Mashabiki wa soka wanaokwenda kuangalia mechi, hususan zile kubwa ambazo ni kioo cha soka letu la Tanzania, pambano linapomalizika hawazungumzii tena jinsi mechi ilivyochezwa.
Hawazungumzii tena wachezaji waliong'ara kwenye mechi hizo, matukio au vituko vilivyojitokeza kama ilivyokuwa hapo zamani.
Siku hizi mechi za Simba na Yanga, au Yanga na Azam zikimalizika 'nyota wa mchezo' wanakuwa ni waamuzi.
Kwa sasa ndiyo wanazungumzwa uwanjani, mitaani, barabarani, kwenye mitandao ya kijamii na kwenye vijiwe vya michezo na kahawa.
Waamuzi hawa hawazungumzwi vizuri na mashabiki wa soka. Wanazungumwa vibaya kuwa wanatumia vibaya nafasi zao.
Wengi wa mashabiki mitaani wanadai kuwa si kwa sababu wao wanakaa majukwaani basi hawajui sheria za soka.
Wanasema kinachofanywa na waamuzi, ndicho kinasababisha baadhi yao kutoona ulazima wa kwenda kuangalia soka uwanjani.
Wanadai wanakwenda uwanjani kuangalia soka ili anayestahili kushinda na ashinde, siyo timu ishinde kwa msaada wa mwamuzi.
Mashabiki wanapotoka uwanjani wanataka wauzungumzie mchezo kama walivyokuwa wakifanya zamani.
Lakini sasa ni tofauti kabisa. Waamuzi ndiyo wanaonekana 'kulibeba' pambano lenyewe na si wachezaji. Wao ndiyo nyota wa mchezo.
Wanasema makosa ya kibinadamu yako hata kwa waamuzi Ulaya, lakini ni kwa matukio machache zaidi.
Lakini hapa nyumbani, mwamuzi anaweza kuchemsha kwenye maeneo zaidi ya manne au matano na wakati mwingine yote. Inaumiza sana.
Nimekusanya baadhi ya kauli za mashabiki, naamini ukizisoma unapata ujumbe.
Kwa nini mechi za Simba na Yanga, au Yanga na Azam zimekuwa na uamuzi wa utata?
Kwa nini mechi hizo kwa siku za karibuni ni waamuzi ndiyo wanaolalamikiwa kila zinapomalizika?
Kwa nini kwenye mechi hizo kuna rafu mbaya hazitolewi uamuzi na marefa? Hawazioni?
Mpira unapomalizika mashabiki wanataka kujadili jinsi pambano lilivyokuwa
Wachezaji gani waling'ara, mchezaji gani alichemsha. Wala hawataki kujua hata jina la mwamuzi aliyechezesha. Lakini kwa sasa wanalazimishwa kujua ni refa gani aliyechezesha pambano.
Wakihojiwa na na kituo cha radio kuhusiana na malalamiko ya waamuzi, Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), Salum Chama walisema kuwa tatizo lililopo ni kwamba baadhi ya viongozi, wanachama na mashabiki huwalaumu waamuzi pale timu zao zinapofungwa au kutopata matokeo waliotarajia.
Wakihojiwa kwenye kipindi kimoja cha michezo kwa nyakati tofauti, walidai kuwa malalamiko hayo wanayasikia kwenye vyombo vya habari, lakini hayapekwi kwao kimaandishi ili yafanyiwe kazi.
Lakini pia wakadai kwa msimu huu malalamiko yamepungua tofauti na msimu uliopita.
Kwa hili la kupeleka malalamiko kimaandishi naliunga mkono, kwani baadhi ya viongozi wanakimbilia kwenye vyombo vya habari kulalamika badala ya kuwasilisha malalamiko TFF.
Lakini pamoja na hayo, bado TFF kupitia vyombo vyake hivyo ina wajibu wa kufuatilia nyendo na uchezeshaji wa waamuzi.
Mfano, Januari mwaka jana kamati hiyo ya waamuzi ilimuondoa kuchezesha mechi za Ligi Kuu refa Mohammed Theofile siku moja tu baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.
Na hii ilitokana na vyombo vya habari kutoa picha ya mchezaji mmoja wa timu hiyo akionekana kumdhibiti isiyotakiwa mshambuliaji wa Yanga Amissi Tambwe, tukio ambalo halikuonwa na mwamuzi huyo.
Sidhani kama kwa siku hiyo moja tu Yanga ilikuwa imepeleka malalamiko yao na kupokelewa na kufanyiwa kazi.
Je, kama kamati ilikuwa na uwezo wa kufanya hivyo, mbona kuna rafu mbaya zinachezwa kwenye mechi kadhaa za ligi bila kuchukuliwa hatua?
Je, Kamati ya Waamuzi ambayo ilikuwa ikikutana kupitia CD pamoja na taarifa za makamisaa wa mechi kuangalia uwezo na udhaifu wa marefa msimu huu haipo?
Kweli mashabiki wamechoshwa na uchezeshaji mbovu wa waamuzi wa soka na mbaya zaidi ni kutochukuliwa kwa hatua zozote.
Kwa nini makosa haya yanayoitwa ya ‘kibinadamu’ ukiondoa mechi kubwa zinazozihusu timu kubwa za Simba, Yanga na Azam, huziumiza zaidi timu ndogo?










