Panama Papers na miaka minne uchunguzi mabilioni ya Uswisi

13Apr 2016
Restuta James
Nipashe
Panama Papers na miaka minne uchunguzi mabilioni ya Uswisi

WAKATI dhoruba ya kashfa ya kile kinachoitwa ‘Panama Papers’ ikiendelea kuutikisa ulimwengu, Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini, Harold Sungusia, anasema ‘ni ufisadi uliopindukia’ unaolelewa na watawala wa sasa.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju.

Miongoni mwa vigogo waliotikishwa na kashfa ya Panama Papers ni Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye amekiri kunufaika na kampuni ya baba yake iliyosajiliwa nchini Panama. Tayari wananchi nchini humo wameandamana wakisema hawamwamini tena na wanashinikiza ajiuzulu.

Nchini Argentina, waendesha mashitaka wamefungua kesi dhidi ya rais wa taifa hilo Mauricio Marcri.

Viongozi kadhaa wa mataifa, watu maarufu na wanamichezo wamehusishwa na tuhumua zilizo katika uchunguzi wa vyombo vya habari za nyaraka milioni 11.5 zilizovuja kutoka katika kampuni ya inaoyotoa ushauri wa kisheria ya Mossac Fonseca.

Kwa ujumla, Panama Papers imeanika mipango ya kifedha ya kisiri ya matajiri na watu wenye ushawishi.

Kashfa ya Panama imemwangusha waziri mkuu wa Iceland na kulazimisha wanasiasa wengine wakubwa kuingia katika hatua kali za kujihami akiwemo Rais wa Urusi, Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping na sasa rais Macri wa Argentina, kiongozi wa mrengo wa kulia anaechipukia katika eneo la Amerika Kusini.
Wakati vigogo wa dunia wakihaha na Panama, hali ikoje hapa nchini.

Mwanasheria katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Sungusia anasema kashfa hiyo ni ndogo na waandishi wa habari wanapaswa kufanya kazi zaidi katika kufichua ufisadi.

“Kuna mambo mengi sana yamefichika na hayajafichika kwa bahati mbaya, yamefichwa na watawala kwa maslahi yao,” anasema Sungusia.

Sungusia anasema ili kufichua kashfa zaidi, kunatakiwa kuundwa kwa mfumo mzuri zaidi wa haki ya kupata habari.
Pia, anasema watoa habari nao wanatakiwa kulindwa ili wanapoibua kashfa zinazowahusu vigogo wa nchi na dunia, waendelee kuishi salama.

“Tukiwa na mfumo mzuri wa haki ya kupata habari na ulinzi kwa watoa taarifa, Panama Papers zitaibuka sana,” anasema.

Anasema kinyume cha hapo, watu wataogopa kutoa taarifa akieleza kuwa hata wezi wa kuku wanapokamatwa huelezwa nani amewataja.

“Huu ufisadi uliopindukia unalelewa na watawala…nina uhakika yapo madudu makubwa zaidi ya Panama au mabilioni ya Uswisi,” anasema.

Anatoa mfano kuwa, hatua ya serikali kuzia vikao vya Bunge visionyeshwe moja kwa moja ni mkakati wa kuficha ‘madudu’ yanayoibuliwa na wabunge.

KASHFA YA MABILIONI YA USWISI
Kuhusu kashfa ya Watanzania 99 kuficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, Sungusia anasema kinachoweza kusaidia vita ya ufisadi hapa nchini ni Katiba nzuri inayowabana watawala na watu wenye ushawishi wanaojihusisha na rushwa.

Anasema: “Tuna mfumo uliooza, lakini bila Katiba madhubuti hata hii kazi ya kutumbua majipu inayofanywa na Rais John Magufuli, inaweza isifanikiwe sana.”

Anasema kazi ya kuwawajibisha wala rushwa na mafisadi nchini bila Katiba madhubuti inaweza kuishia kwa Rais Magufuli na kwamba akiondoka madarakani, rais ajaye hatakuwa na ulazima wa kuwajibisha wabadhirifu.

Kashfa ya Panama Papers inakuja miaka minne baada ya serikali kuchunguza taarifa za Watanzania waliotajwa kumiliki akaunti za mabilioni nje ya nchi.

Naye, Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo cha Mtakatifu Augustine, Prof. Mwesiga Baregu, anapendekeza kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu rushwa na ufisadi ambao utatoa njia muafaka wa kukabiliana na tatizo hilo.

“Sina matumaini ya kupata suluhisho la ufisadi kwenye awamu hii…sijaelewa majipu ni nini hasa. Je, ni rushwa, ubadhirifu, uzembe kazini au watumishi hewa? Imekuwa kama ni msemo tu sasa. Majipu haitoi mwelekeo wowote kuhusu ufisadi au rushwa,” anasema.

“Najiuliza hivi huyu (Rais Magufuli), anataka kusimamia mabadiliko ya msingi au juu juu. Kama yuko serious, aanzie kwenye kashfa za ununuzi wa rada, Epa, Richmond na aunde mfumo mahsusi wa kushughulikia haya madudu,” anasema.

Katikati ya uchunguzi ulionza mwaka 2012, mwaka jana, Watanzania 99 walitajwa kuficha fedha katika benki za Uswisi, kupitia ripoti ya mtandao wa Swiss Leaks chini ya Waandishi wa Habari za Uchunguzi wa Kimataifa (ICIJ), waliofichua uwapo wa akaunti za siri nchini humo zenye mabilioni ya fedha.

Taarifa ya Swiss Leaks ya mwaka jana ilionyesha kuwa miongoni mwa Watanzania hao ni wanasisa na maofisa wa juu wa serikali, ambao walitajwa kuwa na akaunti za siri zenye Dola za Marekani milioni 114, ambazo ni sawa na Sh. bilioni 199.6 wakati huo.

Msingi wa ripoti hiyo ulitokana na aliyekuwa mfanyakazi wa benki ya kimataifa HSBC, Hervé Falciani, kuvujisha siri za akaunti za wateja baada ya kuacha kazi; na mwaka 2008, alivujisha siri za akaunti za siri za baadhi ya watumishi wa umma na wanasiasa wa Ufaransa ambayo mamlaka za kodi nchini humo ilifanya uchunguzi kuthibitisha.

HSBC ni benki kubwa ya biashara duniani ambayo ilianzishwa mwaka 1836 na kwa mujibu wa Swiss Leaks, matokeo ya uchunguzi huo yalitokana na aina tatu za taarifa ndani ya benki kwa vipindi tofauti; Mosi ni taarifa za wateja na uhusiano wao na akaunti za benki nchini Uswisi kwa kipindi cha kuanzia mwaka 1988 hadi 2007.

Pili, ni picha kamili ya kiasi cha juu cha fedha kilichokuwapo kwenye akaunti ya mteja katika kipindi cha mwaka 2006 na 2007 na tatu, ni mawasiliano kati ya mteja husika na wafanyakazi wa benki katika kipindi cha mwaka 2005.

Ripoti hiyo ya Swiss Leaks ilibainisha kuwa taarifa za kiuchunguzi kutoka kwenye benki nchini Uswis zinaonyesha kuwa akaunti hizo zinahusishwa na baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa na watumishi wa umma ambao wamejipatia utajiri wa siri unaotokana na kuanzishwa kwa kampuni hewa.

Hata hivyo, mapema mwaka jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alikaririwa akieleza kuwa uchunguzi ulikuwa umekamilika na kwamba wachunguzi walikuwa wanaandika ripoti ambayo hadi sasa haijawahi kuwekwa wazi.

ZITTO
Tuhuma za kuwapo kwa vigogo wenye akaunti za siri nchini Uswisi ziliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), bungeni mwishoni mwa mwaka 2012.

Agosti 2012, Zitto aliwahi kusema kuwa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswisi na kuchapishwa na magazeti mbalimbali ya hapa nchini mwezi Juni, 2012, ilionyesha kuwa viongozi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara wakubwa ndiyo wametoroshea fedha zao katika benki za Uswis.

Alisema habari zaidi zinaeleza kwamba mabilioni haya yanatokana na ‘deals’ zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kadhaa kwenye sekta za Nishati na Madini. Aliongeza kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa na kampuni za utafutaji wa Mafuta na Gesi katika Pwani ya mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Mwaka juzi, Zitto alikaririwa akisema kuwa wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi na kwamba, wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa.

Zitto alisema vilevile kuwa Tanzania imepoteza jumla ya dola za Marekani bilioni 1.25 kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hiyo ya kuwapo kwa Watanzania wanaoficha fedha zao Uswisi.

Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka 2012 ambayo ilikuwa inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati huo, Jaji Frederick Werema.

Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndulu.

Wakati uchunguzi wa Tanzania ukishindwa kuzaa matunda kwa miaka minne sasa, wenzao wa Ulaya walishafanya uchunguzi na kuwawajibisha watu wao waliobainika kukiuka sheria katika kufungua akaunti za siri.

JE, FEDHA HIZO ZINAWEZA KUPATIKANA?
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaeleza kuwa uwezekano wa Tanzania kupata fedha hizo ni mdogo kutokana na kwamba ni za muda mrefu za wateja wa mwaka 2006 hadi 2007 hivyo inawezekana hata akaunti hizo zikawa zimefungwa. Pia, HSBC yenyewe imeshajitenga na maelfu ya wateja wake.