Kuchoma vituo, kupiga wauguzi si suluhisho la tatizo

03Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Kuchoma vituo, kupiga wauguzi si suluhisho la tatizo

SIKU za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya wananchi kuamua kujichukulia sheria mkononi pale wanapotaka suluhu la tatizo lao haraka.

Tabia hii imeibuka sehemu mbalimbali nchini hali inayosababisha, si serikali kupata hasara, bali hata wananchi wenyewe.
Kwa mfano kuna matukio ya wananchi kuchoma vituo vya polisi kwa sababu ya kushinikiza polisi kuwatoa watuhumiwa waliowekwa mahabusu kwa sababu mbalimbali za kihalifu.

Shinikizo hili la wananchi linatokana na madai ya baadhi ya polisi kuwalinda watuhumiwa hao na wanapoachiwa huendeleza vitendo vyao viovu.

Pale inapotokea polisi wanatekeleza wajibu wao wa kuwalinda watuhumiwa wasidhuriwe, wananchi hupandwa na hasira na huamua kujichukulia sheria mkononi kwa kuchoma kituo na kuteketeza mali na hata kuwajeruhi askari hao.

Ingawa kuna tuhuma kwamba baadhi ya polisi huwalinda wahalifu, lakini kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi huleta madhara makubwa kwa jamii.

Vitendo hivyo vya kuchoma vituo vya polisi, vimesababisha maeneo yaliyotokea matukio hayo kukosa vituo na polisi, hali inayochangia uhalifu kuongezeka pale linapotokea tatizo la dharura kwa wananchi kukosa msaada wa haraka.

Baadhi ya vituo hivyo vimejengwa kwa nguvu za wananchi wenyewe na matokeo yake, huchukua muda mrefu kujenga vingine huku matendo ya uhalifu yakiendelea kutawala.

Hali hii husababisha hata watu wabaya kutumia mwanya huo kuendeleza vitendo viovu kwa kutambua kuwa wananchi hawana pa kukimbilia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kulitolewa taarifa za kusikitisha kutoka mkoani Mtwara, zikieleza kuwa ndugu wa mgonjwa mmoja aliyepelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu, walimshambulia daktari kwa kumpiga na kumdhalilisha kwa kumvua nguo.

Mmoja wa wauguzi aliyekuwa akitoa malalamiko ya kudhalilishwa kwa mwenzao, alisema kama wananchi wataendelea kuachwa wakiendeleza vitendo hivyo ni wazi watashindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Muuguzi huyo alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakichanganya mihemko ya kisiasa sehemu za kazi na kusababisha uvunjifu wa amani.

Suala hilo limepokelewa kwa hisia tofauti na wananchi, wengine wakisema lazima kuna sababu ya watu hao kuamua kuchukua hatua hiyo, huku wengine wakipinga na kuwalaumu waliofanya hivyo.

Kwa wanaounga mkono hatua hiyo, walidai kuwa, baadhi ya wauguzi wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa hatua inayowalazimu ndugu kufikia uamuzi huo.

Hata hivyo, wanaopinga, wanasema wauguzi wanafanyakazi katika mazingira magumu, hivyo wananchi wanapaswa pia kuwa wavumilivu wanapokwenda kupata huduma.

Ukijaribu kutafakari, vitendo hivi vya kujichukulia sheria mkononi havijengi na wala si suluhisho la tatizo. Kama inaonekana mtu hatimizi wajibu wake, sehemu za kumshtaki zipo ili achukuliwe hatua stahiki.

Vitendo vya kuwavamia wauguzi na hatimaye kuwadhalilishwa mbele ya kadamnasi, havipendezi na vinasababisha chuki.
Lazima tuangalie kuwa daktari huyo ana familia na pengine ana watoto, halafu wanasikia baba yake amefanyiwa kitendo hicho. Kwanza unawaathiri watoto hao kisaikolojia na hata familia yake kwa ujumla.

Msemaji wa Chama cha Madaktari, akiongea kwa masikitiko, anasema haivumiliki kuona daktari mwenzao akidhalilishwa kiasi hicho mpaka kufikia hatua ya kuvuliwa nguo, halafu waliofanya vitendo hivyo wakiachwa bila kuchukuliwa hatua.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amekemea kitendo hicho, na kuamuru wote waliohusika na tukio hilo la kumdhalilisha daktari wakamatwe na kuchukuliwa hatua.

Kwa taarifa zilizopatikana tayari watu wawili wanashikiliwa kwa kuhusika na tukio hilo na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

Pamoja na matatizo yanayojitokeza wakati wananchi wakienda kupata huduma hospitali, lakini lazima tuangalie mzigo unaowakabili. Tumeshasikia ripoti mbalimbali zikitolewa za upungufu wa wauguzi ambapo katika baadhi ya maeneo, daktari mmoja hulazimika kuhudumia zaidi ya wagonjwa 100 kwa siku.

Wakati madaktari walipofanya mgomo wa kutoa huduma kwa kudai stahiki zao, nchi ilitikisika na wagonjwa wengi walipoteza maisha kwa kukosa matibabu.

Hivyo, ni jukumu letu wananchi kabla ya kufikia uamuzi, tujitafakari kwanza. Wahenga walisema hasira ni hasara. Unapofanya jambo lolote wakati ukiwa na hasira matokeo yake ni hasara.

Mara nyingi watu wanaofanya maamuzi kwa sababu ya hasira huishia mahali pabaya na kujikuta wakiharibu mipango yao yote waliyokusudia, huku wakiacha familia zikiteseka.
bbandawe@hotmail.com; Simu 0774 466571