Timu hiyo yenye makazi yake Mtaa wa Msimbazi inaweza ikawa inashindana na Mtibwa Sugar, ambayo nayo ina baadhi ya wachezaji waliotapakaa kwenye klabu mbalimbali, ingawa yenyewe wengi wao wapo Simba na Yanga.
Kwenye Ligi Kuu msimu huu kuna wachezaji wengi ambao wameshawahi kuichezea Simba kwa vipindi tofauti, lakini bado wanaendelea kutamba kwenye klabu zingine.
Wengi walihama kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kusajiliwa na timu nyingine, kumaliza mikataba yao na kutoongezewa, kutemwa kwa madai ya kushuka viwango, wengine kutolewa kwa mkopo.
Wafuatao ni wachezaji bora 11 waliokuwa wakiichezea klabu hiyo, lakini hadi leo wako fiti na wanaendelea kukipiga na klabu zingine kwenye msimu huu.
1. Ally Mustapha 'Barthez'-Yanga
Kipa wa timu ya Taifa Taifa Stars. Ndiye kipa tegemeo kwa sasa kwenye kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga.
Alijiunga na timu hiyo mwaka 2012 akitokea Simba alikodaka kwa mafanikio makubwa baada ya kuondoka kwa Juma Kaseja aliyekuwa akimweka benchi.
2. Salum Kanoni-Kagera Sugar
Beki wa kulia wa zamani wa Simba. Aliichezea timu hiyo kuanzia 2010 na kuwa beki wa kuaminika. Hata hivyo, mkataba wake ulimalizika 2012 na viongozi kushindwa kuafikiana hivyo kutimkia Kagera Sugar.
Kwa sasa ni mhimili mkubwa wa klabu ya Kagera Sugar, akisaidia kupeleka mashambulizi mbele, kuzuia, pia ni 'mtaalam' wa kupiga mikwaju wa penalti
3. Juma Jabu-Kagera Sugar
Kama Kanoni, aliichezea Simba mwaka 2010 akitokea Ashanti, akaichezea kwa mafanikio hadi alipomaliza mkataba wake 2012. Baada ya kuondoka Simba alicheza klabu kadhaa. Kwa sasa yupo Kagera Sugar akiwa na Kanoni.
3. Miraji Adam-Coastal Union
Huyu ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi hiki yupo nje ya Simba kwa mkopo.
Alikuwa kwenye kikosi cha pili cha Simba na kupandishwa na wenzake msimu wa 2013/14 na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Patrick Liewig, ambaye hakukaa sana akaletwa Zdravko Logarusic.
Kutokana na vita ya kugombea namba kwenye kikosi hivyo, Simba ilimpeleka Coastal Union na sasa anafanya vizuri akiifungia timu hiyo magoli ya 'frii-kiki' dhidi ya Yanga na Azam.
Kuna asilimia 90 ya Simba kumrejesha tena kwenye kikosi msimu ujao.
4. Haruna Shamte-Mbeya City
Tumemuona hivi karibuni kwenye mechi kati ya timu yake za zamani Simba dhidi ya Mbeya City.
Alicheza kwa ustadi mkubwa na kuwazuia kwa muda mrefu mastraika wa Simba kabla ya kuzidiwa ujanja mwishoni. Alikuwemo kwenye kikosi cha msimu wa 2013/14 akiwa na kina Miraji Adam. Baada ya msimu huo alijiunga na JKT Ruvu, lakini kwa sasa anaichezea Mbeya City.
5. Kelvin Yondani-Yanga
Alikuwa beki wa kati wa kutegemewa wa Simba. Mara mwisho kuichezea timu hiyo ni msimu wa 2011/12.
Alisajiliwa kiutata na Yanga baada ya kutoroshwa kwenye kambi ya timu ya taifa usiku na kwenda kusaini fomu.
Habari zilidai kuwa kazi hiyo ilifanyika kwa msaada wa kiongozi mmoja ndani ya Shirikisho la Soka Tanznaia (TFF), ingawa ilitoa taarifa ya kuwa itatoa tamko kuhusiana na kilichofanyika.
6. Abdallah Seseme-Toto Africans
Mmoja wa viungo waliolelewa kwenye kikosi cha pili cha Simba na baadaye kupandishwa kikosi cha kwanza.
Hata hivyo, ilikuwa ni ngumu kwake kupata namba mara kwa mara kama wenzake Said Ndemla na Jonas Mkude. Kwa sasa anakipiga Toto Africans.
7. Haruna Chanongo-Stand United
Ni mmoja wa wachezaji kutoka kikosi cha pili cha Simba aliyechukua muda mfupi tu na kuanza kutamba kuliko wenzake wote.
Aliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza na kuchukua nafasi ya Uhuru Selemani kuanzia msimu wa 2012/13.
Hata hivyo, haikuchukia muda mrefu kiwango chake kilianza kupungua kabla ya kupelekwa kwa mkopo Stand United.
8. Amri Kiemba-Stand United
Mchezaji mkongwe aliyeisaidia sana Simba akiwa kwenye kiwango chake. Ingawa aliwahi kuichezea Yanga, lakini mafanikio yake makubwa aliyapata akiwa Simba. Moja ya mafanikio yake ni kufunga magoli manane msimu wa 2012/13 ambayo hakupata kuyafunga kabla ya hapo.
Hata hivyo, naye alianza kuandamwa na mashabiki wa Simba kuwa hachezi vizuri akiwa na klabu yake, badala yake anajituma zaidi akiwa kwenye timu ya taifa. Alipelekwa Azam kwa mkopo na baadaye akatua Stand United United.
9. Edward Christopher-Toto Africans
Rekodi zinaonyesha kuwa huyu ndiye mchezaji aliyesababisha Simba kuamua kuwapandishwa wachezaji wake wa kikosi cha pili, baada ya kuwa mfungaji bora wa kwenye michuano ya Kinesi na Banc ABC Super8, pia kiiongoza Simba B kuwa bingwa wa michuano yote hiyo.
Alikuwa nyota kwenye mechi kati ya Simba na Yanga mzunguko wa kwanza msimu wa 2012/13.
Kwa mujibu wake mwenyewe ni kwamba starehe ndizo zilizompoteza.
10. Ramadhani Singano-Azam
Pia ni kati ya wachezaji aliotoka kikosi cha pili cha Simba. Aliyechelewa kidogo kukubalika, lakini baada ya hapo akawa msaada mkubwa kwa timu.
Kilichomuondoa hapo ni utata wa mkataba.
11. Kigi Makasi-Ndanda
Msimu mitatu nyuma aliwahi kuichezea klabu ya Simba, ingawa kabla ya hapo pia alishawahi kuichezea Yanga.
Ni mmoja kati ya mawinga hatari wakati wao. Pamoja na uwezo wake wa kupachika mabao akitumia guu la kushoto, majeruhi ya muda mrefu ndiyo yaliyofanya kuachwa na Simba na kuibukia Ndanda.










