MAHOJIANO: Spika Wawakilishi awapongeza Seif, Shein kudumisha amani

23Apr 2016
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
MAHOJIANO: Spika Wawakilishi awapongeza Seif, Shein kudumisha amani

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zuberi Ali Maulid, amempongeza Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kutoamuru wafuasi wake wafanye vurugu baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa marudio visiwani hapa.

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Zuberi Ali Maulid.

Aidha, Maulid amempongeza pia Rais Dk. Ali Mohammed Shein kwa kudumisha amani iliyopo Zanzibar licha ya kisiwa hiki kupita katika wakati mgumu kisiasa, baada ya kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kuamriwa kuwapo uchaguzi wa marudio wa Machi 20.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu wiki hii, Maulid alisema "nitampongeza (Maalim Seif) kwa sababu angeweza hata kuwashauri wafuasi wake kufanya vurugu baada ya kuona hajakubaliana na hali inayoendelea.

"Lakini kwa sababu ya umri wake na dhima yake kwa Mwenyezimungu akahisi asiwapeleke watu katika janga hilo na kuepuka kubeba mzigo wa dhima."

Maulid ambaye aliwabwaga wapinzani wake wawili katika kinyang'anyiro cha uchaguzi huo, akiwemo Spika Mstaafu Pandu Ameir Kificho, alisema pia anamshauri Maalim Seif kutafuta suluhu ya msimamo wa chama chake ili ifikapo mwaka 2020, Zanzibar iwe kisiwa cha amani tayari kwa uchaguzi huru na wa haki.

Akijibu moja ya maswali ya Nipashe, spika Maulid alisema anampongeza Dk. Shein kwa kuweza kudumisha amani kwa sababu watu wangeweza kufanya vurugu katika kipindi cha kati ya chaguzi hizo mbili.

"Kwa sababu ya hekima yake, tunaona hali iliyopo," alisema Maulid na kueleza zaidi Maalim Seif na Dk. Shein wanahusika kuwepo kwa amani Zanzibar.

"Lakini pia ningemshauri Dk. Shein kama CUF wakitaka kusikilizwa awape nafasi ya kuwasilikiza halafu baadae tukajuwa tunapoelekea kutakuwa na amani kiasi gani."

Yafuayato ni mahojiano kamili kati ya Nipashe na spika Maulid:

SWALI: Utaongoza Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa asilimia 99, je mtaepukaje kuwa sehemu ya Serikali kwa kutopitisha miswada na maazimio kirahisi?

JIBU: Nimewahi kuwa mwakilishi mwaka 2000-2005. Pamoja na kwamba Zanzibar ilikuwa tayari katika mfumo wa vyama vingi, lakini wezetu wa CUF (chama cha Wananchi) waligomea baraza na wakati huo mimi nilikuwa Waziri, sehemu ya serikali.

Lakini sikuona tofauti katika masuala ya uendeshaji wa baraza na michango, na hata wakati ambapo wapinzani walirudi barazani hakukuwa na tofauti.

Hali ilikuwa ni ileile. Unapoendesha baraza au bunge ambalo limetawaliwa na chama kimoja, wajumbe waliopo huwa kama ni wapinzani wa serekali.

Huihoji, na mambo mengine yote yatakuwa na msisitizo kwa sababu wajumbe huchukuwa nafasi ya wapinzani kuibana serikali.

Kwa hiyo sidhani kwa kuwa wajumbe wote katika baraza hili ni kutoka chama kimoja (CCM) baraza litakuwa ni la ubabaishaji, mimi kama spika nitakachotakiwa kukifanya ni kuendesha baraza kwa mujibu wa kanuni na nitakuwa kama refarii.

Kwa hiyo wananchi watarajie kuwa baraza hili nitaliendesha vizuri.

SWALI: Hivi sasa kuna mgawanyiko mkubwa Zanzibar kiitikadi na uchaguzi mkuu wa marudio ni kama umeongeza mgawanyiko huo. Je, hili unalizungumziaje?

JIBU: Zanzibar kihistoria hali hii iliyopo ni ya kawaida na unaweza kuitofautisha na Tanzania Bara. Huku tuna upinzani mkubwa wa kisiasa na ndiyo maana kuna mvutano.

Ni hali ya kawaida na wakati mwingine inatupelekea kwenye vurugu. Lakini mara hii tunashukuru sana kwamba hali imekuwa ya amani sana, na ni ngumu sana kuibadilishika kwa sababu siyo rahisi kubadilishika.

Na tukitaka tuibadilishe ni lazima tuseme tunapiga marufuku vyama vya siasa, lakini sasa ni wakati wa kidemokrasia sio rahisi kuua vyama, tofauti zitaendelea kuwepo lakini tofauti zetu tuzitumie vizuri.

Tutofautiane katika itikadi bila ya kuleta vurugu au maafa kwa watu.

SWALI: Utafanya jitihada gani kuhakikisha kuwa Baraza la Wawakilishi linawawakilisha kweli Wazanzibari wote na siyo kuonekana ni la maslahi ya CCM?

JIBU: Wawakilishi hawakuteuliwa tu na chama halafu wakaja barazani, walikwenda kupigiwa kura na wananchi jimboni.

Kwa hiyo wanawajibika kwa wananchi waliowachagua, lakini kikubwa zaidi ukishakuwa mwakilishi unatumikia watu wote sawia. Kwa hiyo uwakilishi ulioko ni wa wananchi na sio wa CCM.

SWALI: Kwa mtazamo wako nini sasa kifanyike ili Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iwe ya kweli visiwani Zanzibar na sio kama ilivyo sasa?

JIBU: Cha kufanya kwa sasa hakipo. Lakini nashauri wezetu wa CUF washiriki katika uchaguzi wa mwaka 2020 ambapo chama kitakachopata ushindi kitaunda serikali kwa kushirikiana na chama kilichopata asilimia inayotakiwa na katiba ya Zanzibar kuunda serikali yenye sura halisi.

Lakini kwa sasa haiwezekani kwa sababu hakuna chama cha upinzani kilichopata angalau asilimia 10 ya kura za Urais wa Zanzibar.

SWALI: Leo hii ukikutana na viongozi wa CUF kama Maalim Seif Sharif Hamad, ni mambo yapi matatu muhimu utawaambia? Na mambo yapi matatu muhimu utawaambia viongozi wa CCM kama Dk. Ali Mohammed Shein?

JIBU: Kwanza Maalim Seif nitampongeza kwa sababu angeweza hata kuwashauri wafuasi wake kufanya vurugu baada ya kuona hajakubaliana na hali inayoendelea, lakini kwa sababu ya umri wake na dhima yake kwa Mwenyezimungu akahisi asiwapeleke watu katika janga hilo na kuepuka kubeba mzigo wa dhima. Kwa hilo nitampongeza.

Lakini lingine ningemshauri basi ifike pahala akae na wenzake katika vyama na serikali watafute namna ya kufikia suluhu ya jambo hili hatimae tunapofikia mwaka 2020 Zanzibar iwe kisiwa cha amani kama vile ambavyo tunasifika.

Dk. Shein nae nitamsifu kwa kuweza kudumisha amani ambayo tunaiona kwa sababu watu wangeweza kufanya chochote, lakini kwa sababu ya hekima yake tunaona hali iliyopo kwa hivyo wote wawili wanahusika kuwepo kwa hii amani.

Lakini pia ningemshauri Dk. Shein kama CUF wakitaka kusikilizwa awape nafasi ya kuwasilikiza halafu baadae tukajuwa tunapoelekea kutakuwa na amani kiasi gani.

SWALI: Je unazungumziaje uamuzi wa wahisani kama Marekani kusitisha misaada kwa taifa kwa sababu ya uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar?

JIBU: Kwa bahati nzuri mimi kabla ya kugombea uspika niliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Muungano na nilikuwa katika Kamati ya Hesabu za Serikali kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa hiyo hali halisi ya mahesabu ambayo wananchi hawaielewi, mimi imo kichwani mwangu.

Kila kinachoahidiwa na wahisani na wanachokitoa na wakati mwengine kile wanachokitoa ambacho kinafungamana na masharti ya kitu gani kifanyike katika utawala, sio kitu ambacho nakiunga mkono sana.

Mimi naunga mkono zaidi kujitegemea kwa asilimia 100 kama inawezekana. Misaada inahitajika lakini misaada inayofungamana na masharti basi nchi ingejitahidi kuiepuka, tuanze kujitegemea tutaheshimika zaidi kuliko kuwa tegemezi tukadharaulika.

Kwa hiyo mwenendo anaokwenda nao Rais John Magufuli ninaukubali; ni mwenendo mzuri kwa sababu unatusukuma katika taifa la kujitegemea zaidi kuliko kutegemea misaada.

SWALI: Hapo kabla wengi hawakutarajia kuwa utashinda kiti cha Spika hasa kutokana na ushindani ulokuwapo ndani ya CCM. Tupe siri ya mafanikio yako hadi kushika mamlaka ya juu ya Baraza la Wawakilishi.

JIBU: Mimi nimegombea kama mwanachama wa kawaida wa CCM, niliposikia tangazo la kuomba uspika niliomba kama walivyoomba wengine. Tulikuwa tisa lakini baadae chama kikachuja majina na tukabakia watatu akiwemo Spika Mstaafu, Pandu Ameri Kificho.

Tukajieleza mbele ya wawakilishi na wao ndiyo waliofanya maamuzi na kura zikaamuwa kuwa mimi ndiyo niwe spika, hakuna uchawi kwa kweli. Siri siijui, ni bahari tu.

Labda baadhi ya wajumbe waliniona wakati nilipokuwa mwenyekiti wa Bunge mwaka 2002 hadi 2010 na kuweza kukalia kile kiti labda ndiyo maana wakanipa imani hiyo, sina uhakika na hilo.

SWALI: Muundo wa serikali ya sasa hauendani na matakwa ya katiba ya Zanzibar, hasa kukosekana kwa nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais. Kama Spika wa Baraza la Wawakilishi hili unalizungumziaje?

JIBU: Katiba na sheria zimeeleza jinsi makamu wa kwanza wa Rais anavyopatikana. Lakini sifa hazikufikiwa. Lakini pia katiba ipo kimya inapotokea kuwa sifa hizo hazikufikiwa tunafanyaje.

Haina maana kuwa sifa zisipofikiwa turudi katika uchaguzi, hapana. Ni kuendelea kuunda serikali bila ya kuwepo chama cha upinzani, labda kama unaniuliza tunaendaje wakati serikali imeshaundwa? Sijui.

Lakini je, tutahitaji kubadilisha turudi tena katika ule mfumo? Sijui kwa sababu wa kuamua ni wananchi.

Ni wao wa kuwashauri waliowapigia kura ili wafanye maamuzi na hilo suala linahitaji mabadiliko ya katiba, lakini mimi kwa ushauri wangu masuala yote hayo tuyapime na tuyaangalie ni nini faida na zipi ni hasara tunapokuwa na SUK na tusipokuwa na SUK.

Kwa hiyo tukivipima vitu viwili hivyo na tukagundua kuwa faida zinazohusiana na mfumo mmoja wapo ni nyingi zaidi kuliko hasara, tunaweza kubaki katika mfumo huo wenye faida nyingi au kurudi katika mfumo wa serikali ya chama kimoja. Hilo sio langu mimi.

SWALI: Nini ushauri wako kwa Wazanzibari na wajumbe wa baraza la wawakilishi?

Baraza linaenda vizuri. Niwashauri wazanzibari na wajumbe tuijenge nchi yetu na tudumishe amani ya nchi; mwaka 2020 penye uhai sio mbali sana watu wajiandae na kushiriki uchaguzi ili tuijenge nchi yetu.