Alisema Mawaziri waliorejesha fomu hizo ni 15 kati ya 19, yaani wanne hawajarejesha. Aidha, Naibu Waziri waliorejesha fomu za tamko ni 13 na wasiorejesha walikuwa ni watatu.
Akasema Rais Magufuli, Makamu wa Rais, na Waziri Mkuu wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria hiyo.
Waziri mkuu siyo tu alisaini kiapo bali amekitundika ukutani ofisini kwake ili kila mmoja akione.
Jaji Kaganda aliyasema haya wakati wa semina iliyofanyika Ikulu tarehe 25 Februari kwa ajili ya viongozi hao kuhusu sheria ya maadili.
Tukaambiwa semina hiyo ilifadhiliwa na Marekani. Katika taarifa iliyopatikana kwenye vyoombo vya habari nikaona wawakilishi wa nchi hiyo wakiwa wamehudhuria, wakiwa kama viranja
Ndipo nikajiuliza, iweje katika awamu hii ya tano tuombe msaada wa Marekani hata tunapotaka kuwafunza Mawaziri wetu maadili? Sidhani Ikulu ilitoza gharama ya ukumbi wake.
Labda ni gharama za makabrasha na soda, na labda posho nono za kikao kama ilivyo kawaida ya awamu zilizopita. Ni kwa hilo tu tuombe msaada kutoka nje? Magufuli ameidhinisha hilo?
Sasa Jaji Kaganda akamkabidhi Waziri Mkuu majina ya viongozi wasiowasilisha fomu kwa hatua zaidi. Mara moja wakuu hao wakapewa muda wa masaa machache wawe wamewasilisha au watakuwa wamejifukuzisha kazi. Lo masalala! Mbona waliwasilisha haraka haraka.
Baya zaidi, jaji huyo akasikitika kuwa viwango vya maadili miongoni mwa viongozi wa umma vinazidi kuporomoka. Akitoa mfano, alisema kuna mawaziri ambao wanadiriki hata kuwaagiza makatibu wakuu wao kuidhinisha fedha za matumizi binafsi kwa ajili ya mawaziri hao.
Wakiambiwa utaratibu hauruhusu, wanajibu “mimi sijui hilo, wewe si katibu mkuu, fanya uwezalo.” Huu ni mfano mdogo wa jinsi maadili yalivyomomonyoka miongoni mwa vigogo
Ndipo inabidi tujiulize. Sheria hii ya maadili imepitishwa tangu 1995. Tumekuwa tukijisifu (pamoja na wafadhili kutusifu) kuwa tuna sheria ya maadili na secretariati yake, wakati maadili miongoni mwa viongozi yanaporomoka. Je mamlaka husika zimechukua hatua gani?
Wanaotafuna fedha za umma si Mawaziri tu bali pia wamo Maofisa katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya kitaifa hadi wilayani.
Majipu lukuki yameachiliwa yaote kila mahali na hakuna hatua zilizochukuliwa. Ukitaka kujua ukweli huu angalia tu ripoti za kila mwaka za mdhibiti na mkaguzi mkuu (CAG) zinazowasilishwa bungeni kila mwaka na kisha kutupwa kapuni. Hii ni dharau
Ndiyo maana tatizo hili la viongozi kutojaza fomu halijaanza leo wala jana. Limekuwepo siku zote, kwani viongozi wengi wamekuwa wakilichukulia kama mzaha, wengine hata kulipuuza.
Kwa mfano, mwishoni mwa mwaka 2010 tuliambiwa na sekretariat kuwa asilimia 56 ya viongozi walikuwa hawajawasilisha fomu zao kama walivyotakiwa kila mwisho wa mwaka.
Jaji Kaganda alisema jumla ya viongozi 8,410 walitakiwa wawasilishe fomu lakini ni 4,788 tu walifanya hivyo ilipofika mwisho wa 2010. Kwa mujibu wa sheria wasiowasilisha walitakiwa waonywe au hata waadhibiwe. Je kuna hatua zilizochukuliwa? Ndipo kila mwaka hadithi imekuwa ikijirudia mpaka sasa katika awamu hii ya tano mawaziri nao wanatangazwa hadharani
Angalau basi mara hii walitangazwa. Zamani walikuwa hata hawatangazwi. Wananchi hawaambiwi ni kina nani wasiojaza fomu. Na hata hivi majuzi mawaziri walipotangazwa, hatujaambiwa iwapo kuna viongozi wengine waliokacha. Mimi sitashangaa kama wengine wengi walikuwa hawakujaza fomu.
Kwani Kaganda hakuishia kumwambia Majaliwa kuhusu mawaziri wasiowasilisha fomu za maadili, bali alimueleza pia matatizo inapokuja kutekeleza viapo vyao vya maadili .
Alisema uchunguzi wa sekretarieti umebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma wanafanya udanganyifu katika fomu ya tamko la mali kwa kubadili majina ya wamiliki wa mali husika.
Sasa utawezaje kuhakiki fomu za viongozi 15,379 kote nchini wakati tume ya maadili ina watu 200?
Sishangai kama kuna mamia au hata maelfu ya viongozi ambao hawajawasilisha au wanachelewa kuwasilisha fomu. Wengi wao watakuwa pia wanajaza ndivyo sivyo na hakuna anayejali.
Hawa Mawaziri wametajwa kwa sababu ya vyeo vyao, lakini nani atajua iwapo hakimu wa wilaya amedanganya? Kwanza fomu ni siri, hazitangazwi kwa wananchi ili waweze nao kutoa mrejesho. Hayo yote ni majipu au vijipu ambavyo vimerundikana na kugeuka mijipu.
Ndiyo maana nasema kuwapo kwa sheria pekee haitoshi, iwapo mfumo uliozoeleka ni mbovu Kwani ukweli ni kuwa hata wakati wa ukoloni watawala wa Kiingereza walitunga sheria (ordinance) ya kuzuia rushwa tangu mwaka 1958
Halafu mwaka 1995 tukatunga sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Sheria hii iliwagusa maelfu ya watu, wakiwemo wabunge, wanasiasa, maofisa wa serikali kuu, majaji, wakuu wa vyuo, wakuu wa mashirika ya umma, mameya, maofisa wa serikali za mitaa na kadhalika.
Pia mwaka 2001 ilipitishwa sheria iliyoanzisha tume ya haki za binadamu na utawala bora, na mwaka 2007 ikaja sheria ya TAKUKURU
Mnamo Disemba 1994 mawaziri wa Afrika ya mashariki, kati na kusini walikutana mjini Pretoria. Wakaunda kile walichokiita ulingo wa kupambana na rushwa Kama hayo yote hayatoshi, mnamo Agosti 2008 rais wa wakati ule, Jakaya Kikwete aliliambia
Bunge nia yake ya kuwafanya viongozi watangaze mali zao kabla ya uchaguzi wa 2010.
Kwanini Kikwete atangaze kuwa fomu zitajazwa kabla ya uchaguzi wa 2010? Kwa nini wasijaze kama walivyotakiwa chini ya sheria ya mwaka 1995? Inaonekana hakuna aliyejali kujaza fomuhizo.
Ndiyo maana ikawa sehemu ya kampeni. Hata hivyo sina hakika kama ahadi hiyo ilitekelezwa
Badala yake secretariat ya maadili ikaomba msaada kutoka Canada ili kuwafunza maofisa wake jinsi ya kutekeleza sheria, kwa vile viongozi wengi walikuwa wakiipuuza
Kutoka Canada wakaja “wataalamu” wawili kuanzia Januari hadi Novemba 2009. Wakaja na kuondoka mara tatu na wakatumia dola 273,108. Huo ndio mfano wa “msaada” wa kigeni kwa nchi yetu. Leo tena tunaomba Marekani watusaidie kuendesha semina ya maadili kwa mawaziri! Tumekuwa nchi tegemezi kwa kila kitu, hata matangazo ya ukimwi katika redio ni kwa hisani ya Marekani!
Pamoja na kasoro zote hizi, kuna hatua moja muhimu ambayo inaweza ikachukuliwa kuhusu hizi fomu za maadili. Ni kuzifanya ziwe wazi badala ya ‘kuzificha’ katika sekretariat. Kwa vile Rais
Magufuli amejitolea kutumbua majipu ni vizuri akaanza na fomu zake.
Wazo hili limetolewa kuwa Rais Magufuli aanze kwa kutangaza hadharani mali zake ili awe mfano kwa viongozi walio chini yake. Chini ya mfumo wa sasa viongozi wanawasilisha maelezo kwa tume ya maadili ambayo inaweka habari hizo kama siri yake.
Raia anaruhusiwa kuona kwa kibali maalum na baada ya kuona haruhusiwi kumwambia mtu mwingine
Mtindo huu hausaidii uwajibikaji na maadili kwa vile wananchi hawaruhusiwi kujua mali za viongozi wao. Hii haileti maana yoyote wala haina mantiki, kwani kiongozi wa umma ameajiriwa na umma.
Ameomba kazi kwa umma. Hivyo kama vile mgombea uongozi anavyotangaza wasifu wake (CV) ili tumchague, hali kadhalika na utajiri wake (au umasikini wake) hautakiwi uwe siri yake.
0713-562181










