Maguli ajipoteza kiajabu

03Apr 2016
Lasteck Alfred
Lete Raha
Maguli ajipoteza kiajabu

UENDA ikawa mwisho wa straika Elias Maguli kuichezea Simba huku mwenendo wake ukionekana kutoivutia klabu yoyote ya juu. Straika huyo ameingia kwenye mgogoro mkubwa na uongozi wa klabu na benchi la ufundi kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

straika Elias Maguli.

Klabu ya Stand United inajadili hatua za kumchukulia straika huyo ikiwemo ile ya kumsimamisha huku wakiwa tayari wamesema kuwa hawatamuongezea mkataba baada ya msimu kumalizika.

Straika huyo amekuwa akimtuhumu kocha wake, Patrick Liewig kuwa hampangii kwenye mechi nyingi hivyo amekuwa akinyimwa fursa hiyo huku akitumia nena maarufu mtaani la ‘ananibania.’

Lete Raha iliwahi kupiga kambi ya wiki mbili ikifuatilia kwa undani suala la mgogoro kati ya straika huyo na kocha lakini sasa gazeti hili limefuatilia mgogoro kati ya mchezaji huyo na uongozi wa juu wa klabu hiyo inayodhaminiwa na kampinu ya Acacia.

Lete Raha imegundua kuwa Maguli amekuwa akitoa taarifa za kupotosha baada ya kubaini kuwa mchezaji huyo amekuwa akilalamika kuwa hapangwi ilhali amecheza mechi sita kati ya nane ambazo amekuwa analalamika hapangwi.

Imegundulika kuwa kocha Liewig amekuwa akimpa nafasi kwenye kila mchezo kwa kumuanzisha au kumwingiza akitokea benchi.

Kwenye mechi nane za klabu hiyo , amekosa mbili ambazo ni dhidi ya Azam na Majimaji ambapo ripoti ya kocha inaonesha kuwa hakuwa kwenye kikosi cha dhidi ya Majimaji kutokana na kocha kuamua kujaribu wachezaji wengine, Pia alikosa mechi ya Azam kutokana na kile alichodai kuwa anaugua Malaria.

Kingine ambacho kinadaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu ni jinsi mchezaji huyo ambavyo amekuwa akizungumza na vyombo vya habari akielezea mambo ambayo hana mamlaka ya kuyazungumzia.

Vyombo vya habari
Kocha wa Stand United pamoja na uongozi wa timu kwa kauli moja ulipozungumzia suala hilo walisema kuwa mchezaji huyo amekuwa akitoa taarifa za kupotosha kwenye vyombo vya habari na kwamba umekuwa ukiivuruga timu.

Msemaji wa Stand United, Deo Makomba alisema, “ Tumekaa na viongozi wa Stand, tumezungumza na tunapenda kuueleza umma kuwa straika Maguli amekuwa akipotosha kwenye vyombo vya habari kutokana na taarifa ambazo amekuwa akitoa.

“Hatumnyimi mchezaji kuzungumza bali haruhusiwi kuzungumzia mambo yanayohusu uendeshaji wa klabu lakini pia hana mamlaka ya kuamua au kutaka kocha afanye anachokitaka yeye,” alisema.

Kocha Liewig
Kocha huyo alisema kuwa amekuwa akichoshwa na tabia ya Maguli nje na ndani ya uwanja na kwamba hatoweza kupiga hatua kwa muenendo huo.

“Nimempa nafasi kwenye mechi zote alizokuwa mzima wa afya isipokuwa nilimweka kando kwenye michezo miwili kwa lengo la kujaribu mastraika wengine lakini yeye amekuwa akipotosha kwenye vyombo vya habari kwamba ninamweka benchi makusudi.

“Mimi ni kocha profesheno, napenda kuona kila mchezaji akifanikiwa kwa njia iliyo sahihi. Nataka kuona kila mchezaji anaonesha nidhamu nzuri japo kwa maendeleo yake binafsi na timu.

“Sioni haja tena ya kuwa na Maguli kama amekuwa an nidhamu mbaya ya kudanga kwenye vyombo vya habari, kuwatukana viongozi wa timu lakini pia kumtukana msaidizi wangu (Bilali Athumani).

“Hakuna kocha anayeweza kuvumilia ujinga wa aina hiyo, tena akumbuke mimi na bilali na timu yenye viongozi makini ndiyo waliomsaidia kurudisha makali yake baada ya kuchemka Simba.”

“Nataka afahamu kuwa Stand kuna wachezaji wengi wenye uwezo kama wake na pengine ambao wanaweza kuwa na uwezo zaidi yake sema hawakupata nafasi kwasababu hakucheza,” alisema kocha huyo ambaye tayari alishafanya mazungumzo na kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars, Boniface Mkwasa akimuomba amsaidie kumshauri Maguli kuwa na nidhamu njema.

Kocha huyo alienda mbali na kusema kuwa hana uadui na Maguli wala mchezaji yoyote bali amekuwa akitamani kila mmoja afike mbali. “ Hatuna uadui na Maguli, Maguli ndiyo anayecheza dhidi ya timu, dhidi ya wenzake, viongozi na hata makocha.”

ETI HATAKI KUFUNGA
Kocha huyo alisema kuwa amekuwa akishangazwa na nidhamu ya straika huyo pale anapokuwa akicheza kwa kuwa amekuwa akiacha kufunga mabao ya wazi.

“Nimesoma saikolojia, Maguli amekuwa akicheza na kupata nafasi nyingi lakini amekuwa akiwadakisha magolikipa mpira. Kiukweli nimeona kama anawakosea wenzake kwani nyakati nyingine anapopata nafasi anapiga nje lakini kwa hali nilivyokuwa nikiiona anafanya makusudi. Kiukweli sifurahishwi na mwenendo wake,” alisema kuwa si macho yake pekee yaliona hivyo bali hata benchi lote la ufundi liliona hivyo.

Kocha Mkwasa
Kuna nafasi kubwa ya Maguli kukatwa kwenye kikosi cha Stars kwa kile kinachodaiwa kuwa staa huyo ananidhamu mbovu kwenye klabu yake na hii ni baada ya kikao cha hivi karibuni kati ya kocha Mkwasa na kocha Liewig kwenye ofisi ya kocha huyo iliyopo Karume jijini Dar es Salaam.

Mkwasa alisema, “Tulikutana Karume na Liewig kwa lengo la kutatua mzozo kati yake na straika Maguli lakini straika huyo hakutokea kwasababu alikuwa na kambini Stars. Lakini baada ya kupata taarifa ya kocha wake, tulikutana na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa lengo la kumshauri lakini Maguli alikataa kila tuhuma ambayo kocha wake alimpa.

“Tulionelea kuwa kama uongozi na kocha wa Stand pamoja na mchezaji angekuwepo basi tungeweza kusuluhisha lakini hatujafanikiwa mpaka sasa zaidi tumemshauri Maguli kuzingatia nidhamu.

“Nataka atambue kuwa, Stars haitakuwa na mchezaji asiyekuwa na nidhamu. Nidhamu ni kitu muhimu na ndicho kinachotakiwa kuonesha kwa wachezaji wengine. Ningependa kuona Maguli akicheza na kama kweli ni mtovu wa nidhamu basi ajue kuwa hakuna mchezaji aliye juu ya klabu au hata wachezaji wenzake,”alisema.

Kocha Kerr anasemaje
Aliyewahi kuwa kocha wa Simba, Muingereza Dylan Kerr amesema kuwa nidhamu ya Maguli Elias ilibadilika pale alipomweka nje ya kikosi ambacho kilicheza mechi siku ya Simba ‘Simba Day’ Baada ya kumweka nje ya kikosi hiko mchezaji huyo alisusa na ndipo alipojiondoa kwenye klabu hiyo na kutimkia Stand United.

“Nilisingiziwa kuwa mimi ndiye niliyesababisha Maguli kuondoka Simba lakini sikuhusika, nilimshauri mara kadhaa kuwa kuwekwa benchi au kutokuwa kwenye kikosi si mwisho lakini niliona kana kwamba alikuwa hataki kuendelea kuwa Simba, “alisema kocha huyo.

Uongozi kutoa tamko
Kupitia kwa msemaji wa Stand, Deo Makomba, uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa una mpango wa kumchukulia hatua mchezaji huyo baada ya kupitia ripoti mbalimbali za kinidhamu zinazomuhusu mchezaji huyo.

Makomba alisema, “Tunampenda Maguli na tungependa arekebishe nidhamu yake, aache matusi ya nguoni, aache kuwadhalilisha walimu wake na afanye kazi yake. Jumatatu uongozi utakapokaa utaamua nini cha kufanya,”alisema.

MECHI ZA MWISHO ZA STAND UNITED AMBAZO MAGULI ALICHEZA LAKINI ALIDAHI KOCHA HAKUPANGI
v Mtibwa Sugar 1 - 0 (alicheza dakika zote)
v African Sports 0 - 0 (alicheza dakika zote)
v Simba 2 - 1 (alicheza dakika 45)
v JKT Ruvu 1 - 1 (alicheza dakika zote)
v Prisons 1 - 0 (alicheza dakika zote)
v Mbeya City 2 - 0 (alicheza dakika zote)
v Maji Maji 1 - 0 (aliwekwa benchi)
v Azam 1 - 0 (alikuwa anaumwa Malaria)
v Ndanda 1 - 1 (Hakupangwa hata benchi)