Kutokana na urefu, nguvu na kipaji cha soka alichojaliwa, mabeki wa Al Ahly walionekana kumfuata kwa tahadhari, huku pia kukiwa na wasaidizi ambao walikuwa tayari kumsaidia yeyote atakayepitwa na straika hiyo.
Kocha wa Al Ahly, Martin Jol, baada ya mechi ya Dar es Salaam kumalizika alimsifu straika huyo na kusema kuwa aliwaweka roho juu muda wote wa mchezo na aliwaambia mabeki wake kuwa makini sana naye.
Kwenye mechi ya pili iliyochezwa nchini Misri, kwa sababu hata mabeki wa timu hiyo akili yao ilikuwa ni kuwasaidia viungo na washambuliaji kupeleka mashambulizi mbele ili kupata magoli, walifanya kosa moja ambalo Ngoma alilitumia kuukwamisha mpira wavuni na kuandika bao la kusawazisha.
Goli hilo liliwaweka roho juu wachezaji, viongozi, makocha na mashabiki wa Al Ahly waliokuwa nyumbani wasijue nini hatma ya timu yao, iliyoonekana imebanwa vilivyo na mabingwa wa soka Tanzania Bara.
Bahati mbaya sana, timu yake ya Yanga ilifungwa goli kwenye dakika za majeruhi na kutolewa kwenye mechi hiyo ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa sasa anatarajia kuyahamisha makali yake kwenye Kombe la Shirikisho la CAF.Sasa amedhihirisha kuwa ni mmoja wa mastraika wachache bora kabisa kutoka nje ya nchi walioingia Tanzania kucheza soka la kulipwa kwa siku za karibuni, wakiongozwa na Emmanuel Okwi.
Ingawa aina ya uchezaji wao inatofautiana, lakini anafanana na Okwi kwenye uwezo wa kuipigania timu kwa machozi, jasho na damu, na pia uwezo wa kuamua kuibeba kwa mikono yake mwenyewe wakati inapokuwa ipo kwenye hali mbaya na mbinu nyingine zote kushindikana.
Anafanana sana na Mganda huyo anayecheza soka la kulipwa nchini Denmark kwa sasa, katika kuisaidia timu kwenye mechi za kimataifa kama alivyoisaidia Simba kuing'oa ES Setif 2012, na kuibeba Yanga kwenye mechi dhidi ya Al Ahly 2014 hadi kutolewa kwa mikwaju ya penalti.
Ngoma anaweza kuwa msaada mkubwa kwa viongozi wa klabu za Simba, Yanga na Azam ambao wataamua kusaka washambuliaji nje ya nchi.
Kwenye Ligi Kuu Tanzania amekuwa akiwapa wakati mgumu mabeki wengi jinsi ya kumkaba kiasi kwamba wamekuwa 'wakizikoga' kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya.
Hali hiyo imesababisha straika wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Dua Said, kutoa somo kwa mabeki jinsi ya kumkaba.
"Wataendelea sana kutolewa kwa kadi nyekundu kama watakuwa wanaruhusu awaegemee. Ngoma ni mjanja sana,
anamuegemea beki na kwa sababu ana nguvu huwezi tena kumdhibiti, lakini dawa yake ni kutoruhusu kabisa akuegemee na wewe fuata mpira tu, hapo itakuwa umemuweza," anasema Dua.
Kwa sasa ana magoli 14 kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.Uwezo wake ni wa kucheza kwenye ligi au timu yoyote kubwa barani Afrika, akiwa na umri wa miaka 27 sasa tangu alipozaliwa nchini Zimbabwe Februari 4, 1989.
Yanga ilimsajili msimu huu akitokea FC Platinum.










