Fitina, utawala mbovu, majungu, kutowajibika vinaua soka nchini - 2

14Mar 2016
Romana Mallya
Dar
Nipashe
Fitina, utawala mbovu, majungu, kutowajibika vinaua soka nchini - 2

KWA muda mrefu soka la Tanzania limekuwa likilalamikiwa kuwa ni ‘kichwa cha wendawazimu’ kutokana na matokeo mabaya ya timu zake kongwe kitaifa na kimataifa.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

Licha ya timu kongwe Simba na Yanga mara kadhaa kuvuka mipaka kusaka makocha wa kimataifa wakiamini ndio wenye uwezo wa kulivusha soka letu, lakini mwisho wa siku, wameishia kuwatimua mara timu hizo zinapoboronga katika ligi. Mtafiti mzalendo wa soka, Dennis Manumbu, amefanya tafiti ambazo anaamini Serikali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na klabu kama zitaungana naye, soka litapiga hatua. Inaendelea kutoka wiki iliyopita.

MCHANGO WA SERIKALI
Mtafiti anasema licha ya serikali kuwa mdau mkubwa, lakini haingilii moja kwa moja masuala ya soka kwa sababu yako chini ya TFF.

“Michango ya serikali ni kuwepo kwa sheria mbalimbali zinazotambua soka kama mojawapo ya michezo na kuwa chini ya usimamizi wa TFF, serikali inatimiza wajibu wake,” anasema.

KUPOROMOKA KWA SOKA
Manumbu anasema miaka ya 1970 na 1980, Taifa Stars na klabu za Tanzania zilikuwa tishio katika mashindano ya kimataifa.

“Inawezekana timu tishio ikawa inajengwa na wachezaji wageni, hivyo ikawa haina mchango wowote katika kutoa wachezaji bora wa Taifa Stars au timu tishio ikajengwa na wachezaji wazawa ambao wataunda Taifa Stars tishio,”anasema na kuongeza:

“Kuporomoka kwa kiwango chetu cha soka katika klabu na Taifa Stars kumesababishwa na kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa utambuzi wa wachezaji wenye vipaji tangu wakiwa na umri mdogo na wale wanaotambulika kutokusimamiwa vizuri hivyo hukata tamaa.

Pia anasema sababu nyingine ni soka kuondolewa kwenye vipaumbele vya wizara na taasisi za serikali tofauti na zamani kilikuwa kigezo kimojawapo cha ajira.

Aidha, anasema awali kulikuwapo na uwanja mpana wa kuwapata wachezaji, lakini baada ya serikali kuondoa sera ya kuwepo michezo kwenye shule za msingi na sekondari na kufanya wigo wa kupata wanasoka kuwa mdogo.

Lakini pia, anabainisha sababu nyingine ni mpira kukabiliwa na mmomonyoko wa maadili kuanzia kwa viongozi, makocha, waamuzi na wachezaji, kubadilika kwa hali ya maisha kiuchumi, ambayo imesababisha maisha duni kwa jamii, kuweka mikakati ya zimamoto ambayo haina tija katika kuinua soka zaidi ya kuigharimu TFF.

“Tanzania kuwa na makocha wachache na uhaba wa wataalamu wanaoendana na soka la ushindani wa mashindano ya kimataifa,”anasema.

JE, VIWANJA VINAKIDHI?
Mtaalamu huyo anasema havikidhi haja ya kukuza soka kwa sababu vimegawanyika katika makundi ya ngazi ya taifa, mikoa, wilaya na maeneo mengine.

“Vile vya ngazi ya taifa, vinakidhi vigezo vya kukuza soka vilivyowekwa na Fifa, lakini vya ngazi ya mkoa na wilaya havikidhi vigezo vya kukuza soka kwani, vingi havina vyoo, havijakamilika vipimo, havina alama za msingi, sehemu yake ya kuchezea ni kipara na ina mabonde na miinuko, havina miundombinu ya kutoa maji kipindi cha mvua,” anaeleza.

ANAWAZUNGUMIZIAJE MAKOCHA WAZAWA
Manumbu anasema wamegawanyika sehemu mbili wale wanaofundisha wanasoka wa timu za wakubwa na wale wa timu za watoto.

“Hawa wana leseni za ukocha za madaraja tofauti kutokana na vigezo walivyovitimiza, lakini pia wapo wengine ni makocha kwa jina kwa kutokuwa na leseni na vyeti vya ukocha wa soka ambao kwa mazingira ya nchi yetu ndio wengi wanafundisha timu za mitaani na madaraja ya chini,” anasema.

Anasema wanahitaji kuongezewa elimu ya ukocha wa mpira ili waweze kuendana na mabadiliko ya kukua kwa mbinu na ufundi wa soka duniani ili waingie kwenye ushindani na makocha wa nchi nyingine.

Anasema mfumo wa ufundishaji wa kozi za soka unatakiwa kuimarishwa na kutolewa mara kwa mara kuanzia kwenye kiwango cha cheti cha awali, cheti cha kati, cheti cha juu na kozi maalum za wakufunzi toka nje.

Pia TFF inatakiwa ije na motisha ya kuwashawishi wadau wa soka wafungue shule za ufundishaji wa ukocha wa soka kwa viwango tofauti.

“TFF ngazi ya wilaya na mkoa zifanye utambuzi wa makocha ambao wapo ngazi za vitongoji, vijiji/mitaa, kata na wilaya na kuwaainisha kiuwezo na kiviwango kisha iwepo program ya kuwaendeleza,” alisema.

Anafafanua kuwa, kwa ujumla makocha wazawa hawawezi kushindana kwenye ushindani wa ajira na makocha wa nchi nyingine kutokana na uchache wa utolewaji wa kozi za ukocha hapa nchini, huku uwezo wa wakufunzi wa ndani nao mdogo.

Akitoa maoni yake kuhusu vyuo vya michezo kama kile cha Malya cha Mwanza, anasema vinatoa masomo kwa utaratibu wa kutoa kozi za jumla za michezo.

“Madhara yake ni kuminya mgawanyo wa michezo kama soka, riadha, netiboli isipate muda wa kutosha kufundishwa, mitaala ya kozi za Malya nilizofanikiwa kuziona za kufundisha michezo, soka linafundishwa kwa kiwango cha chini vitu muhimu ambavyo kocha wa mpira anatakiwa avijue havimo kwenye mitaala, hivyo bado hatujapata mwarobaini ya kupandisha kiwango chetu cha soka,” anasema.

Anasema mabadiliko ya ufundi na mbinu za soka ambazo zinabadilika kila mara, wakufunzi wanatakiwa wazijue kwa kuzisoma, kuzielewa na kuzitekeleza ikiwezekana na kuziandikia vitabu kwa lugha ya Kiswahili ili makocha wazawa waelewe kwa sababu waliowengi wana elimu ya chini.

MTAZAMO WAKE KWA MAREFA
Anasema marefa wa sasa kiwango chao cha uchezeshaji kipo chini na uthibitisho ni wale wanaofungiwa na kuondolewa kwa kuchezesha kwa kiwango kibovu na wanaoshindwa mitihani ya urefa.

“Viwnago vipo chini kutokana na kuwa na uelewa mdogo wa elimu ya urefa na kushindwa kutafsiri sheria za soka, kuwa wabunifu mchezoni, kutokuwahi sehemu ya matukio na kutokufanya uamuzi kwa wakati, utimamu wa mwili kuwa dhaifu,” anasema na kuongeza:

“Utafiti wangu unaonyesha wana ukosefu wa maadili, wanapokea rushwa na kufanya uamuzi wa upendeleo, kukosa uzalendo wa nchi, lakini wanaathiriwa na hali ya uchumi wa nchi kwa kukosa vitendea kazi, kutokuwepo motisha za kuvutia na uhaba wa kozi za mara kwa mara,” anasema.

NINI TATHMINI YAKE YA KIUFUNDI
Mtafiti huyo anabainisha kuwa ianzishwe programu maalum ya utambuzi, ukusanyaji, uendelezaji watoto kuanzia miaka 5 hadi 17 wenye kipaji cha kucheza soka kuanzia ngazi za wilaya hadi mikoa.

Pia kukaa na wadau wa michezo, kuwashawishi kwa kuandika na kuwapatia mwongozo wenye masharti nafuu ya uanzishwaji timu za soka za watoto.

Kadhalika, ianzishwe programu maalumu ya utolewaji wa kozi za mara kwa mara za ukocha na urefa zenye masomo yanayoendana na soka la kisasa ili waweze kushindana katika fursa za ukocha/urefa kitaifa na kimataifa.

Anabainisha nyingine ni sheria na kanuni za mpira wa miguu zipitiwe na kuja na kanuni zitakazoleta tija kukuza na kuendeleza soka la Tanzania.

“Kuimarisha na kupitia muundo wa menejimenti kuanzia ngazi ya klabu, vyama vya TFF wilaya, mkoa na taifa kwa viongozi kupata semina za uongozi wa soka, kuthibiti vitendo vya rushwa katika soka kuanzia kwa wachezaji, makocha, marefa, viongozi, wanachama, wapenzi na wadau wa soka kwa kutunga kanuni zenye adhabu kali,” anasema na kuongeza:

“Kutengeneza mfumo wa eletroniki wa kukusanya mapato ya soka viwanjani, TFF ikae na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuja mkakati wa kuboresha viwanja vya soka vilivyo chini ya umiliki wake,” anasema.

Pia anasema Serikali ishirikishwe moja kwa moja kwenye maendeleo ya soka kwa kuweka bajeti maalum ya kutekeleza mipango ya uendelezaji wa soka kuanzia ngazi za chini na irudishe na kuwekeza katika soka mashuleni na vyuoni.
Manumbu anasema TFF itafute wafadhili, watu wa masoko wa ndani na nje ili kutoa rasilimali zikiwemo vifaa, fedha kwa ajili ya kuendeleza soka.

“Mawakala wa wachezaji wenye weledi wapatikane wa kutosha kwa ajili ya kuwatafutia wachezaji timu za ndani na nje ya Tanzania na kuingia mikataba yenye masilahi kwa wachezaji,” anasema.

SIASA NA MAENDELEO YA SOKA
Anasema mazingira ya siasa ni dhaifu kwa maendeleo soka kwa sababu pamoja na kutokutajwa moja kwa moja kwenye Ilani, wakati wa utekelezaji inaundiwa wizara inayojumuisha michezo yote.

“Kwenye programu za wanasiasa wamekuwa wanaitumia soka kama ghiribu kwa wapigakura kipindi cha uchaguzi unapokaribia utawaona wanaanzisha mashindano, wanagawa vifaa kama jezi, mipira, viatu… Na wakati mwingine wanapoombwa msaada na timu za soka za majimbo yao wengine wanakimbia,” anasema na kuongeza:

“Wakati mwingine wanasiasa wamekuwa wanaingizwa kwenye kamati za kuleta ushindi, kutengeneza programu za maendeleo ya soka lakini bado hatupigi hatua kwa maslahi yao binafsi, Kwa hiyo naweza kusema siasa inafanya usanii kwenye maendeleo ya soka letu,” anasema.

MUUNDO WA TFF KUKUZA SOKA
Anasema muundo wa TFF wa sasa wa soka kuanzia vijijini hadi ngazi ya taifa sio sahihi katika kukuza soka kwa sababu ipo kuanzia ngazi ya wilaya.

“Tuangalie kwenye ngazi ya wilaya vyama vya mpira havijiwezi kabisa vipo taabani, vyama vingi kolamu ya uongozi haikamiliki na viongozi waliopo ni dhaifu kuendeleza soka, hakuna msaada na usimamizi wa moja kwa moja wa TFF Taifa, muundo huu ujengwe upya na tathimini ifanyike kubaini udhaifu,” anasema.

Akitoa maoni yake kuhusu ligi kuanzia zile za madaraja ya chini hadi juu kama zina nafasi ya kukuza soka, anasema mfumo wake unaleta ushindani, na ni mzuri na una timu chache kwa kila daraja hivyo hauchoshi wachezaji.

“Ligi zetu hizi ni nzuri katika nafasi ya kukuza soka letu changamoto kubwa ni uwekezaji, hivyo zinachezeshwa kimasikini sana,” anasema.