JOHANSEN: avunja kikwazo cha yatima na kupaa kielimu

26Apr 2016
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
JOHANSEN: avunja kikwazo cha yatima na kupaa kielimu

JOHANSEN Joseph ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Minziro iliyoko wilayani Missenyi mkoani Kagera.Kwa sababu ya, kufiwa na baba yake mzazi akiwa na umri mdogo alilazimika kufanya vibarua ili amalize elimu yake ya msingi.

johansen Joseph.

Joseph anayelelewa na bibi yake aitwaye Leonsia Mattelo anasema, baada ya kufiwa na baba yake na kubaki na mama yake, ambaye hakuwa na kipato chochote alianza kuchota maji na kuuza ili kupata mahitaji ya shule.

“Nilisoma kwa shida sana, nikajisikia kukata tamaa nikataka kuacha shule lakini Mungu alinisaidia nikaona ili nifanikiwe katika maisha yangu lazima niwe na elimu, ikabidi nichote maji yakuuza ili nipate fedha za kununulia sare na mahitaji mengine ya shule,” anasema.

Anasema alipomaliza darasa la saba mwaka 2010 alichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari lakini kutokana na hali ngumu ya maisha katika familia yao hakujua kama ataweza kuendelea na masomo.

“Nilianza kuhangaika kuomba msaada kwa watu mbalimbali ili niendelee na elimu ya sekondari, kwa bahati nzuri nikaitwa na uongozi wa mfuko wa maendeleo ya elimu wa kata Minziro, wakakubali kunilipia mahitaji ya shule kwa miaka yote minne” anasema Joseph.

Anasema mwaka 2011 alianza kidato cha kwanza na sasa amehitimu kidato cha nne katika shule hiyo akichukua masomo ya sayansi.

“Nina imani nitafanikiwa, na nikifanikiwa nitajitahidi kuwasadia wengi watakaokuwa na matatizo kama yangu kupitia katika mfuko huu” anasema.

Anasema alijitahdi kusoma kwa bidii ili kuwatia moyo wanaomsaidia .Katika mtihani wake wa mwisho wa kuingia kidato cha nne alishika nafasi ya pili.

“Malengo yangu ni kuwa daktari wa binadamu, nina uhakika ndoto zangu siku moja zitatimia ili niweze pia kusaidia familia yangu hasa wadogo zangu” anasema.

Katika familia yao anasema kuwa, walizaliwa yeye akiwa mtoto wa kwanza na kwamba wadogo zake wengine wanaishi mazingira tofauti maana wamechukuliwa na jamaa wengine.

Joseph anawashauri wanafunzi wanaopatiwa misaada kwa ajili ya kusoma, waitumie misaada hiyo vizuri kwa kusoma kwa bidii na kukabilioana na mazingira magumu waliyonayo.

Wakifanya hivyo anasema kwamba, itawasaidia baadaye kutimiza ndoto zao za kuwa na maisha mazuri na kusaidia kuinua uchumi katika familia zao.

Katibu wa Mfuko wa Elimu katika kata ya Minziro unaomfadhili masomo mtoto huyo Bethuel Elias anasema kuwa, tangu mwaka 1998 wamefadhiliwa gharama za masomo kwa wanafunzi 31.

Elias anasema kuwa, watoto wanaosaidiwa ni yatima na wengine wanatoka katika familia za watu wasiojiweza, lengo ni kuwawezesha kupata elimu kwa manufaa yao ya baadae.

Anasema kuwa fedha za kuwafadhili masomo wanafunzi wanaosoma katika shule ya sekondari Minziro, zinatolewa na chama cha Wanaminziro waishio Ujerumani cha Entwicklungsverein e.v. kupitia katika mfuko huo.

Anasema kuwa wanafunzi wanaofadhiliwa kupitia mfuko huo wanaoendelea na masomo husomeshwa hadi elimu ya vyuo ili kuwawezesha kupata ajira na kuweza kujitegemea katika maisha yao.

“Mtoto akimaliza kidato cha nne ukaachana naye, unakuwa hujamsaidia chochote maana elimu ya kidato cha nne tu inaweza isimsaidie zaidi, ndiyo maana tunawalipia hadi gharama za vyuo vikuu,” anasema.

Anasema wamepokea sh. milioni 6.1 kutoka chama cha Entwicklungsverein e.v. kwa ajili ya matumizi ya shule kwa wanafunzi 15 wanaoendelea na masomo katika ngazi mbalimbali.

Wakati watu binafsi, vyama na mashirika yasiyo ya kiserikali wakijitokeza kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kielimu, pia serikali kupitia katika halmashauri, nayo haiko nyuma.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara ya maendeleo ya jamii wilaya ya Missenyi, watoto mbalimbali hupatiwa misaada kulinga na fungu linalopatikana kwa ajili hiyo.

Anna Ndile ambaye ni Ofisa katika Idara ya Maendeleo ya Jamii wilayani humo, anasema katika mwaka wa fedha 2012/2013 watoto 900 wamepatiwa huduma za elimu.

Kwa mujibu wa Ndile idadi hiyo inajumuisha wanafunzi wa shule za sekondari 600 ambao walilipiwa ada za shule na wanafunzi 300 wa shule za msingi ambao walipatiwa vifaa mbalimbali vya shule.

Anasema kuwa, katika kitengo hicho hawatoi msaada wa kielimu tu bali pia hupokea malalamiko yanayohusu manyanyaso kwa watoto na kuyapatia usuluhishi.

Anasema kuwa jumla ya mashauri 26 yanayohusu unyanyasaji wa watoto yaliwasilishwa katika kipindi hicho, mashauri 24 yamesuluhishwa na mawili yamepelekwa ngazi za juu kwa msaada zaidi wa kisheria.

Ndile anasema, uchunguzi umebaini kuwa watoto wengi huteseka katika jamii kutokana na wanajamii wenyewe kushindwa kuweka mipango ya kuwahudumia kutokana na kuzaliwa katika familia maskini na wengine baada ya kufiwa na wazazi wao.

“Baada ya kuona familia zimesahamu majukumu yao katika kuhudumia watoto na kusababisha ongezeko la watoto wa mitaani, wilaya yetu imeanzisha mkakati wa kuhakikisha jamii inabadilisha mtazamo na kuona kuwasaidia watoto hao ni jukumu lake” anasema.

Aidha anasema kuwa ,pia wameweka mipango itakayowezesha elimu inatolewa sawa kwa wasichana na wavulana, ili waweze kujitegemea katika maisha yao ya baadae.

Anasema kuwa pia wilaya hiyo inapambana na ajira mbaya kwa watoto na mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Ukimwi ambao nao umekuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la watoto yatima.

Anasema jitihada nyingine ni kuihamasisha jamii kuanzisha vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) na Vicoba ili kujipatia kipato kwa ajili ya kuzihudumia familia zao na watoto wahitaji.

KUNA usemi usemao kwamba, kama unaona elimu ni ghali basi jaribu ujinga. Usemi huu unawafanya watu wengi hata wasio na uwezo wa kifedha kujituma ili waweze kupata elimu.