Utandawazi, kukosa maji kwaongeza mimba shuleni Tabora.

15Mar 2016
Gaudensia Mngumi
Nipashe
Utandawazi, kukosa maji kwaongeza mimba shuleni Tabora.

UKOSEFU wa huduma za jamii na kuwaacha watoto huru kupindukia, inatajwa kuwa sababu za mabinti kubakwa, kupewa ujauzito na kuozwa utotoni.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbola wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Aloyce Zacharia

Mtendaji wa Kijiji cha Mbola wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Aloyce Zacharia, anasema kukosekana maji, mabweni, chakula au migahawa shuleni kunawakwamisha wasichana masomoni.

Anayaeleza hayo wakati wa utafiti uliofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Watu (UNFPA) mkoani Tabora mwaka jana, kuchunguza vitendo vya unyanyasaji watoto na wanawake.

Uhaba wa maji umewalazimisha watoto wa sekondari na msingi kutembea umbali mrefu tena usiku kutafuta maji na kukutana na wanaume waharibifu wanaowahadaa.

“Shuleni hakuna bweni wanaishi mitaani.Hakuna maji wanayatafuta usiku muda ambao wanaume wanawafuatilia na kuwashawishi kufanya ngono kwa ahadi za kuwachotea maji, kuwahamishia maeneo yenye maji na kuwapa fedha za kujikimu ili wasiteseke,” anasema Zacharia.

Anaendelea kusema:“Kuishi mitaani kwa kukosa mabweni kunawafanya kuwa huru mno kwani hakuna udhibiti. Wanapokuwa huru wanadanganyika zaidi kwa ahadi za kupewa simu, fedha na nguo nzuri.”

Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mabinti hawa walio huru wanakuwa wateja wa disko usiku, mikesha ya harusi ama ya sherehe za kijamii usiku kucha bila hofu.

Anasema kwa vile hakuna wanaowafuatilia wanakwenda kwenye mabanda ya video mitaani wakati wote kutizama sinema hata za ngono.

“Hapa wanakutana na watu wanaorubuni kirahisi ikiwa ni pamoja na kuwapangia vyumba na kuwatumia kingono,” anasema kiongozi huyowa kijiji.

Baadhi ya Shule za Kata kama Ilolangulu na Ndono wilayani Uyui, hazina mabweni kwa hiyo wanafunzi hulazimika kupanga mitaani.

Wasichana huhadaiwa kuwa watawalipiwa vyumba, kukodishiwa bodaboda za kuwapeleka shuleni, kupewa chakula na mavazi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilolangulu, Abdallah Sikwala, anasema wazazi wanashindwa kujenga mabweni sababu ya umaskini kwani ni vigumu kuchangisha fedha kwa vile hawana kipato wala fedha ya kukimu familia.

“Utawaomba watu michango inakuwa ngumu zaidi.Mimba za wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari zinapatikana kwa vile wamekosa ada na fedha za kujikimu shuleni kwa vile wazazi hawana kipato cha kuwaendeleza,” anasema Sikwala.

Hata hivyo, hana takwimu zinazoelezea ukubwa wa tatizo hilo, kijijini kwake.

Pili Salum Malembeka, mama aliyetelekezwa na kushuhudia wanae wakipata ujauzito, anazungumzia suala hili kuwa watoto wakiwa kwenye nyumba za sinema mchana, mikesha au wakiranda mitaani kwa kukosa mabweni shuleni wengi hushawishiwa na kutumbukia kwenye ngono.

WALIMU

“Pamoja na udanganyifu huo walimu wanatuhumiwa na ujauzito shuleni kwani hutumia mbinu za kuwafundisha mabinti twisheni au kuwaomba wasaidie kazi za nyumbani kisha huwarubuni na kuwabaka,” anasema Rose Yakub.
Rose ni mzazi mwenye miaka 45, ana mabinti walioathirika na ujauzito shuleni.

Rose na Pili wanaongeza kuwa walimu wengine vijijini wanawahadaa wanafunzi kwa twisheni. Lakini ili kuficha lengo wanawapa kazi kama kuosha vyombo au hata kutafuta kuni au kusafisha nyumba.

“Wanaweza kuwaambia watoto kabla hamjaondoka nisaidieni kusafisha sufuria au vyombo. Anatumia ujanja kuwa siyo vingi wengine mnaweza kutangulia ‘fulani’ akazimalizia ili msichelewe,” anasema Pili.

Anaongeza: “Baada ya wanafunzi wengine kuondoka mwalimu anambaka binti aliyembakiza kusafisha vyombo au kufagia nyumba na kumtisha kuwa iwapo atatoa siri atamuua.”

Pili amefukuzwa na mume kwa kumwandikia talaka kuwa hamtaki pamoja na kizazi chake na kusambaza nakala ofisi ya Kijiji cha Ilolangulu Kusini, pia kwa wazazi na jamaa zake.

Anasema:“Wanaume hawana maadili wanaona ni vyema kurubuni watoto ili wapate ngono kwa gharama nafuu. Wanahofu kuwa wakiwafuata watu wazima watawapa pesa, chakula na kuwaomba mahitaji ya kujikimu. Wanaume hili wanalikwepa ndiyo maana wanakimbilia kwa mabinti zetu wasiojifahamu.”

Pili anasema mara nyingine watoto wanalazimishwa kuolewa na watu wazima wenye zaidi ya miaka 40 wakati mabinti wana miaka 15.

“Ndoa kama hii imejaa manyanyaso kwani haina upendo, mwanaume anatumia shida za mkewe kumtusi, kumpiga na muda wote analewa pombe,” anaongeza Pili.

Anafafanua kuwa mabinti huolewa nyakati za msimu wa mavuno ambao Tabora ni maarufu kama ‘mapokezi’ yaani muda wa kupokea fedha.Hiki ni kipindi cha neema kwa wakulima kwani vyama vya ushirika huwalipa wakulima fedha zao.

Anaeleza kuwa wakati wa mavuno uhasama hukithiri kwenye ndoa kwa vile wanaume wana fedha nyingi na hukimbilia kwa mabinti wasiojua kujitetea,wasiokuwa na gharama wala hofu ya kuambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Ndiyo maana wanawake wanapika na kuuza pombe za kila namna ili kupata chakula cha familia akiwamo baba ambaye ni mtegemezi.

Matatizo ya familia kama ndoa za utotoni, watoto kushindwa kusoma yana mzizi ndani ya wanaume ambao wanatarajiwa kutunza na kuongoza familia, lakini hawafanyi hivyo.

WAZAZI NI KIKWAZO

Hadija Selemani mkazi wa Kijiji cha Ndono, wilayani Uyui, anasema wazazi hasa baba wanawavunja moyo mabinti kwa kuwaambia maneno ya kukatisha tamaa.

Anasema wanawaambia mabinti maneno haya; ‘Kusoma siyo kupata wakimaanisha kuwa maisha hayapo darasani, mafanikio yamo kwenye kile wanachowaeleza.’

Pia wanawaambia ‘angalia binti wa fulani mbona kasoma, lakini hakuna alichopata, sikashindwa mko naye hapa.’

Ananukuu maneno ya vijana na jamaa wa nyumbani kwao wanaomwambia: “Unachelewa viwanja,utakuta wenzako wamejenga, wamezaa, utasoma hadi lini,’ angalia wenzako wa shule za kata wanavyoboronga.”
Hadija anasema: “Kauli hizi zinakatisha tamaa labda kama binti hana watu wa kumtia moyo.”

Mabinti waliopata ujauzito ambao pia hawajasoma, Chiku Ramadhani (18) na Zuena Iddi (17), wakazi wa Kijiji cha Kiyungu wilayani Urambo hawakusoma hata darasa moja.

Maelezo yao yanawatuhumu wazazi (baba), kuwa alisisitiza kuwa hawawezi kwenda shuleni kwa vile watapata mimba na hakuna watakachovuna.

ATHARI

Mabinti hawa ambao wameolewa utotoni, lakini pia hawakusoma wanataja athari ya kushindwa kujiajiri ili kuendesha maisha yao kuwa ni athari wanayoiona.

Kushindwa kuwachagua viongozi kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana kwani hawajui kusoma.Kadhalika wanashindwa kujiamini.

Kwa upande wake, Zuena anasema kukosa elimu na kuolewa akiwa mtoto kumesababisha aishi ndani ya mila za kishirikina.

“Kila mara nikiumwa ninakwenda kwa waganga, ninachoambiwa ni kurogwa, watoto wakifa wamerogwa. Tunaishi kwa hofu ya kurogwa, lakini ningekuwa nafahamu kusoma na kuandika ningekwenda mbali kutafuta tiba za kisasa,”anaeleza.

Anaongezea kuwa athari nyingine za kukosa elimu ni watoto kulelewa na bibi na babu, hivyo kukosa upendo wa wazazi kwa vile wazazi wao nao ni watoto.

Anataja hatari ya kupata fistula na ulemavu. Kadhalika kuambukizwa VVU utotoni na kutelekezwa kuwa ni mambo yanayowanyemelea mabinti.

UDHIBITI

Asasi za kiraia zinafuatilia mathalani Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu ya Tabora Paralegal, ilivyofuatilia suala la polisi kuzembea kwenye kesi ya mtuhumiwa wa ubakaji.

Asasi hii, Novemba 20, 2014 ilimwandikia Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Uyui, kuhoji sababu za askari kulinda mtuhumiwa wa ubakaji wa mwanafunzi wa miaka nane (majina na barua tunazo).

Zinaeleza kuwa hospitali ilithibitisha kosa hilo, lakini mtuhumiwa alitoweka baada ya kuandaliwa uhamisho uliomwondoa Tabora Manispaa na kuua kesi hiyo, akidaiwa kuwa haonekani.

Ofisa Elimu Taaluma -Sekondari wa Wilaya ya Urambo, Lilian Rubaba, anasema kujenga mabweni shuleni hapo kumepunguza mimba na ndoa hizo.

Anathibitisha kwa takwimu kuwa mwaka 2013, wanafunzi 14 walipata ujauzito wakati Novemba mwaka juzi walikuwa sita.
Rubaba anaamini kuwa kukiwa na maji, mabweni, chakula na ufuatiliaji shuleni mimba na utoro utapungua.