Utatu unaowashikilia walimu na serikali katika anguko la mitihani

15Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Utatu unaowashikilia walimu na serikali katika anguko la mitihani

WIKI tatu ya mwezi Februari mwaka huu, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), lilitangaza matokeo ya mtihani wa wanafunzi wa kidato cha nne kwa iliyofanyika mwezi Novemba mwaka jana.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Charles Msonde (kushoto), akitangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha sita.

Takwimu zinaonyesha kati ya watahiniwa takriban 433,000 waliofanya mtihani huo, ni watahiniwa 89,929 ambao ni sawa na asilimia 25 tu ndio waliofaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu, wakati wanafunzi 343,071 sawa na asilimia 75 wana daraja la nne na sifuri.

Kwa mara nyingine matokeo hayo yamekuwa na ufaulu usioridhisha ukiwa ni mwendelezo wa takriban miaka sita mfululizo sasa.

Nitoe mifano michache katika kuthibitisha hilo. Matokeo ya mwaka 2013 yanaonyesha kuwa, asilimia 64.26 ya watahiniwa 235,227 hawakupata nafasi ya kuingia kidato cha tano.

Mwaka 2012 asilimia 65.5 ya watahiniwa 458,139 walipata daraja sifuri. Asilimia 50 ya wanafunzi 354,042 walipata daraja sifuri mwaka 2010.

Huo ni ufaulu usioridhisha na hasa katika shule zinazomilikiwa na serikali. Ni matokeo yanayoakisi mfumo wa elimu nchini ulivyo. Kwa upande mwingine, yanatoa changamoto kwa wadau wa elimu kuangalia sababu za miaka yote iliyopita, kuna matokeo ya mitihani inayofanywa na vijana katika hali isiyoridhisha.

Ufaulu hafifu wa wanafunzi unaathiri wazazi, wanafunzi, walimu, serikali na wadau wa elimu kwa ujumla. Ni matokeo yanayoashiria kwamba tusipokuwa makini na elimu iliyopo nchini, mbele ya safari kuna hatari.

Kuna uwezekano wa kuwa na kundi kubwa la kizazi cha wachuuzi ambacho hakina ustadi wa kujishughulisha na kunufaika na malighafi, pia rasilimali za uzalishaji nchini.

Ni hatari ya kukosa wataalamu wa fani mbalimbali, pia kukosa watu wenye uwezo wa kutafakari na kuchambua mambo kwa kina kupitia stadi za kisomi, katika kupiga vita ujinga, umasikini na maradhi.

Ni hali inayojenga dira mbaya kwa taasisi ya elimu ya juu kukosa wanafunzi bora wa kuwadahili, ili kutengeneza uzao wa wataalam.

Ili kukabiliana na matokeo hafifu ya mitihani, kuna namna serikali imekuwa ikikabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa kuanzisha sera, miongozo na mipango ya maendeleo, ikigusa elimu na maeneo mengineyo.

Miongoni mwake, Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) wa mwaka 2013, Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi wa mwaka 2002 (PEDP) na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari wa mwaka 2005(SEDP).

Hiyo na mipango mingine mingi, inaongeza idadi ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, pia inalenga kuongeza ufaulu wa watoto shuleni, ina maana kubwa katika maendeleo ya talauma, mtazamo unaohusu hadi ngazi ya vyuo.

KILIO CHA WARAKA KANDAMIZI

Kuna baadhi ya mambo ambayo ni chagizo kwa matokeo hayo. Kuanzia miaka ya 2000, walimu wamekuwa na mwamko wa kujiendeleza kielimu. Mwaka 2009, serikali ilitoa waraka unaoelekeza walimu wanaohitimu mafunzo baada ya kujiendeleza, wasipandishwe vyeo hata kama mwalimu huyo alikuwa amefikia hatua ya kupanda daraja.
Badala yake, mwalimu huyo apewe barua inayotambua kujiendeleza kwake na kubadilishiwa muundo wa utumishi ambao kitaalamu inatambulika kama ‘Recategorization.’

Katika utaratibu huo, mabadiliko na utambuzi huo unafanyika na kisha wanabaki katika katika cheo cha zamani, kabla ya kwenda masomoni kwa kipindi cha miaka mitatu zaidi.

Inaelezwa, huo ni waraka unaowakera zaidi walimu hata wakaubatiza kwa jina “waraka kandamizi”
Ni waraka unaowafanya walimu wawili walioanza kazi pamoja na katika cheo na ngazi moja ya mshahara, ila wanatofautiana kimaslahi baadaye, kwa sababu mwalimu ambaye hakwenda kujiendeleza, anaendelea kupanda daraja wakati aliyejiendeleza anabaki nyuma kimaslahi.

Waraka huo umenigia katika lawama kuwa, unawavunja moyo walimu na unawakwaza vijana kujiendeleza.
Lakini kuna ukweli unaobaki kwamba walimu nchini ni rasilimali muhimu ambayo uwekezaji juu yake hauna mjadala.

Wanataaluma hao wana vilio vingi kama vile kutopewa nauli wakati wa likizo, malimbikizo ya mishahara yao kwa wakati na sasa kuna malalamiko kuwa wengi hawajapata tangu mwaka 2011, jambo ambalo ni kinyume kwa watumishi wa serikalini.

Mazingira yao ya kazi si rafiki. Madarasa yana mlundikano mkubwa wa wanafunzi, kama ilivyo kwa ushuhuda wa jijini Dar es Salaam, katika Shule za Msingi Benako katika Manispaa ya Kinondoni, Kivule - Manispaa ya Ilala na Maji Matitu katika Manispaa ya Temeke.

Je katika mlundikano huo wa wanafunzi, kuna matarajio gani ya kupata matokeo bora katika mitihani yao? Katika mchakato huo huo, msingi wa matokeo bora ya shule za msingi, ndio inayozaa ufanisi katika mitihani ya kidato cha nne, kama ilivyo katika mfano “Huwezi kuwa na nyumba imara kama msingi wake ni matope.’

VIFAA VYA KUJIFUNZA

Vifaa vya kufundishia na kujifunza, ni sababu nyingine inayochangia matokeo hafifu katika mitihani. Shule nyingi za Dar es Salaam zina uhaba wa vitabu vya masomo ya sanaa.

zinaelezwa kuwa na uwiano mzuri wa vitabu vya sayansi na wanafunzi, 1:1 wakati masomo ya sanaa, uwiano wake ni 1:30.

Inaelezwa pamoja na kuwa na vitabu vingi vya sayansi, changamoto inayozikabili shule nyingi ni upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Mwaka 2014, serikali ilihamasisha ujenzi wa maabara na ilifanikiwa katika sehemu nyingi. Zipo zilizokamilika na zingine hazijakamilika na nyingi zilizokamilika bado hazina vifaa vya kutosha.

Walimu wanatumia vyumba vya madarasa kufundisha kwa vitendo. Hakuna maktaba katika shule nyingi, hasa sekondari za kata.

Vitabu vinahifadhiwa kwenye meza za walimu. Ni mazxingira magumu kupata matokeo chanya katika ufundishaji na wanafunzi kujifunza katika mazingira hayo.

Mamlaka za Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi zinazohusika na udhibiti wa ubora wa elimu nchini, inapaswa kuangalia uwezekano wa kuimarisha vituo vya walimu nchini (TRCs).

Walimu wengi katika vipindi vya maisha yao kazini tangu wanapohitimu mafunzo yao vyuoni, huwa hawapati mafunzo kazini za kuwaboresha kwenda na mahitaji ya wakati husika.

Vituo hivyo ni muhimu katika kuwakutanisha walimu, ili wabadilishane stadi na ujuzi wa ufundishaji. Iko bayana kuwa maarifa na ujuzi unabadilika kila wakati.

WANAFUNZI NA UELEWA DUNI

Katika mazingira hayo, mshangao unatoka wapi mwanafunzi anapojiunga na elimu ya sekondari akiwa hajui kusoma na kuandika? Uhalisia wa mitihani uliopo (mfumo wa kuchagua majibu) unamuwezesha mwanafunzi kubahatisha majibu ya swali kuanzia la kwanza hadi la 50 na akafaulu.

Mwanafunzi anayejiunga na elimu ya sekondari kwa kufaulu kupitia mtindo wa kuchagua majibu, asitegemee kufanya vizuri anaopokuwa sekondari.

NINI KIFANYIKE?
Ufunguzi wa njia ni kwamba, tunapotaka kushinda mtihani kesho, tunapaswa kuanza kujipanga sasa. Walimu wanapaswa kuwa na mazingira rafiki ya kuishi, kufundishia na kujifunzia.

Wazazi nao wana nafasi yao, kwani weana wajibu mkubwa wa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wanafunzi na walimu wao. Hiyo inafanyika kupitia usimamizi wa nidhamu, kukutana na kujadili na walimu kuhusu uhalisia uliopo kwa vijana wao.

Pia, dhana ya kuwapatia watoto vifaa na mahitaji muhimu katika masomo na ufuatiliaji wa maenedeleo yao, kupitia kukutana na walimu shuleni.

L Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa mdau wa elimu na anapatikana kwa namba ya simu: (+255) 0658 434493