Shule hiyo ilipokea wanafunzi wa kwanza mwaka 1965, ikiwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 288 wa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Mwaka 1970 ilianza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na mwaka 1971 ilitaifishwa na serikali kutoka mikononi mwa kanisa Katoliki.
Pamoja na ukongwe wa shule hiyo yenye wanafunzi wa kike pekee, bado inaendelea kusifika kwa kuendelea kusimamia maadili ya watoto wanaosomea pale, huku ikiendelea kupata ushindi wa wastani katika matokeo ya mitihani ya taifa.
Mwaka 2010 shule hiyo ilianza kupokea wanafunzi wenye ulemavu mbalimbali ikiwamo wa viungo, wasioona, wasio sikia na albino. Kuanza kupokelewa kwa wanafunzi wenye ulemavu kumechangia kuongeza changamoto zinazoikabili shule hiyo, kutokana na kutokuwapo kwa mazingira rafiki ya kundi hilo.
Jonatha Semeo ni mwanafunzi mwenye ulemavu wa viungo anayesoma kidato cha pili katika shule hiyo, anasema kuwa kutokana na kutokuwapo kwa miundombinu rafiki, hali imekuwa ikisababisha baadhi ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo kubebwa na wanafunzi wenzao kuwapandisha katika ghorofa ya tatu, ili waweze kuingia darasani kujifunza.
“Wakati mwingine tunalazimika kuacha baiskeli zetu chini na kupandishwa darasani kwa msaada wa wanafunzi wenzetu.Tunawapa shida lakini kama ingekuwapo miundombinu rafiki, tusingekuwa tunawasumbua,” anasema Jonatha.
Tatizo jingine wanalokabiliana nalo ni kwa mujibu wa Jonatha ni wakati wa kwenda chooni maana ni vigumu kwenda kwa baiskeli.
“Tunalazimika kuacha baiskeli kuingia nayo chooni haiwezekani. Wakati mwingine vyoo vinakuwa vichafu, naomba tujengewe vyoo vyenye mazingira rafiki, ili kutuepusha na magonjwa,” anasema.
Wakati walemavu wa viungo wakilalamikia changamoto ya kubebwa ili kupelekwa darasani na vyoo visivyofaa kutokana na ulemavu walio nao, wanafunzi wenye uoni hafifu wanalalamikia kutokuwapo kwa vitabu vyenye maandishi makubwa ambavyo vingewawezesha kusoma vizuri.
Mmoja wa wanafunzi hao Janeth Msedem anasema kuwa, ukosefu wa vitabu vyenye maandishi makubwa huwafanya kulazimisha kusoma vitabu vyenye maandishi ya kawaida ambayo husababisha macho kutoa machozi wakati wa kusoma.
“Tunapotumia vitabu vya maandishi ya kawaida macho yetu hutoa machozi kwa sababu ya kuyalazimisha kusoma kitu ambacho hatukioni vizuri.Tunaomba kama serikali inatutambua na inatuonea huruma itusaidie juu ya hili” anasema Janeth.
Alvera Kashushura ni miongoni mwa wanafunzi wa kwanza na dada mkuu wa kwanza katika shule hiyo, anasema alimaliza kidato cha nne mwaka 1968.
Kashushura anasema kuwa, shule hiyo ilijengwa wakati huo na Kardinali Laurean Rugambwa maana alipenda sana watoto wa kike wapate elimu. “Alipenda kutuinua kielimu, alitusimamia na kuhakikisha tunafanya vizuri,” anasema.
Anasema kuwa wanafunzi wengi waliosomea katika shule hiyo miaka ya mwanzo walifaidi malezi mazuri waliyoyapata katika shule, ambayo yaliwawezesha kufaulu vizuri na kufanya kazi katika nyadhifa tofauti kwa uadilifu na uaminifu hata kuchangia kulijenga taifa.
“Hata ambao wamemaliza shule na kuwa mama wa familia tu waliweza kuzisimamia familia zao na kuwalea watoto wao katika maadili mema, kutokana na malezi bora waliyoyapata,” anasema.
Kashushura ambaye kwa sasa ni mkuu wa shule ya sekondari ya St. Joseph Kolping inayomilikiwa na kanisa Katoliki iliyoko katika manispaa ya Bukoba, anasema wakati huo walisomea katika mazingira mazuri maana mahitaji yao ya wakati ule yaliendana uwezo wa shule.
“Tulisomea katika mazingira bora, tulikuwa na walimu wa kutosha, lakini hata mitaala ilifuatwa,” anasema mama huyo mwenye taaluma ya ualimu.
Anasema changamoto za sasa zinaonyesha kuna uhitaji wa walimu lakini enzi zao hayakuwapo, na kuwa hali hiyo sio kwa Rugambwa pekee, bali ni kilio cha shule nyingi katika nchi nzima.
“Tatizo la Rugambwa kwa sasa ni miundombinu ya shule hasa majengo yanahitaji kuboreshwa maana yamejengwa miaka mingi iliyopita, ombi langu kwa serikali ifanye jitihada za makusudi kuweka mazingira yanayovutia” anasema.
Anasema majengo hayo ni ya zamani na kuwa serikali iyafanyie ukarabati wa kutosha ili wanafunzi waliopo waweze kusoma kwa amani,furaha na kuomba wapatikane walimu wazuri na wa kutosha ili heshima ya shule hiyo iendelee kuwapo.
“Rugambwa kuna wengi wamesomea hapa na wana mafanikio, lakini pia wana ndugu na jamaa zao ambao wanaweza kushirikiana nao kuboresha mazingira ya kusomea na kuendelea kutoa mazao bora ambayo yataendelea kuitangaza shule hii kwa ubora wao kitaaluma na kiutendaji,” anasema.
Pamoja na wataalamu wengine, miongoni mwa watu maarufu waliomalizia katika shule hiyo ni Profesa Anna Tibaijuka aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Makazi (UNHABITAT) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika serikali ya awamu ya nne.
Prof. Tibaijuka pia ni mbunge wa sasa wa jimbo la Muleba Kusini. Mwingine aliyesomea katika shule hiyo ni mkurugenzi wa zamani wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Valerie Msoka.
Godfrey Twende ni mwalimu mwandamizi wa miradi katika shule hiyo, anasema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutokuwapo kwa usalama wa kutosha kwa wanafunzi kutokana na ukweli kuwa shule hiyo haina uzio.
Changamoto nyingine anazitaka kuwani ufinyu na uchakavu wa bwalo la chakula lililojengwa mwaka 1963 kwa lengo la kuhudumia wanafunzi 288 wakati huo, kwa sasa linategemewa na wanafunzi zaidi ya 800.
Nyingine ni mabweni yaliyopo hayatoshelezi mahitaji pia kutokuwapo mabweni yenye miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu, ambao kwa sasa wanapelekwa katika shule hiyo tofauti na mazingira ya zamani.
“Hakuna pia madarasa yenye miundombinu rafiki na wanafunzi wenye ulemavu hasa wa viungo. Pia kuna tatizo la maji kukatika mara kwa mara linalotokana na miundombinu yake kuchoka, inabidi kuwekwa miundombinu mipya,” anasema.
Anaona pamoja na kuwekewa miundombinu mipya ya maji, pia inabidi kupatiwa matangi kwa ajili ya kuvunia maji ya mvua, ili waweze kupata maji hata ya bomba yakikatika.
“Hata umeme katika baadhi ya majengo miundombinu yake imechoka ni ya zamani, nayo inahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuweka mazingira salama kwa wanafunzi” anasema.
Kufuatia shule hiyo kuandamwa na matukio ya moto kipindi cha nyuma, bweni moja lenye uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 175 liliungua lakini hadi sasa bado halijafanyiwa marekebisho, hatua inayosababisha shule hiyo kupokea watoto kulingana na uwezo wa mabweni yaliyopo.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, mwalimu Twende anabainisha jitihada zinazoendelea kufanyika miongoni mwake ikiwa pamoja na kujiandaa kufanya jubilei ya miaka 50 itakayokwenda sambamba na harambee ya kuchangia maendeleo ya shule hiyo.
“Tunalenga kupata zaidi ya shilingi milioni 811 ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili shule hii, ikiwamo kujenga bweni lenye miundombinu rafiki na watoto wenye ulemavu, kujenga uzio wa shule na kukarabati bweni la zamani na jengo la utawala na kupanua bwalo la chakula” anasema.
Anasema ili kuhakikisha jubilei hiyo inafanyika hadi sasa wamekwishafanya makongamano mbalimbali kwa lengo la kuweka mikakati itakayowezesha kupatikana kwa fedha za kufanikisha kazi hiyo.
“Tunawashirikisha wadau mbalimbali wapenda maendeleo, watu waliomalizia katika shule hii, ndugu na marafiki wa shule, na tunawaomba wengine kujitokeza zaidi ili azma hii iweze kutimia, na hatimaye mazingira ya shule kuboreshwa na kuwafanya watoto kusoma kwa raha” anasema.
Kagemulo Lupanka ni mkuu wa shule ya sekondari Rugambwa anasema kuwa, endapo bweni lililoungua moto litakarabatiwa basi ni heri maana litawezesha idadi ya watoto wanaopelekwa katika shule hiyo kuongezeka.
“Tunapokea watoto kulingana na mabweni yaliyopo, kawaida wakati wa uteuzi huwa tunashirikishwa ili kujua uwezo wa shule, na inapotokea shule ikapewa wanafunzi wengi zaidi ya uwezo wake, inatokana na wingi wa wanafunzi wanaoshinda kujiunga na elimu ya sekondari kwa wakati huo,” anasema.
Anasema ili kudhibiti msongamano usiwe mkubwa katika shule hiyo, inapoonekana wamepokea watoto wengi zaidi ya uwezo wa mabweni yaliyopo, huruhusu wanafunzi wanaotaka kuhama lakini hawaruhusu wanaohamia.
Kuhusu miundombinu ya umeme ambayo ilitajwa kuwa ndicho chanzo cha kusababisha baadhi ya mabweni ya shule hiyo yenye majengo ya ghorofa kuungua moto mara mbili mfululizo na kusababisha uharibifu wa mali za wanafunzi na majengo, anasema kwa sasa imefanyiwa ukarabati.
“Tangu mwaka 2012 hadi sasa halijatokea janga lolote la moto baada ya miundombinu ya umeme iliyokuwa imechakaa kufanyiwa ukarabati, tulipata fedha shilingi milioni 50 kwa ajili ya ukarabati huo kutoka serikali kuu, ambazo zilitumika kukarabati umeme na baadhi ya majengo,” anasema.
Aidha kuhusu jubilei iliyokuwa ifanyike Machi mwaka huu kwa ajili ya kupata fedha za kuboresha mazingira ya shule hiyo, anasema kuwa baada ya kuona jamii haijahamasishwa kwa kiwango cha kutosha katika suala la kuchangia, imesogezwa mbele.
“Baada ya kuona fedha hazijapatikana za kutosha kwa ajili ya kufanya jubilei tuliona tusifanye kwanza badala yake tuendelee kuhamasisha, ili tuweze kupata watu wengi zaidi” anasema Lupanka.
Anasema kwa sasa wanalenga kuomba fedha kutoka kwa mashirika na makampuni mbalimbali ndani na nje ili kuwezeshwa, kwa kuandika maandiko ya miradi na kuyasambaza. Anatumia fursa hiyo pia kuwaomba wananchi wenye mapenzi mema na shule hiyo kujitokeza kuchangia.
Katika uendeshaji wa shule anasem, siku za nyuma walikuwa wakitegemea ada na michango mingine kutoka kwa wazazi, lakini sasa fedha kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo inatumwa na serikali, na kuwa hata kwa matumizi ambayo wanaona yako nje ya uwezo wa shule wanayapeleka serikalini.
“Mgawo unaotolewa na serikali kupitia mpango wa elimu bure sio mdogo maana unatolewa kulingana na mahitaji ya wanafunzi walipo, mfano shule yangu inapokea zaidi ya sh. milioni 30 kwa mwezi ikiwamo pia ya chakula maana ni shule ya kulala,” anasema.
Pamoja na shule hiyo kuwa kongwe, imekuwa ikijitahidi kufanya vizuri katika mitihani ya taifa, na mwalimu huyo anataja siri ya mafanikio kuwa ni usimamizi mzuri kuanzia wanafunzi na walimu na kuwapo kwa mahusiano mazuri kati ya walimu, uongozi na wanafunzi.
Anasema kuwa pia shule hiyo imekuwa ikitoa motisha kwa walimu wanoonekana kufanya vizuri, ili kuwawezesha kuwa na moyo na kufikia malengo waliyojiwekea ambayo huchangia asilimia kubwa ya watoto kushinda.
“Vifaa vya kufundishia sio adimu sana, lakini vingine upatikanaji wake unahitajika ubunifu wa walimu husika sio lazima kutumia vifaa vya kununua madukani,” anasema.
Anasema kuwa pia wanafunzi wanapata muda wa kujisomea, kila siku baada ya chakula cha jioni kuanzia saa mbili usiku wanakuwa darasani wakijisomea isipokuwa siku ya Jumamosi, na kuwa hujitahidi kuwasimamia.
Kuhusu walimu anasema idadi iliyopo inaendana na idadi inayotakiwa lakini bado wana changamoto ya walimu wa masomo ya sayansi.
“Tuna walimu 52wanatosha kabisa, lakini changamoto iliyopo ni ya uhaba wa walimu wa sayansi tunahitaji walimu wanne ili kukidhi mahitaji kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita” anasema.
Katika mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana, wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 182, wanafunzi 14 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 27 daraja la pili, wanafunzi 44 daraja la tatu, daraja la nne wanafunzi 80, huku waliopata ziro wakiwa ni wanafunzi 17.
Shule ya sekondari Rugambwa ina wanafunzi 815 wakiwamo 42 wenye ulemavu wa aina mbalimbali.










