Usiempenda kaja Aggrey Morris arejea uwanjani baada ya miezi minne

14Mar 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Usiempenda kaja Aggrey Morris arejea uwanjani baada ya miezi minne
  • Beki huyo wa zamani wa Mafunzo FC, hakuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC katika mechi 19 kilizocheza tangu Novemba Mosi ...

TANGU kuumia goti kwa Aggrey Morris, Azam FC imefungwa mabao nane katika mechi 11 za Ligi Kuu huku mabingwa hao wa 2013/14 wa Tanzania Bara wakitupia mabao 16.

Aggrey Morris akifanya mazoezi.

Beki huyo wa zamani wa Mafunzo FC ya Ligi Kuu ya Zanzibar, aliumia goti wakati akiwa na kikosi cha Zanzibar Heroes kilichokuwa kinajiandaa kwenda Ethiopia kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji na kulazimika kupelekwa Afrika Kusini kufanyiwa upasuaji.

Kuumia kwake kulikomfanya akose mechi 19 (11 za Ligi Kuu, tatu za Kombe la Mapinduzi, tatu za michuano maalum Zambia na mbili za Kombe la FA), kulionekana kuwa tatizo kubwa kwa safu ya ulinzi ya Wanalambalamba inayoongozwa na Serge Wawa.

Huku akiadhimisha miaka 32 tangu kuzaliwa kwake Machi 12, 1984, Morris alirejea uwanjani juzi na kuiongoza Azam FC kuibamiza Bidvest Wits ya Afrika Kusini mabao 3-0 katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Morris amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi la Azam FC akitengeneza kombinesheni ya ukuta wa 'chuma' na Muivory Coast, Wawa. Kuumia kwake kulimlazimu kocha mkuu Stewart Hall amtumie 'kinda' Abdallah Kheri ‘Sebo’.

Hata hivyo, Sebo pamoja na beki mwingine Racine Diouf waliumia hivi karibuni na kusababisha kuyumba kwa safu ya ulinzi ya Wanalambalamba. Katika kipindi hicho, kiungo mkabaji Erasto Nyoni alilazimika kucheza katika nafasi ya beki wa kati akishirikiana na Wawa, David Mwantika na Said Morad.

Kupona kwa Morris pengine ni habari mbaya kwa timu za Ligi Kuu ambazo bado zina mechi dhidi ya Azam FC msimu huu ikiwamo Simba.

Beki huyo ana uwezo mkubwa katika kukaba na kongoza timu. Ubora wake katika kupiga mashuti na penalti, ni sifa nyingine inayompa hadhi ya kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Azam.

Pengine msimu huu si mzuri kwa Morris. Katika mechi tisa za mwanzo za Ligi Kuu, beki huyo alicheza saba (kabla ya kuumia) kutokana na kulazimika kukosa mechi mbili dhidi ya Mbeya City FC na Coastal Union baada ya kulimwa kadi nyekundu wakati wa mechi yao ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC mkoani Shinyanga.

Morris ndiye mchezaji wa kwanza na pekee wa Azam FC aliyetolewa kwa kadi nyekundu katika mechi zote 20 walizocheza Ligi Kuu msimu huu.

KUHUSU MORRIS
Jina Kamili: Morris Aggrey Ambros[1]
Kuzaliwa: Machi 12,1984 (Umri 32)
Mahali: Zanzibar, Tanzania
Urefu: m 1.78 (ft 5 in 10)
Na. ya Jezi: 13
Alikotoka
2003–2009: Mafunzo
2009 hadi sasa: Azam FC

MECHI ALIZOKOSA MORRIS VPL
1. Azam FC 2 - 2 Simba SC
2. Majimaji 1 - 2 Azam FC
3. Azam FC 2 - 0 Kagera Sugar
4. Azam FC 1 - 0 Mtibwa Sugar
5. Azam FC 1 - 1 African Sports
6. Mgambo JKT 1 - 2 Azam FC
7. Azam FC 1 - 0 Mwadui FC
8. Coastal Union 1 - 0 Azam FC
9. Mbeya City 0 - 3 Azam FC
10. Tanzania Prisons 0 - 0 Azam FC
11. Azam FC 2 - 2 Young Africans