na Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari tawi la Songea na Arusha, vinavyoendeshwa na Chuo Kikuu cha St. Joseph.
Ni uamuzi uliofikiwa na TCU, baada ya kukiuka taratibu za uendeshaji. Hatua hiyo ya serikali ilitanguliwa na uamuzi wa uongozi wa chuo hicho, kukifunga kwa muda kutokana na vurugu za mara kwa mara zilizokuwa zikizushwa na wafunzi hao.
Wakati hayo yakitokea, tawi lingine la Dar es Salaam, liliandamwa na vuguvugu la kugoma, kwa kile wanachokidai ni kukosa haki zao za msingi.
HALI ILIVYOKUWA
Ilikuwa asubuhi, upepo na baridi uliokuwa umeambatana na mvua ya rasha rasha wakati Waziri wa Elimu Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alipowasili eneo la Chuo cha St. Joseph kilichopo Mbezi Luguruni.
Taswira ya ujio wake kwenye shule hiyo ilizua matumaini mapya kwa wanafunzi waliokuwa wamekusanyika chini ya miti iliyooteshwa kwa ustadi kando ya shule hiyo.
Waliinua mikono na wengine kuondoka chini ya miti wakijaribu kufuatilia gari la waziri lililowasili shuleni majira ya asubuhi saa 3 na dakika 24 asubuhi.
Licha ya wanafunzi hao kupokea ujio wa waziri katika sura ya furaha, lakini kwa waziri haikuwa kiu yake. Alijielekeza kiu yake katika kukagua madarasa na vifaa vya kufundishia wanafunzi hao.
Profesa Ndalichako alipitiliza moja kwa moja na kuwaacha wanafunzi hao ambao taratibu walianza kujongea kujaribu kumfuata, wakidhani angesimama ili kuzungumza nao.
Alipeleka salamu za ujio wake moja kwa moja kwa uongozi wa chuo hicho, ambao walimpokea kwa mikono miwili huku wakimuonyesha tabasamu la wasiwasi juu ya ujio wake.
Bila shaka waliwaza kuwa huenda amekwenda ‘kutumbua majipu.’
Mara baada ya kuwasili, hakupoteza muda wa kuwasikiliza, bali alielekea kukagua vifaa vya kufundishia ambako alitumia takribani dakika 45 kukagua madarasa hayo.
Hali haikuwa ya kawaida kutokana na watumishi kufanya kazi kwa wasiwasi, wakati wakimuelekeza namna vifaa hivyo vinafanya kazi, huku wakiwa hawafahamu nini hasa waziri huyo atawaeleza.
Mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, moja kwa moja aliketi na uongozi wa chuo hicho ili kumpa kinagaubaga cha wanafunzi hao kugoma.
Ofisa Uhusiano wa chuo hicho, Rechiel Jackon, anatumia fursa hiyo kumueleza kile ambacho wanafunzi hao walikuwa wakilalamikia, hali iliyosababisha kugoma kuingia darasani kwa siku tatu.
Maelezo hayo hayakumridhisha Waziri Ndalichoko na alilazimika kuhitaji kuongea na uongozi wa serikali ya wanafunzi hao, ambao kwa pamoja walishiriki kueleza kero zao bila ya uongozi wa chuo kushiriki.
Baada ya maelezo ya awali ya viongozi hao na madai yao, Waziri Ndalichako alilazimika kuvua nafasi ya uwaziri wa elimu na kuvaa nafasi ya mkazi na kuanza kuwapa elimu kama mama.
“Mambo mengine mnayonieleza inabidi niwasaidie kama mzazi sasa. Maana wanangu inabidi mtambue serikali inawathamini na ndio sababu imewekeza kwenu kwa kuwapatia mkopo. Yote mnayonieleza yanazungumzika” alitamka kwa upole.
Pamoja na kuendelea kuwaelekeza baadhi ya mambo kama mzazi na mlezi, Profesa Ndalichako anatumia nafsi yake ya kuwa mhadhiri na mkufunzi, kuwaelewesha kuwa mitaala ya masomo ya sayansi haibadiliki kwa vyuo vyote duniani, bali inatokana na ufundishaji wa walimu.
Awali, viongozi hao wa wanafunzi walimueleza Profesa Ndalichako kuwa, baadhi ya walimu wanaowafundisha wana umri mdogo na hawakidhi vigezo vya kutoa elimu vinavyotakiwa, pia vyumba vya kufundishia kwa vitendo masomo ya uhandisi na sayansi havitoshelezi.
“Pia walimu wanatufundisha wanatumia mitaala inayotumika kufundishia wenzetu wa masomo ya sayansi haituwezeshi kuwa na sifa ya kuwa wataalamu wazuri,” anasema mmoja wa viongozi hao.
Jambo hilo lilimfanya Profesa Ndalichako kumkatisha na kumueleza kuwa:“ Nilishakuwa mkufunzi (mhadhiri) wa masomo ya sayansi nchi nyingine, hivyo mtambue kuwa mitaala inayofundishia wanafunzi wa vyuo kwa masomo ya sayansi haibadiliki. Ndio sababu nimeweza kufundishia nchi nyingine japokuwa elimu yangu nimepatia nchini.”
Waziri wa Elimu wa wanafunzi hao, Emmanuel Lyatuu, alimueleza Profesa Ndalichako kuwa, wanafunzi wanaomaliza ngazi ya stashahada na kujiunga na shahada, huwa wananyimwa fedha za kwenda mafunzo kwa vitendo hadi wanapoingia mwaka wa pili, lakini wale wanaomaliza kidato cha sita na kujiunga na chuo hupatiwa fedha hizo.
Baada ya kuketi na wanafunzi hao kwa zaidi ya saa moja, alilazimika kuzungumza na wanafunzi juu ya makubaliano yao kusitisha mgomo, baada ya kubaini hakuna madai ya msingi kati ya yote waliyoyaeleza.
AKUTANA NA WANAFUNZI WOTE
Akiwa katikati ya kundi la wanafunzi ambao walimpokea kwa shangwe zilizompa nguvu mpya ya kuanza kuzungumza nao licha ya kuwa alionekana ameshachoshwa na mazungumzo ya viongozi alipokuwa ndani.
Profesa Ndalichako anaanza kwa salamu, huku akiwahakikishia wanafunzi amekuja kumaliza mgogoro huo.
Rais wa wanafunzi hao, Celestine Makota, alikuwa wa kwanza kuzungumza kwa kuwatuliza wanafunzi wenzake wamsikilize waziri huyo.
Mara alipoanza kuzungumza na wanafunzi waliokuwa wamesimama kwenye jua saa 6 na dakika 45 mchana, walimpokea kwa kelele za kumtaka atumbue majipu.
Profesa Ndalichako alianza kubainisha aliyoelezwa na viongozi wao, baadhi yakipingwa vikali na wanafunzi ambapo mengine yalipingwa vikali na wanafunzi hao kwa kuzomea.
Hali hiyo ilimfanya aanze kuwasihi kwamba waheshimu muda wake alioutoa kwa ajili ya kwenda kuwasikiliza, badala ya kumshutumu kwa kuzomea.
Pia aliwaeleza juu ya kile alichokibaini kwa wanafunzi hao kuwa ni kutaka chuo hicho kifungwe kama vilivyofungwa vinginge ambavyo ni vya mmiliki mmoja.
“Haiwezekani kufanya kazi kwa mashinikizo. Nilichokibaini hapa mnataka chuo (St. Joseph- Dar es Salaam) nacho kifungwe kama vingine vilivyofungwa. Hili halikubaliki! Hataujaona tatizo kubwa la kukifanya chuo hiki kifungiwe au muendelee na mgomo wenu,” anasema.
Akatumia muda huo kuwataka wanafunzi warudi darasani na kuanza kujiandaa kwa mitihani ambayo aliagiza ianze kufanyika Jumatatu wiki hii.
“Baada ya kukaa na uongozi wa chuo, viongozi wa serikali ya wanafunzi na kuhoji sababu za mgomo huu sijaona jambo kubwa la kupelekea (kusababisha) chuo hiki kifungwe, bali matatizo yote yanaweza kufanyiwa kazi mara moja na wanafunzi wakaendelea na masomo yao,” anasema .
Pia akaiagiza TCU kuhakikisha inashughulikia matatizo yote yaliyoainishwa na wanafunzi hao, ikiwamo kuwachunguza watumishi waliolalamikiwa.
“Mkimaliza mitihani mnafunga chuo wiki mbili. Hakikisheni mnamaliza matatizo yote yaliyoainishwa mara moja kuhusu watumishi wa TCU ambao hamna imani nao na wenyewe tutawachunguza na hatua zitachukuliwa,”anasema.
AWAPA ONYO
Profesa Ndalichako alitumia fursa hiyo kuwaonya wanafunzi walioonekana kuwa wajeuri na kutoheshimu taratibu za chuo hicho, kuwa hata wao watetea endapo watafukuzwa shule.
Anasema:“Kama mtashindwa kufuata taratibu na kanuni za chuo na kufanya mambo yaliyo kinyume uongozi wa chuo ukiwafukuza serikali haitawatetea.”
Pia, anawataka kuendelea kulipa ada waliyokubaliana na chuo hicho kabla ya kujiunga na kwamba, hataweza kuushinikiza uongozi wa chuo upunguze, wakati walishaamua kusoma hapo.
Ahadi ya waziri ni kwamba, suala la ada elekezi kwa vyuo vikuu nchini lilatolewa baadaye mwaka huu na serikali.
KATIBU TCU ATETA
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, anahoji sababu za wanafunzi hao kugoma wakati wao - TCU wapo ajili ya kushughulikia matatizo yao.
Anasema jambo hilo walilishughulikia kwa kukaa nao, lakini walitaka madai yao yafike kwa waziri ambaye hata hivyo amefika.
“Maagizo yaliyotolewa na waziri, tutaanza kuyafanyia kazi mara moja na kwamba watashirikiana na serikali ya wanafunzi na uongozi wa chuo, kubaini changamoto zilizoelezwa, ili kuzitafutia ufumbuzi,” anasema na kuendelea:
“Hatuwezi kusema changamoto hizi zitaisha lini, lakini kama tulivyoelekezwa tunaanza kuzifanyia kazi mara moja na malalamiko mengine kama mlivyoona yameshaanza kutafutiwa ufumbuzi,” anasema.
Anaeleza sababu za kuitwa ‘jipu’ na wanafunzi hao, kushindwa kutii matakwa ya baadhi ya wanafunzi, wahamishiwe katika vyuo vingine au kukifunga chuo kama ilivyofanyika kwa tawi la Arusha na Songea.










