IBRAHIMU AMANI IBRAHIMU:Mwana Mapinduzi aliyekufa na ushujaa Zanzibar

16Mar 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
IBRAHIMU AMANI IBRAHIMU:Mwana Mapinduzi aliyekufa na ushujaa Zanzibar

MUASISI wa Mapinduzi ya Zanzibar Ibrahim Amani Ibrahim amefariki na kuacha pengo kubwa miongoni mwa wana Mapinduzi wa Zanzibar waliofanikisha Mapinduzi ya Mwaka 1964.

Ibrahim Amani Ibrahim.

Kifo chake kimefanya idadi ya wana Mapinduzi sasa kubaki mmoja akiwa hai ambaye ni Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Ramadhani Haji Faki kati ya wana Mapinduzi 14 wa mstari wa mbele Visiwani humu.

Ibrahim Amani ni mmoja kati wana Mapinduzi aliyeongoza kambi ya siri ya wana Mapinduzi katika msitu wa Chukwani wakati huo na kufanikiwa kuvamia boma la Polisi la Ziwani katika harakati za kufanikisha Mapinduzi wakiwa na silaha za kienyeji Mwaka 1964.

Kabla ya kifo chake kutokea machi 10 mwaka huu baada ya kuugua na kulazwa hospitali ya mnazi Mmoja Zanzibar, Mzee Ibrahim Amani alifanya mahojiano ya mwisho na mwandishi wa makala hii katika kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwa nyumbani kwake huko Nyamanzi nje kidogo ya mji wa Unguja.

Alisema walifanikiwa kufanya Mapinduzi kwa kutumia silaha za kienyeji yakiwemo mapanga, mashoka,mishale na mawe na kufanikiwa kuuondoa utawala wa kisultan chini ya mfalme wa mwisho Jamshed Bin Abdullah Januari 12 Mwaka 1964.

Mzee huyo ambaye ni mmoja kati ya wanasiasa wakongwe wa Zanzibar, anasema kazi ya kupindua haikuwa kama kucheza lelemama, walijitokeza awali na kukubali kushiriki baadhi yao walipokaribia vituo vya polisi vya Mtoni, Ziwani na Malindi ili kuviteka walikimbia makundi kwa makundi.

Anasema kama yalikuwa ni makundi ya watu mia tatu , walijikuta wakibaki 30, wengi walibwaga mapanga, mashoka na kukimbia kama jet wakihofia maisha yao,watoto na wake.

Anakumbuka siku moja kabla ya Mapinduzi walishinda kwenye msitu wa Chukwani kutwa nzima wakila matunda, mikate mikavu na maji , fatiki ya Mapinduzi ilianza majira ya saa 8.01 usiku baada ya Serikali ya kikoloni kufanyiwa hadaa ya kupigwa kwa ngoma , densi na fete mitaani kwenye maeneo ya makaazi ya waswahili (ng’ambo).

“Serikali ya kifalme na askari wa kiingereza walikuwa kama waliopata fununu ya kutokea ghasia au uasi, walifanya doria huku na huko lakini walipoona michezo ya fete ikifanyika, waswahili wakitibwirika kwa kucheza ngoma na madensi, waliioona hakuna lolote na wao kutotilia maanani”alisimulia Mzee Amani wakati wa uhai wake.

Anasema asili ya kuungana kwa Waafrika wa Zanzibar na kuwa kitu kimoja imara kulitokana na mchango wa wanasiasa wawili wa juu ndani ya ASP kutumia hekima, busara na haiba ya ushawishi wao kisiasa na kuiongozi.

Anawataja Mzee Abeid Amani Karume na Sheikh Thabit Kombo Jecha ni watu waliotumia maarifa makubwa kuziweka pamoja jumuiya za Waafrika ili Washiraz wapingane na ukoloni.

ASP walifanikiwa kuwashirikisha wana Mapinduzi wengi wenye asili nje ya Zanzibar ili kuwajumuisha katika kazi hiyo ya siri kuliko waliojiita wazaliwa na wenyeji wa Zanzibar.

Pengine hilo kama lisingefanyika anasema mpango wao ungevuja na wakoloni wangeweza kuwakamata na kuwatia vitanzi vya shingo na kuwa mwisho wa maisha yao.

“Tulipekuana kintelejensia ili kuwachuja na kuwapata watu madhubuti ma haikuwa kuokotaokota kila mtu na kuwatia vibaraka au wenye tabia ya woga, Waafrika waliotoka nje ya Zanzibar mchango wao ni mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi hayo ”.alisimulia katika mahojiano yake tukiwa kijjini kwake Nyamanzi

Anaeleza kuwa ameshiriki hatua zote za kufanikisha Mapinduzi kimawazo, ushauri na kivitendo tokea mwanzo hadi mwisho na mara zote amekuwa bega kwa bega na Mzee Karume katika kuzungumzia hatma ya Zanzibar na utawala uliokuwa chini ya mikono ya wageni walioikalia Zanzibar kwa miaka mingi ni vipi wataondoka.

Vipi ushiriki wa John Okello?.Mzee Ibrahim alisema kuwa Okello alikuwa raia wa Uganda aliyefika Zanzibar na kuanza kuishi Pemba kama fundi Seremala baadae akaja Unguja.

Aliingia katika vuguvugu la harakati za Mapinduzi baada ya ASP kupitia kwa Katibu wake wa mpango wa Mapinduzi Abdallah Said Natepe kumtuma mwanachama mmoja aliyeitwa Said Lumumba azungumze nae, akajua msimamo na ujasiri wake katika kuitetea Afrika na kukataa ukoloni.

Lumumba akarudisha majibu akisema na kuhakikisha Okello ni mtu madhubuti, imara, jasiri na anayetamani wakoloni waondoke Afrika na Zanzibar.

Tuliona tumepata mtaji mpya katika kushamirisha harakati zetu,hata alipokutana na na viongozi wa juu baadae alithibitika kwa vitendo na matamshi yake kuwa ni muumini wa Afrika na anayekataa ukoloni na madhila yake.

ASP iliitumia sauti yake yenye lahja ya kigeni ili kuwatisha tuliowapindua na waliotamani kutupinga,huo ndiyo ushiriki wake lakini kabla ya hapo hakujua lolote kwani siku tarehe 12,Januari ilikuwa ni matokeo ya mchakato wenyewe na kwamba Mapinduzi yalipangwa zamani yatokee na Okello hakuwepo Zanzibar.

Siku ya tukio hilo ASP ilimficha kiongozi wake mkuu Mzee Karume mahali kusikojulikana,vijana jasiri wakaenda mstari wa mbele kukabiliana na maadui waliokuwa wameikalia na kutumia rasilimali za Zanzibar kwa manufaa binafsi na familia zao.

Tulimwambia Mzee Karume siku ya tukio atuachie vijana watupu ,tusije tukakamatwa na kunyongwa pamoja, alipomaliza kuweka mikakati na mipango, alituaga na kututaka tutambue kuwa tumebeba hatma ya nchi yetu na vizazi vijavyo.

Mzee Ibrahim alisema ndipo walipoanza kutawanyika katika makundi na kuvivamia vituo vya polisi wakiwa hawana silaha za moto, hata hivyo kabla ya kufika vituoni vijana wa kiafrika walishambuliwa kwa risasi na kufa, hatukukata tamaa,tulisonga mbele na kuingia bomani hadi kupata silaha za moto.

Hafidhi Suleima Almas alivunja ghala la silaha kwa kutumia gari na kufanikiwa kupata silaha katika kituo cha Mtoni ambacho kabla ya kukikamata kulikuwa na mapigano ya piga ni kupige na hapo kila mmoja aliona kifo kiko mbele yake.

Hata hivyo, anasema na kukumbuka mwezi mmoja kabla ya Mapinduzi walifanya kikao cha mkakati wao na kumuomba Mzee Karume awapatie shilingi 300 za kazi za kimapinduzi ili kununua petrol , zikakosekana, hata alipotakiwa Hassan Nassor Moyo atoe fedha hizo katika mfuko wa ASP alipiga chenga na kutoweka.

Hatimaye fedha hizo tulitoa watu wawili, mimi na Ramadhan Haji Faki, mimi niliuza ardhi yangu , Faki alikuwa na mafao ya kuacha kazi ya polisi katika jeshi la kiingereza lililoulinda ufalme.

Lengo letu lilikuwa ni kuhakikisha Mapinduzi yanafanikiwa kwa kutumia vijana wa ASP ambao walikuwa wamepanga kuviwasha vituo vyote vya mafuta na baadaye nyumba, misitu na magari yateketee ili kukiteketeza kisiwa kizima cha Unguja.

“Tulisema ikiwa Mapinduzi hayatakuwa , hakuna haja ya kubaki ufalme, watu wanaotaabika na ukoloni pia vyama vya ZNP, ZPPP na ASP visiwepo Zanzibar,iwe mwanzo na mwisho ” alisema Mzee huyo ambaye hadi kifo chake anasema hajutii yaliyotokea katika kuyafikia matokeo ya kupindua.

Alisisitiza kwamba ili kukamilisha mpango wa Mapind kulikuwa hakuna tena njia mbadala ya kurudi nyuma kwani tayari njama na hila za Waingereza na Sultan zilielekea kuwakatisha tamaa baada ya kuwa wanapata kura nyingi tokea mwaka 1957, 1961 hadi 1963 na kunyimwa kushika madaraka na utawala wa Zanzibar.
Amamfahamu vipi Moyo katika harakati za Mapinduzi ya Zanzibar?

Namtambua Moyo kama kiongozi wa chama cha wafanyakazi, alikawia sana kujiunga na ASP, hata kuja kwake kulikuwa na masharti, hakujiunga na ASP kwa hiari na ridhaa ya kupigania maslahi ya umma na ukombozi, alikuja baada ya kufanyika mazungumzo na kuwekeana mkataba na ASP.

Moyo alimueleza Mzee Karume yupo tayari kuja ASP ila chama chake cha Wafanyakazi kipewe idadi ya viti sita, akaambiwa atapata kimoja , hata yalipofanyika Mapinduzi kiti hicho akakichukua yeye na kuwa Waziri katika Serikali ya kwanza ya ASP .

“Anayoyafanya sasa siyashangai na siyastaajabu, namjua na yeye ananifahamu sana, mara tatu amewahi kuja hapa kwangu kunishawishi nikubaliane naye, lakini akawa anashindwa kuniingia moja kwa moja, anajua si mtu wa kuyumba na kuyumbishwa”Anaeleza Mzee huyo.

Anaeleza kuwa mara baada ya Mapinduzi watu wengi waliojifanya ni wapinga Mapinduzi na misimamo ya ASP walipelekwa wakachunge ng’ombe mwituni.“Anasema bila ya kufafanua kwa undani na anapoulizwa ananyamaza.

Anasisitiza kuwa watu hao bado wako hadi sasa malishoni wakichunga wanyama , huku wanakatazwa kurudi, acha wachunge na wanaotaka kuchunga wangeweza kuwafuta machungani.

Anawakumbuka wanawake wanne ambapo watatu kati yao majina yao yamemtoka na kulikumbuka jina moja la Khadija Jabir na Biubwa Aboud Nadhif.

“Khadija yule ni mwanamke wa aina yake, mumewe alikuwa askari katika jeshi la kikoloni, hata siku moja hakumwambia mume mpango wa Mapinduzi, hawa wengine wawili nimewasau majina yao, hawakuwa wanawake mchezo mchezo” Anakumbuka Mzee Ibrahim.

Katika maelezo yake anaukumbuka utawala wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Abeid Amani Karume kwamba ulikuwa ni wa mfano na vigumu kupatikana kiongozi anayefanana naye kitabia, uzalendo wake na malengo aliyokuwa nayo.

Anasema umefanyika ukatili mkubwa kuyakatisha maisha ya Mzee Karume na kusema leo Zanzibar ingelikuwa mbali kimaendeleo, kiuchumi na maisha ya watu yangekuwa bora zaidi kuliko yalivyo sasa.

“Mwenzetu mungu alimsaidia , alibahatika kuijua dunia kabla ya Waafrika wengi kutembea ulimwenguni , alijua maana ya neno maendeleo, ndiyo maana aliweza kuyasimamia kwa vitendo , bidii na maarifa akijua kila jambo jema maana yake nini na baya likoje” Anakumbuka Mzee huyo.

Uongozi wake wa miaka minane hauna mfano wake, alipania kuijenga Zazibar, alichukia maonevu, alionya hatari ya kujengeka mataba na alichukia ubaguzi kutoka moyoni mwake.

“Nyie vijana wa sasa hebu sikilizeni hotuba za Mzee Karume kila asubuhi katika sauti ya Zazibar, mimi hutokwa na machozi, hufikiri kama Mzee bado yu hai, amaesema maneno ambayo hadi sasa bado ni mazima, Zanzibar imepoteza kiongozi shupavu.

Ibrahim Amani Ibrahim(86)amefariki na kuacha watoto 28 pamoja na wajukuu ambao idadi yao haijulikani.

Mungu aiweke roho yake marehemu mahali pema peponi .Ameeen