Masuala mengi yamesikika katika matukio yaliyohusu bomoa bomoa, hasa jijini Dar es Salaam; agizo alilopewa Jaji Mkuu na mahakama anazozisimamia juu ya dhana ya haki; na mtindo wa Rais na wa mawaziri wa kuaachisha kazi hadharani kama vile hakuna taasisi na mifumo yaliyobuniwa kusimamia masuala ya kazi.
Wako watumishi wengine wa serikali ambao (kwa sababu wanazozifahamu wenyewe), wanajiingiza mkumbo mkumbo katika utamaduni huu. Hivi karibuni zimeenea taarifa, ikiwamo katika idhaa za kitaifa, kutoka Pemba kuwa polisi itawafungia wafanyabiashara wanaokataa kutoa huduma kwa wengine na kuwafungulia mashitaka.
Polisi wameelezea hatua hii kama mwendelezo wa juhudi zao za kulinda haki za watu, hasa wale ambao walioahidiwa kulindwa na serikali na chama kwa kushiriki uchaguzi wa marudio.
Bila shaka kazi moja kuu ya Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Lakini kuingilia suala la biashara na uendeshaji wa biashara ndio kazi ya polisi? Katika nchi inayojitapa kushajiisha biashara, tena huru, inayumkinika kuwa biashara sasa inasimamiwa na virungu?
Ingawa si jambo jema kuwabagua wananchi kwa itikadi zao na kuwaadhibu kwa maamuzi wanaofanya- iwe ya kisiasa au kimaisha, lakini pia kamwe si jambo halali kwa taasisi isiyohusika kimamlaka kuingilia taasisi, chombo au mhimili mwingine.
Ziko taasisi zimeundwa mahsusi kusimamia biashara na mwenendo wake. Sasa kwa nini jeshi la polisi lijiingize katika masuala kati ya muuzaji na mteja? Kama ni hivyo basi wangeanza pia na mahoteli haya makubwa ya kifahari. Mbona kwa muda mrefu wamekuwa wakiwanyima wenyeji wa maeneo husika haki hata ya kupita katika maeneo ya wazi kwa sababu wana hoteli zao?
Sote tunakumbuka namna suala hili lilizua kasheshe kwenye mashamba ya Unguja miaka ya nyuma pale wananchi wa maeneo husika walipokuwa wanazuiliwa na walinzi wa hoteli zilojengwa kama mpango wa kukuza utalii visiwani Zanzibar kulima mwani wao katika fukwe za bahari ambamo walikuwa wakilima mwani huo vizazi kwa vizazi.
Hili tatizo limehama shamba na sasa kuhamia mjini ambapo hoteli kubwa nyingi zimeshamiri. Wakazi wa Mji Mkongwe, wengi wakiwa wamezaliwa na kukulia maeneo hayo, wanalalamika kuhusu kuvurumishwa na virungu vya walinzi wa hoteli kubwa wanapokuwa wanapunga upepo katika maeneo ambayo enzi na enzi ni za kijamii. Moja ya sehemu hizi ni mbele ya iliyokuwa eneo la wazi kati ya hoteli za Tembo na ya Park Hyatt.
Kadhalika katika sehemu nyingi za burudani na hata za chakula nchini kuna matangazo yanawekwa kuwa wenye biashara au uongozi unabaki na uhuru wa kuzuia mtu kuingia katika sehemu yao. Je, na hawa pia wanaguswa na hili tangazo au ndio polisi wamo katika kuendeleza ushabiki wa kisiasa?
Makatazo haya ya polisi pia tutayaingiza maofisini ambapo wakazi wengi wa Zanzibar wanadai watu wanapewa vyeo kwa mujibu wa ‘uwenzetu’? Enzi za ‘rais komando’ ilikuwa kama sera katika taasisi zote za serikali watu kuachishwa kazi kama walishukiwa kuwa wapinzani au ni watu ambao wana mwelekeo wa ‘upinzani’. Kuna mwenzangu mmoja aliwahi kunihadithia kuwa baba yake alifukuzwa kazi kwa vile jina lake lilikua Hamad na akidhaniwa kuwa na uhusiano na Maalim!
Wakati wengine wakiachishwa kazi wengine wakipewa kazi si kwa mujibu wa sifa zao, lakini kwa mujibu wa kuwa ‘mwenzetu au si mwenzetu’. Na wenzangu Unguja wananiambia kuwa kwa sasa kuwa mwenzetu si kuwa mwana chama tu, lakini pia kutoka eneo fulani.
Kama haya yote ni kweli je, hili mbona halisemwi na pia kujumuisha miongoni mwa mambo ya kushitakiwa maana liliwanyima watu haki zao za ajira na inaendelea kuwanyima raia wenye sifa fursa za ajira au masomo kwa sababu tu ya mwelekeo wao kiitikadi?
Siku chache baada ya tangazo hilo la awali akasikika msemaji mmoja wa polisi, tena mwenye cheo kikubwa, kutangaza kukamatwa kwa wahusika wa matukio ya mabomu yaliyoambatana na kipindi cha Uchaguzi wa marudio Zanzibar. Polisi huyo akawataja kwa majina hao waliokamatwa akidai kwa uhakika kuwa ndio wao waliohusika.
Katiba ya Zanzibar, Ibara za 12 na 14, zinasema mtu anapokamatwa na vyombo vya dola ni mtuhumiwa mpaka hapo mahakama au chombo cha haki kitakampata au kuona hana hatia. Iweje leo mtu kakamatwa na hajafikishwa popote atoke kwenye utuhumiwa kuwa mhalifu mwenye hatia kutokana na hukumu iliyotolewa nyuma ya deski la kamanda mmoja wa polisi?
Watu na hususan watumishi kuingilia mamlaka au kazi ambazo si zao ni udhaifu mkubwa hapa kwetu. Mwisho wa siku huwa wanaendeleza ushabiki na siasa za kishabiki badala kusimamia na kutii sheria.










