Babu Tale ajitosa kumuokoa Chid Benz

24Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar
Nipashe
Babu Tale ajitosa kumuokoa Chid Benz

BABU Tale, Meneja Diamond Platnumz, amemchukua msanii Chid Benz na kumpeleka kituo cha Life and Hope Rehabilitation kilichopo mjini Bagamoyo, Pwani ili asaidiwe kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

Babu Tale, Chidi Benz na Kalapina.

Babu Tale amechukua uamuzi huo baada ya msanii huyo kuomba msaada kutokana na kushindwa kukabiliana na matatizo ya kiafya yanayomsumbua kwa muda mrefu sasa.

Katika mahojiano na moja ya vituo vya redio vya jiji la Dar es Salaam juzi, Babu Tale, alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kusikia kilio cha msanii huyo na kwamba jambo la kwanza lililkuwa ni kumpeleka hospitali kumpima afya.

"Baada ya kumpima, aligundulika kuwa hajaathirika na ugonjwa wowote bali ni matumizi ya dawa za kulevya na amekubali kupelekwa Bagamoyo ili kupata huduma itakayomsaidia kuachana na dawa hizo," alisema Babu Tale.

Mdau huyo mkubwa katika muziki wa Tanzania,
aliwataka wasanii nchini kuachana na matumizi ya dawa hizo kulinda afya zao.