Nchini Tanzania, maadhimisho hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza kwa kuadhimishwa na familia inayolea mtoto mwenye ugonjwa usiyofahamika.
Katika kundi hilo, yamo magonjwa yasiyo ya kuambukiza, lakini yana athari kubwa katika afya ya binadamu. Kwa kifupi ni magonjwa ambayo chanzo chake yamejificha.
Miongoni mwa magonjwa hayo ni watoto wadogo kupata matatizo ya kuvimba kichwa kinachojaa maji, huku baadhi ya watoto hawakui huku umri wao ukiongezeka.
Siku hiyo katika nchi nyinginezo, ilizinduliwa kwa mara ya kwanza na taasisi ya Eurordis pamoja na Baraza Fungamani la Taifa la mwaka 2008.
Tangu wakati huo, matukio mbalimbali yamefanyika duniani na kufikia mamia ya watu wenye magonjwa hayo.
Ni jambo lililofanya kutambulika kwa uwepo na magonjwa hayo na namna yanavyoismbua jamii, kisha ikaanza kuripotiwa katika jamii na mamlaka husika kupitia vyombo vya habari na mijumuiko ya kijamii.
Hayo ni matokeo ya mchango unaotolewa kupitia sera na mipango ya kitaifa kwa magonjwa hayo katika baadhi ya nchi.
Kihistoria, kampeni kuhusu magonjwa hayo ilianza kama tukio lililowahusu watu wa barani Ulaya, lakini hatimaye likafikia hatua nzuri. Marekani iliungana na ajenda hiyo mwaka 2009.
Mwaka 2015 zaidi ya nchi 80 duniani kote zilishiriki kampeni hiyo.
Kaulimbiu ya Siku ya Magonjwa hayo yanayotokea kwa kundi dogo la jamii ya mwaka 2016 ni ‘Sauti za Wagonjwa.’
UZOEFU WA MAGONJWA HAYO
Miongoni mwa wanaouguza watoto wenye maradhi hayo, ni Sharifa Mubaraka, ambaye ni mama wa watoto wawili. wa kwanza ni Ali Kimara, mwenye umri wa miaka mitano.
Mama huyo anaelezea namna alivyopitia changamoto za kuuguza motto huyo.
Sharifa anasema mtoto wake huyo alianza kuugua akiwa na umri wa miaka miwili. Anafafanua: “Ilikuwa ni majira ya jioni, Ali alishikwa na homa kali na baada ya kumpeleka kwa daktari wa watoto, alisema hajawahi kuona ugonjwa kama huo.”
Mama huyo anasema kuwa, Ali aliyebanwa na kifua na kubadilika rangi inayofanana na bluu, alikimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Sharifa anasema, Ali aliwekewa mashine ya kupumua kwa siku mbili na baadaye alipata nafuu, lakini wakati akikaribia kutoka, hali yake ilibadilika na kuzidiwa zaidi.
“Mwanangu alibanwa na kifua kisichoelezeka na kwa sababu hospitali haikuwa na vifaa vya kumtibu na kutambua ugonjwa wake, walituhamishia hospitali yao Nairobi nchini Kenya,” anasema mama huyo.
Anabainisha kuwa, alimtibu mtoto wake kwa miaka miwili mfululizo, huku akiendelea kumtumaini nafuu kutoka kwa Mungu.
“Yapo magonjwa tofauti yanayowasibu watu wachache takribani 7000 ambayo yameshabainishwa duniani hadi leo na Tanzania haiwezi kujitoa kwenye hili,” anasema na kuongeza:”Hata hivyo watu wengi hapa Tanzania hawana uelewa kuhusu magonjwa hayo.”
Sharifa anasema mwanawe wa pili, Nasreem Mohammed (3), naye anasumbuliwa na magonjwa hayo.
Anasema uzoefu wake amepa msukumo na kuamua kuwaunganisha wazazi, wagonjwa wenye matatizo hayo, pia watu wenye mapenzi na wagonjwa kuchukua hatua ya kusaidiana.
“Watoto wangu wawili wanaugua magonjwa haya yanayowakabili, sehemu ndogo ya jamii tangu walipozaliwa,” anasema kwa hisia na kuongeza kuwa, uzoefu kutoka kwa familia yake, umemhamasisha kuishtua jamii kuwa na uelewa wa uwepo wa magonjwa hayo nchini.
DAKTARI BINGWA ANENA
Mtaalam bingwa wa tiba ya watoto, Dk. Karim Manji, anasema maishani mwake hajawahi kukutana na ugonjwa uliomsumbua akili kama wa mtoto Ali, ambaye alimpokea kwa mara ya kwanza na kumpatia huduma ya kwanza.
Anasema Ali ambaye alikuwa amebadilika rangi na kuwa wa bluu, alishindwa kutambua namna ya kumtibu, kwa sababu aliokosa vifaa vya tiba hiyo nchini.
“Kwanza sijawahi kuona mwanamke jasiri kama Sharifa, ambaye hakuonyesha kukata tamaa hata mara moja wakati wa kumuuguza mtoto wake na badala yake alionyesha ujasiri na kuzidi kumuombea,” anasema.
TAFSIRI YA KIDAKTARI
Dk. Manji ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUCHS), anatoa tafsiri ya kitaalam kuwa, magonjwa yasiyotambulika ni “yale ambayo hayatambuliki kwa haraka.’
Anasema magonjwa hayo serikali imekuwa haiyapi kipaumbele, kwa sababu hakuna vifaa tiba vya kuyatambua.
Mtaalam huyo anasema magonjwa hayo huwakumba watoto wadogo, muda mfupi baada ya kuzaliwa au wengine wanazaliwa nayo.
Anasema magonjwa hayo pia husababisha athari kama vile mtindio wa ubungo na matatizo ya akili.
CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto zinazowakabili magonjwa yasiyotambulika,ni kutokuwa na wataalam wa kutosha wa kuyatambua kwa urahisi.
Anasema changamoto kubwa ni wazazi kuwaficha watoto wao na kuogopa gharama za matibabu.
“Mzazi akiona anamtibia mtoto bila ya kuonyesha dalili za kupona anaamua kuacha na kumficha ndani,” anasema.
Pia anasema changamoto nyingine ni kuhusu magonjwa hayo ni dhana ya ushirikina, hali inayowafanya wazazi kuwaficha watoto wo.
NINI KIFANYIKE?
Dk. Manji anasema kuwa wazazi na walezi wenye watoto hao, wanapaswa kujitokeza kuwatibu na kuchukulia katika hali inayofanana na magonjwa mengine ya kawaida.
Anashauri serikali iyatambue na kuyapa kipaumbele, kwa kuandaa vifaa tiba na wataalam wa kuyatambua na kutibu.
Dk. Manji anasema serikali inapaswa kujenga shule za kuwapeleka watoto hao, ili wapate elimu, kwani mazingira yao hayawezi kuchanganya na wengine.
“Lazima serikali ingilie kati kwa kuyatambua magonjwa haya na kuweka mazingira mazuri ya kutoa tiba, pamoja na wataalam wa kuyatambua,” anasema.
Anasema pia jambo kubwa ni elimu ya utambuzi juu ya magonjwa haya kwa jamii ili kuondokana na mila potofu pamoja na unyanyapaa.
“Jamii inapaswa kupatiwa elimu juu ya magonjwa haya, ili kuondokana na unyanyapaa unaowakuta watu wenye magonjwa haya wakidhani ni ushirikina au hali isiyo ya kawaida,” anasema.
Anasema jamii ikielimishwa, wagonjwa hawatafungiwa ndani tena na jamii itawasaidia watoto pamoja na wazazi kuepuka vitendo vya kuwaficha ndani.
MAADHIMISHO YA SIKU HIYO
Mdau wa sekta ya afya, Monica Joseph, anasema lengo la kuadhimisha “Siku ya Magonjwa Yasiyotambulika” ni kujenga uelewa miongoni mwa jamii.
Anasema kuwa, magonjwa hayo yanayotokea kwa kundi dogo la jamii na athari zake kwa maisha ya mgonjwa.
Monica anasema kwa kushirikiana na wadau anaowajumuisha na watu wenye magonjwa ambayo ni mara chache huathiri watu wengi, wametangaza kampeni ya kujenga uelewa kuhusu magonjwa na maadhimisho ya siku hiyo.
“Siku hii ambayo haifahamiki sana nchini Tanzania inalenga kujenga uelewa miongoni mwa jamii kuhusu magonjwa yanayotokea kwa kundi dogo la jamii na madhara ya magonjwa hayo,” anasema Monica.
Pia anaongeza kuwa ni wakati muafaka kwa Watanzania kuwa na tahadhari kwa magonjwa hayo, ili jamii ifahamu mbinu za kuyadhibiti, pindi watakapoyakuta ndani ya jamii.










