Sumatra, Polisi acheni kulea majipu

13Mar 2016
Nipashe Jumapili
Sumatra, Polisi acheni kulea majipu

ENZI za kulala barabarani wakati wa safari za mikoani imeshapita kutokana na kujengwa miundombinu ya kisasa na kuwapo kwa mabasi yenye viwango na madaraja mbalimbali.

MABASI YAKIWA KATIKA KITUO CHA MABASI UBUNGO

Hata hivyo wakati mwingine wasafiri hulazimika kulala barabarani, kwani iko mikoa ambayo safari huchukua zaidi ya siku moja kutokana na sheria, kanuni na taratibu za kulinda usalama zilizowekwa na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Nimelazimika kuwaza kwa sauti, hili ambalo nitaliandika kwa mapana na marefu baada ya kuwa miongoni mwa abiria ambao walionja adha ya kulala njiani kwa safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ambako kwa mujibu wa taratibu za Sumatra wasafiri walitakiwa kufika Mwanza kati ya saa 5:00 na saa 6:00 usiku.

Kama kawaida basi ambalo nimehifadhi jina lake liliondoka Ubungo saa 12:00 alfajiri lakini mwendo wake ulikuwa ni wa kinyonga hata hivyo tulifika Chalinze saa 3:00 asubuhi na baada ya kupita kwenye mji huo mdogo gari hilo liliharibika na kulazimika kusubiri kifaa ambacho kingeletwa na magari mengine. Abiria walikaa kwa zaidi ya nusu saa kungoja kipuri hicho.
Tuliendelea na safari lakini mwendo ulikuwa wa kusuasua hadi tulipofika Morogoro majira ya saa 5:00 asubuhi, mahali ambako kwa mwendo wa kawaida tulitakiwa kufika saa 3:00 asubuhi hivyo tukachelewa kwa saa mbili.

Safari iliendelea tulivyofika Mvomero basi liliharibika tena na ilichukua zaidi ya dakika 45 kulitengeneza. Tukaanza tena safari ya Mwanza japo kasi ya basi ilizidi kupungua na haikuchukua muda mrefu likaharibika tena baada ya kuingia Gairo.

Kazi ya kulikorokochoa ilitumia zaidi ya dakika 30 kabla ya kurudi tena barabara na kutembea kwa hofu hadi tulipofika Dodoma saa 11 jioni.

Kwa uzoefu wangu kwa gari linalotembea mwendo unaotumiwa na mabasi kwa mujibu wa taratibu na sheria na usalama barabarani, kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma linatumia saa sita, lakini kwa basi bovu lililoruhusiwa kubeba abiria wa masafa marefu tulitumia saa 12.

Safari haikuwa rahisi tulipelekwa kwenye gereji ya basi hilo na kupewa gari jingine ambalo tuliendelea nalo lakini nalo kumbe halikuwa zima, lilikabiliwa na tatizo tena.Tukalazimika kusimama kusuburi kipuri kilichokuwa kimeharibika, mbaya zaidi kisafirishwe kutoka Dodoma, kwa kujua hasira za abiria walikuwa wakidanganywa kuwa basi linamsubiri abiria aliyeachwa kwa bahati mbaya.

Tulifanya jitihada za kuwasiliana na Sumatra lakini kwa masikitiko zaidi walieleza kuwa kampuni ya mabasi hayo ni korofi na inawasumbua sana wakawashauri abiria wasitumie tena magari hayo.

Mbaya zaidi dereva na kondakta wa basi la pili walikuwa ni wale ambao mteja kwao ni ‘fala’, kila tulipohoji juu ya kinachoendelea na sababu za kusimama mara kwa mara walikuwa wakali na kuwaeleza abiria kama walitaka kuwahi wangepanda ndege ama magari yao binafsi kwa kuwa mwenye mabasi ana hiari ya kufanya atakalo na mali yake wala hapaswi kupangiwa na kwa hasira walianza kwenda kwa mwendo kasi.

Kama haitoshi walipofika Igunga waliliegesha gari pembeni ya barabara wakaenda kulala nyumba ya wageni bila kuwasiliana na wasafiri ambao waliachwa ndani ya basi bovu na lenye viti ambavyo wasafiri hawakuwezesha kuvilaza ili wapumzike hivyo walibaki wima muda wote.

Kilichonisukuma kuandika haya ni kauli za kukera na adha abiria wanazokumbana nazo huku mamlaka za usimamizi wa usalama na usafiri barabarani zikizembea na kutoa maelezo kuwa kampuni fulani ni korofi na mabasi yake ni mabovu tena wakipata kigugumizi kuchukua hatua dhidi yake kwa sababu ambazo hazijulikani. Huku ni kufanya kazi kizembe na kinachohitajika ni kuwajibishwa.

Mathalani, Sumatra wanawaeleza wasafiri kuwa wasitumie mabasi hayo, je hilo tangazo limetolewa wapi na abiria wangapi wanaofika kukata tiketi mapema au siku ya safari wanapata taarifa za mabasi fulani kuwa hayastahili kutumiwa kwa safari?

Nilitaraji kwa kuwa polisi na Sumatra wana taarifa kamili za kampuni korofi wangechukua hatua kwa mujibu wa sheria kuliko kuacha wasafiri waendelee kunyanyasika na kusota barabarani kwa sababu ya kuogopana au kusubiri maafa makubwa kama ya ajali ndipo watoe salamu za pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na watakaotunza walemavu tena wakiwasihi madereva kufuata sheria za usalama barabarani.

Ndani ya basi hilo kumepambwa stika za Sumatra zikishawishi abiria kupaza sauti kwa kuwa jukumu la usalama barabarani ni la kila moja, iwaje upande mmoja unatengwa na kuachwa utaabike kwa sababu ambazo hazijulikani?
Haki ya abiria iko wapi au ndiyo kutimiza usemi wa msafiri kafiri? Kwanini polisi na Sumatra kuwe na kigugumizi kuwaeleza ukweli wamiliki na kuacha abiria wateseke kwani ndani ya basi hilo kulikuwa na mama wenye watoto wadogo pengine na wagonjwa.

Mbaya zaidi makondakta na dereva wake ni wenye kauli chafu na wala hawajali wateja kwa kuwa tulivyofika Dodoma kila mmoja alitakiwa kutoa mzigo wake kwenye buti ya gari la awali bila kujali kuna urefu kiasi gani, kimsingi ni kunyanyasa wateja kwa kuwa hawana watu wa kuwasemea.

Sumatra na polisi wa usalama barabarani msipotusemea abiria nani atusemee? Au mnasubiri ajali? Kwanini mnalea majipu mnayoyajua huku watumiaji wa mabasi hayo wakitaabika? Kigugumizi chenu juu ya mabasi hayo kinatoka wapi, tunajiukiza na hatupati majibu.

Chonde msisubiri kujitokeza mbele ya kideo kutoa masikitiko yenu juu ya ongezeko la ajali za barabarani bali zizuieni kwa kuchukua hatua kwa makampuni yenye mabasi mabovu.
Mungu ibariki Tanzania.