Na tunaweza kusema tu kuwa kama unaipata fursa basi ni vema sana ukajitiahidi kuitumia fursa hiyo kufahamu japo machache kuhusiana na sheria hii.
Uelewa wa sheria hii ya Mwenendo wa Kesi za Madai ni muhimu kwa sababu ndiyo inayotawala mashauri takribani yote kuhusiana na kesi za madai hapa nchini Tanzania.
Kesi za madai ni zile ambazo hazihusiani na jinai moja kwa moja, japo hutokea sheria za jinai zikaweza kurejewa katika mahakama za madai na pia kinyume chake (yaani sheria za madai kutafsiriwa pia wakati kesi fulani ya jinai ikiendelea).
Sheria hii, ambayo tunawajuza leo kupItia safu hii inaitwa Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Madai (kimombo ikijulikana kama Civil Procedure Code).
Sheria hii tunayotumia sasa ni ya mwaka 1966 (kama ilivyohakikiwa upya sambamba na sheria nyingine takribani zote za nchi hii zilizokuwa zikitumika kufikia mwaka 2002). Sheria hii hutajwa pia kama Sura ya 33 ya Sheria za Tanzania (toleo lililohakikiwa). Hata hivyo sheria hii imejulikana zaidi kama CPC (kifupi cha maneno ya kimombo ‘Civil Procedure Code’).
Basi, haitakustaajabisha sana uwapo katika duru la kimahakama kuwasikiliza waheshimiwa Majaji, mahakimu, Mawakili, waendesha Mashtaka pamoja na makarani wa mahakama wakitamka neno hili ‘CPC’ popote zilipo mahakama zetu hapa nchini.
Hii ni kwa sababu, kama tulivyodokeza awali, Sheria hii ndiyo kila kitu linapokuja suala la uendeshaji wa kesi za madai, iwe ni shauri la ardhi, mkataba, kuhitilafiana baina ya mpangaji na mwenye nyumba, migogoro ya kazi, kesi za mirathi na talaka, mashtaka baina ya mtu na serikali, mashauri ya Katiba na kila kesi nyingine ambamo jinai haihusiki moja kwa moja ama inahusika kidogo sana.
Izingatiwe pia kuwa, ni muhimu uelewe kuwa matumizi sahihi ya sheria hii yanapaswa kuhusisha mabadiliko yake na hasa mabadiliko madogo yaliyofanywa kupitia matangazo ya Serikali yaliyotolewa mwaka 2010 na pia mwaka 2011, na pia mabadiliko mengine kupitia sheria nyinginezo zenye kuathiri matumizi ya sheria hii.
Dhumuni kubwa la kutumika kwa sheria hii ni kudhibiti mienendo ya kesi mahakamani, kuokoa muda wa mahakama, kujenga nidhamu baina ya wanaoshtaki na wanaoshtakiwa katika daawa, kupunguza mianya ya udanganyifu, rushwa ama hila fulani fulani kutokea tofauti na kama sheria hii isingekuwepo (hata hivyo zipo nyakati ambapo kanuni zilizomo nani ya sheria hii zimetumika kunyima haki stahiki na hivyo kutafsiriwa na wengine kuwa sheria hii imechochea kuweko rushwa mahakamani kwa vile wapo waheshimiwa katika mhimili wa Mahakama na mawakili wajanja-wajanja ambao wameitumia kugandamiza haki kwa sababu japo walitambua fika kuwa mtu fulani kama kesi ingeendeshwa pasipo kuzingatia sana kanuni za kimwenendo (rules of procedures) yule anayeshinda kwa kunufaika nazo asingestahili kushinda kesi).
Hata hivyo, pamoja na mapunufu yake, sheria hii ni muhimu na inapaswa kuendelea kuwepo kwa sababu manufaa yake ni makubwa kuliko ambavo kama isingekuwepo.
Na ukweli wa msimamo huu utaufahamu tu pale utakapotumia muda wake, kuisoma na kuilewa zaidi sheria hii ambayo kwa tahadhari tu ni kuwa mtu wa kawaida si rahisi kuielewa pasipo kuwa na misingi ya kufundishwa na wanazuoni wa sheria.
Tunasema hivi kwa sababu, hata miongoni mwa wanasheria wapya na wazoefu pia bado yapo mambo mengi ya kitafsiri ambayo yameendelea kuwasumbua katika matumizi ya sheria hii.
Na kwa vile muogoleaji mzuri hapaswi kuogopa maji ya kina kirefu, bado pia unaweza kujifunza zaidi kuifahamu sheria hii pamoja na ugumu wake. Na hakuna mahali mazuri pa kuanzia kama kupitia machapisho yanayokubalika ndani ya tasnia hii.
Machapisho ya hayati Jaji Chipeta, Dk.Sengondo Mvungi, Profesa Mgongo Fimbo na Pia Dk. Masumbuko Lamwai ni kati ya yaliowasaidia wengi hapa nchini kuielewa zaidi sheria hii na wewe unaweza kufuata mkondo huu pia. Kwa machapisho ya nje ya Tanzania, pengine hakuna nchi yenye wanazuoni mahiri katika kuielewa sheria hii kama India (pamoja na sheria za mienendo na pia zile za Ushahidi).
Nenda katika duka lolote la vitabu na uulizie machapisho ya Mulla on the Indian Civil Procedure Code ama Sarkar on the Indian Civil Procedure Code basi utakuwa na msingi mzuri sana wa kuielewa sheria hii, kama utaielewa.
Mwisho, lakini muhimu zaidi, itafute sheria yenyewe katika maduka ya vitabu vya Serikali, Ofisi za Mawakili. Bahati nzuri pia Sheria hii utaipata katika mtandao kupitia tovuti ya Google. Nimekusaidia uipate kirahisi kama utaingia katika ‘Google’ halafu chapa maneno haya ‘Denis Maringo Civil Procedure Code Tanzania’.
Ila nikutahadharishe tu kuwa ,kile kilichoko katika mtandao hakijumuishi mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa kupitia sheria hii tangu ilipotumwa mtandaoni.
Katika makala yanayofuata tutaipitia sheria hii kwa kuvichambua vifungu muhimu zaidi kwako wewe msomaji, japo tutafanya hivyo kwa kifupi sana.
Tafadhali usikose kwa sababu yale utakayopata ni sehemu ya elimu muhimu zaidi ambayo umewahi kuipata hapa duniani. Kaa mkao wa kula.
*Denis Maringo ni Mwanasheria aliyeko Dar es Salaam. Mawasiliano: simu: 0719270067. Barua-pepe: dnmaringo@gmail.com










