyo maana shule nyingi binafsi zinatumia walimu wa kigeni,” anasema.
Anatumia fursa hiyo kuiomba serikali kuvipitia upya vyuo vyote vya walimu ili kujiridhisha kama walimu wanaohitimu wameandaliwa inavyostahili, na kama wanao uwezo wa kufanya kazi hiyo vizuri, ili kupunguza tatizo la kuzalisha baadhi ya walimu wasio na viwango.
Anasema kuwa,baadhi ya walimu wanaohitimu vyuo vya hapa nchini kama hawajafuatiliwa vizuri inaweza kudhaniwa wanao uwezo wa kufundisha vizuri lakini wakifanyiwa usaili na kufuatiliwa uwezo wao wa kufundisha, inagundulika kuwa wana mapungufu makubwa.
Anaitaka serikali kuondoa vikwazo vilivyopo vinavyosababisha shule binafsi kushindwa kuajiri walimu wa kutosha kutoka nje ya nchi, ikiwamo kikwazo cha gharama kubwa inayotolewa kwa ajili ya kumpatia mwalimu wa nje leseni ya kufanya kazi hapa nchini.
“Kila mwalimu inabidi kumlipia dola 1,000, gharama hii ni kubwa sana na wakati huo huo serikali inatambua upungufu mkubwa wa walimu uliopo hasa wa masomo ya sayansi,” anasema Katiti.
Anasema kuwa, kama serikali inataka kusaidia sekta ya elimu iangalie namna ya kupunguza au kuondoa vikwazo, hasa kwa walimu wanaotoka katika nchi za Afrika Mashariki, ili shule hizo ziwe na uwezo wa kupokea walimu wa kutosha wenye uwezo wa kufanya kazi na kuwasaidia watoto wa Kitanzania kupata elimu bora.
“Shule yetu ina walimu 29 wa Kitanzania, lakini mbali na hao kuna walimu 22 wa kutoka nje ya nchi, hawa bado tunaendelea kushughulikia vibali vyao ili washirikiane na wazawa kufundisha, tunaomba serikali itusaidie vibali visichelewe,” anasema Katiti.
Pamoja na umuhimu wa walimu wenye sifa, meneja huyo wa shule anaona pia kuwapo kwa mlo wenye viwango bora kwa wanafunzi ni muhimu na kuwa watoto inabidi wapewe vyakula vya kuwasaidia kujenga mwili na kuwafanya kuwa na afya bora.
“Mtoto mwenye afya bora, lazima awe na uwezo darasani, lakini kama mtoto hana lishe bora hawezi kuzingatia masomo, na ndiyo maana hapa shuleni watoto wanabadilishiwa vyakula kila siku, baadhi ya vyakula wanavyotumia ni wali, pilau, ndizi na ugali, pia wanakunywa chai na uji,” anasema.
Anasema kwa upande wa mboga wanatumia samaki, nyama, maharage, mboga mboga, pia wanatumia matunda kama maparachichi, mapapai, ndizi mbivu, machungwa na nanasi. “Tunajitahidi watoto wapate mlo kamili” anaongeza.
Aidha anasema suala la uzingatiaji wa muda wa masomo ni muhimu na kuwa katika shule hiyo siku ya Jumatatu hadi Ijumaa kuanzia saa moja kamili hadi saa kumi jioni, kila siku watoto wanakuwa darasani.
“Baadae kuanzia saa moja usiku hadi saa 2:30 wanasoma masomo ya usiku, kila siku isipokuwa siku za Jumamosi na Jumapili,” anasema.
Hata hivyo, bado anaona michezo ni muhimu sana katika kujenga afya ya mtoto na kuwa kwa kuzingatia hilo kila Jumamosi na Jumapili majira ya mchanawatoto wanakwenda kwenye michezo hadi saa 12 jioni. Kuna michezo ya aina mbalimbali ikiwamo mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu na kukimbia.
Katiti anaitaka jamii kuacha dhana kwamba, kufanya vizuri kwa shule binafsi katika mitihani ya taifa kunatokana na udanganyifu ikiwamo kuiba mitihani, kupata mitihani kabla na kuingiza walimu katika vyumba vya mitihani siku za mitihani, na kuwa matokeo mazuri yanatokana na shule hizo kufundisha kwa bidii.
Anasema kuwa mtazamo huo sio wa kweli, maana kauli za hivyo hazitumiki kwenye masuala ya mitihani tu hata katika masuala ya kisiasa mtu yeyote anayefanya vizuri, utasikia kuwa ametumia njia zisizo sahihi.
“Napenda kuthibitisha kuwa, katika shule ya Kaizirege hakuna suala kama hilo, tunachokifanya ni kuwaandaa vizuri wanafunzi, na ngazi yeyote ya serikali ambayo wanahisi kuna udanganyifu unafanyika, sisi tuko tayari serikali ichunguze, inawezekana katika shule nyingine wanafanya lakini sio hapa” anasema.
Anasema ushindi wa shule hiyo unatokana na mambo makuu matatu ambayo ni kufanya kazi kwa bidii na kusimamia mikakati wanayojiwekea ili kutoa elimu bora, kuhakikisha nidhamu inakuwapo kwa wafanyakazi wote na wanafunzi, na kuhakikisha wafanyakazi wanapata stahili zao kwa wakati na kutoa motisha.
Yonah Ludomya ni mkuu wa shule ya sekondari Kaizirege, anazungumzia ushindi ambao wamekuwa wakiupata kuwa huupokea kwa furaha maana ni msingi na dira ya shule hiyo kufanya vizuri, baada ya kutoa taaluma iliyo bora inayolenga kutoa matokeo mazuri, na kufanya kuwapo kwa watoto wenye ubora katika taifa.
“Ushindi tunaoupata mbali na kutokana na nidhamu pia masuala kama utoaji wa taaluma bora, lishe, afya, malezi bora na mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia, kufanya kazi kwa bidii na kwa kushirikiana ni nguzo tunazozisimamia,” anasema.
Aidha mkuu huyo wa shule anaiomba serikali, kuzidi kufuatilia namna ya utekelezaji wa mitaala shuleni kupitia idara zilizopo chini ya wizara ya elimu mfano kitengo cha ukaguzi, na kuhakikisha utoaji wa elimu katika shule unazingatia mitaala iliyopo.
“Kitengo cha ukaguzi kisizembee, kikague shule zote na kuangalia kama misingi ya shule na ubora wa elimu inayotolewa kwenye shule kama inakidhi viwango, naishukuru serikali ya awamu ya tano ambayo sasa imeanza kuangalia shule zinatoa elimu kwa viwango gani na ubora upi” anasema.
Anasema serikali inapaswa kuimarisha zaidi kitengo hicho cha ukaguzi wa shule, ili shule zitakazobainika kuwa hazina uwezo wa kutoa elimu bora zishauriwe namna ya kufanya, na zitakazoshindwa kuzingatia ushauri huo basi zifungiwe kutoa huduma hiyo, lengo ni kutengeneza raia wenye uwezo wa kuleta ushindani katika soko la ajira, ndani na nje.
Shule ya sekondari Kaizirege mwaka jana ilihitimisha wanafunzi 72 ambao wote walipata daraja A na kuifanya kushika nafasi ya kwaza kitaifa kwa mara ya tatu mfululizo, tangu mwaka 2013, 2014 na 2015. Shule hiyo sasa ina wanafunzi 464.










