Kuiongeza Sudan Kusini EAC ni maslahi ya nani?

13Mar 2016
J.M. Kibasso
Nipashe Jumapili
Kuiongeza Sudan Kusini EAC ni maslahi ya nani?

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), iliyoundwa na Tanzania, Kenya na Uganda baada ya kupata Uhuru miaka ya 1960, licha ya kufanya vizuri kiuchumi ilivunjika mwaka 1977 na kuundwa tena 1999.

Viongozi Wakuu wa EAC akiwamo Mwenyeki wa EAC Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli

JUMUIYA ya Afrika Mashariki (EAC), iliyoundwa na Tanzania, Kenya na Uganda baada ya kupata Uhuru miaka ya 1960, licha ya kufanya vizuri kiuchumi ilivunjika mwaka 1977 na kuundwa tena 1999.

Juhudi kubwa zilifanyika ili kuisuka upya jumuiya hiyo kuanzia awamu ya wastaafu Rais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, ili kuirudisha tena na baada ya kusimama iliziongeza Rwanda na Burundi kuwa na wanachama wapya.

Wiki iliyopita katika kikao cha wakuu wa nchi hizo wameipa uanachama Sudan Kusini hivyo kufanya idadi ya wanachama kufikia sita.

Awali ya yote napenda nichukue fursa hii kuipongeza Sudan Kusini kwa kujiunga na mataifa hayo mengine matano kutoka Afrika Mashariki, wahenga walinena “umoja ni nguvu utengano ni udhaifu” karibu sana Sudan Kusini ndani ya muungano.
Harakati za kuundwa kwa jumuiya za ushirikiano wa kikanda barani Afrika zilivyoanza kupata mwamuko katika miaka ya 1960 mara baada ya nchi nyingi kupata Uhuru.
Magwiji wa siasa wakiwamo Dk. Kwame Nkurumah wa Ghana, Julius Nyerere na Patrice Lumumba wa Congp, ndiyo walikuwa vinara waliochochea muungano wa mataifa barani Afrika.

Historia inakumbusha jinsi magwiji wawili wa kisiasa Nkurumah na Nyerere walivyotofautiana kifikra juu ya utaratibu ambao ungefaa kufuatwa katika kufikia shirikisho la mataifa yote huru barani Afrika (Umoja wa Mataifa Huru ya Afrika.

Wakati Dk. Nyerere alipendekeza mataifa yaanze kuungana kikanda mfano Jumuiya ya Afrika Mashariki, ile ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika Magharibi ( Ecowas) na ya Pembe ya Afrika (IGAD) Dk. Nkurumah alipendekeza mataifa yaungane moja kwa moja badala ya makundi madogo ya kikanda.

Mkanganyiko huo wa kifikra ndiyo uliochochea Marais Jomo Kenyatta wa Kenya, Nyerere na Milton Obotte wa Uganda kukubalina kuanzisha EAC.

Muungano wa mataifa haya matatu sasa yameongezeka na kufikia sita. Hizi ni juhudi ambazo viongozi wakuu hawana budi kupongezwa kwa dhati kuongezeka kwa Sudan Kusini sasa kunaashiria kupanuka kwa ushirikiano wa kidemokrasia, uchumi na siasa miongoni mwa wanajamii wa nchi hizi.

Hata hivyo, wadadisi wa mambo ya siasa wanajiuliza, kulikuwa na umuhimu gani kuongeza Sudan Kusini wakati huu? Hili ni swali ambalo limekuwa likiwasumbua siyo tu wadadisi wa siasa bali hata wananchi wa kawaida.

Kimsingi dhima ya kuunda EAC, Tanzania, Kenya na Uganda ililenga hasa baadaye kuja kuwa na shirikisho, hatimaye kumpata Rais mmoja. Hili lengo halijafikiwa hadi leo.

Kuongezeka kwa mataifa ya Rwanda na Burundi, matarajio yalikuwa ni kufikia shirikisho. Tarajio ambalo nalo halijafikiwa hadi leo.

Ninachokusudia kusema ni kwamba, muda ulikuwa haujafika wa kuruhusu Sudan Kusini, kujiunga na EAC sababu mambo mengi yaliyotarajiwa kurekebishwa baina ya nchi hizo hayajafanyika.

Kwa mfano, Rais Paul Kagame wa Rwanda aliamua kuitisha kura ya maoni (refrundum) nchini kwake ili apate kibali cha kuongeza muhula wa tatu. Sambamba na hilo Rais Pierre Nkurunzinza, wa Burundi naye alitangaza kugombea kwa muhula wa tatu.

Kama hayo hayatoshi, Rais Yowen Museveni wa Uganda naye ameendelea kuongoza bila kujali dhana ya demokrasia.
Tulitarajia nchi wanachama kwa kutumia jukwaa la EAC viongozi hawa wangeitwa na kuelezwa kinagaubaga kuwa huo ni ukiukwaji wa katiba za nchi zao na ikibidi walazimishwe kuachia ngazi.

Kwa bahati mbaya hakuna aliyekemea marais hao badala yake wamebaki “kuleana” huku wakiimba wimbo wa kuimarisha jumuiya na kuongeza mataifa mengine kama hiyo Sudan Kusini.

Pengine hapakuwa na umuhimu wa kuongeza nchi hiyo , wanachama wameshindwa kufikia hata nusu ya malengo. Wengi wanasema kupanuka kwa EAC ni kiini macho kwasababu demokrasia imeendelea kutupwa kapuni.

Kinachoendelea nchini Burundi na Rwanda ni vielelezo tosha kwamba wakuu wa nchi wanalindana. Haiwezekani Rais akaamka asubuhi na kutangaza jambo ambalo linaenda kinyume na katiba ya nchi huku wanachama wakidai hawana mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya mwanachama mwingine kijeshi.

Kwa msingi huo, siyo muda muafaka kuongezwa kwa Sudan Kusini kwani nchi tano zinazounda jumuiya hiyo zingeandaa kwanza mfumo unaowapa nguvu ya kuichukulia hatua za kijeshi nchi inayokaidi maamuzi ya wenzake.

Kwa mazingira haya tusubiri kuona vituko vya nchi hizi sita kuanza kugawanyika kimaslahi kama tulivyowahi kushuhudia nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zikitenga Tanzania na Burundi na kuunda ushoroba wao.

Hii ndiyo maana wadau tunajiuliza kuongezeka kwa nchi ya Sudan Kusini ni kwa maslahi ya nani? Nchi gani itafaidika katika ongezeko la taifa hilo changa duniani.

Mawasiliano: 0713 399004/0767 399004, jmkibasso@gmail.com