HIVI sasa dunia inashuhudia mabadiliko katika mifumo tofauti ya kijamii nchini, ikiwa ni matokeo ya uongozi wa Rais John Magufuli.
Rais Magufuli ameonyesha ujasiri kwa kufikia hatua kadhaa zilizofikirika, kwamba isingekuwa rahisi kwa kiongozi wa nchi anayetokana na mfumo unaoshutumiwa kwa kuifanya nchi kuwa masikini zaidi, kufanya uamuzi anaoufanya sasa.
Amefanya uamuzi katika maeneo mengi, miongoni mwa hayo ni kubadili taswira ya maana ya utumishi wa umma kutoka kwa unyang’anyi na uporaji wa mali za umma, jeuri na kiburi, unyanyasaji na ubaguzi, badala yake kuitafuta, kuisimamia na kuiendeleza haki.
Yapo mambo ingawa si ya ovyo, lakini yalitengewa fedha nyingi za umma ambazo zingefaa kuelekezwa katika matumizi mengine yenye tija na manufaa kwa walio wengi. Ndivyo inavyofanyika sasa.
Mfano ni kuagiza mamilioni ya Shilingi yaliyotengwa kwa ajili ya hafla, yakitumika kama sehemu ya kupora fedha za umma. Rais Magufuli akaagiza zielekezwe katika upatikanaji na uboreshaji wa katika huduma za jamii.
Uzembe katika maeneo ya kazi hasa kwa sekta za umma ilikuwa moja ya sifa chafu za Tanzania na Watanzania, lakini sasa utawala wa Rais Magufuli umechangia kuleta mabadiliko.
Uwajibikaji umekuwa sehemu ya sifa za mtumishi bora katika sekta za umma na binafsi. Hivi sasa walio wengi wanajituma, wanawajibika, wanafanya kazi kwa nguvu na maarifa.
Ule msemo wa ‘nchi inajengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno’ sasa herufi zake zinafutika. Utafika wakati mstari mzima ukatoweka. Watu watawajibika kwa mambo wanayoyafanya. Ndio kusudio lililo jema.
Kikubwa zaidi ni namna watu wachache walivyotumia propaganda ya ovyo ya ‘kasungura kadogo ka taifa’, wakimaanisha uwapo wa rasilimali chache hasa fedha za ndani katika kuleta maendeleo.
Ukweli unabainika sasa kupitia kwa utawala wa Rais Magufuli, kwamba kumbe ‘kasungura’ kalikofanyiwa propaganda kaliwekwa nje ya banda lenye mifugo minono iliyotaifishwa na wachache, wakijineemesha.
Wao wakaendelea kula nyama, kunywa maziwa na kutumia mazao ya mifugo kwa kutengeneza vitu vya thamani, mamilioni ya Watanzania wakapumbazwa na uwapo wa ‘kasungura’, wakikakodolea macho wasijue cha kufanya.
Rais Magufuli akalibaini hilo na kurejea kile kilichojaribiwa na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kupitia dhana yake ya ‘fagio la umma.’
Lakini kwa Rais Magufuli, kasi na kiwango cha kuwashughulikia walioficha mifugo minono ya umma (mafisadi) wakieneza propaganda ya uwapo wa ‘kasungura kadogo…hakatoshi’ imekuwa kubwa.
Zipo sababu kadhaa za kasi ya Rais Magufuli kuyashughulikia hayo, miongoni mwake ni ongezeko la mbinu na teknolojia zinazofanikisha uporaji wa rasilimali za umma. Mara nyingine vikifanyika kupitia mifumo sahihi ya sheria zilizopo.
Nyuma ya pazia inabainika kuwa sehemu ya sheria hizo, mathalani ile ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 zinatoa mianya ya kufanyika ‘wizi mwema’ unaohalalishwa na sheria husika.
Pia wapo watumishi wa umma wanaotumia madaraka ama ofisi za umma vibaya. Wakageuka kuwa ‘miungu watu’ wanaoamua kiasi gani cha rasilimali za nchi zielekezwe katika kujimilikisha, ikiwamo kupitia tafsiri hasi za kanuni na taratibu zinazowaongoza.
Kwa maana nyingine, hali kama hizo na nyingine zote zinazokwamisha maendeleo ya nchi na ustawi wa watu, zinatimiza ile hekaya ya ‘kila jaribio lina mlango wa kutokea.’
Kwamba wahusika wanafahamu vema juu ya uovu wanaoufanya, dhuluma wanayolitendea taifa na raia wake masikini, lakini wanaambulia kupora, kuiba na kuhujumu rasilimali za nchi.
Wanatambua kuwapo ukosefu wa huduma bora katika sekta kama za maji, kilimo, afya, elimu, usafiri, mawasiliano na nyinginezo. Kwao si kitu zaidi ya kufikiria manufaa binafsi.
Katikati ya hali hiyo, Rais Magufuli na utawala wake wanaleta tumaini jipya ambalo hata hivyo lipo katika hatua za awali, kiasi cha baadhi ya watu kutahadharisha isijekuwa ni ‘nguvu ya soda’.
Rais Magufuli anajibu hofu hiyo mara kadhaa akisema hakuna nafasi ya kupungua kwa nguvu halisi ya serikali yake katika kuwatumikia wananchi na kudhibiti dhuluma zilizowaathiri kwa miongo kadhaa sasa.
Lakini wapo wanaopinga utendaji huo unaojulikana zaidi kama ‘kutumbua majipu’, wakimkosoa kuwa uamuzi wake haukidhi matakwa ya kisheria.
Ni kweli utawala wa kisheria ni moja ya misingi ya demokrasia, lakini ni sheria hizo zinazotumika kwa tafsiri halisi ama hasi, kupora rasilimali za umma.
Ni sheria hizo zinazofichwa kwenye kabati za ofisini na kutoa mianya kwa wanaopaswa kuzisimamia, kuwa mfano wa wanyang’anyi. Rais mwenye mapenzi mema kwa nchi yake.
Pamoja na kuwapo hoja zinazojadilika kutoka kwa wanaomkosoa Rais Magufuli, ikumbukwe kwamba hatua kadhaa zinazofikiwa sasa zinatoa jawabu la hitaji la umma kwa takriban miaka 10 iliyopita kuhusu kuchukuliwa kwa uamuzi mgumu.
Miongoni mwa wanasiasa, viongozi wa dini, waandishi wa habari, wanataaluma na wengine, walihoji udhaifu wa serikali uliosababishwa na kutochukuliwa kwa uamuzi mgumu.
Kwa tafsiri rahisi, uamuzi mgumu ni ule unaolenga maslahi ya umma hata kama utakuwa ni kinyume cha sheria kandamizi zinazopaswa kufutwa haraka iwezekanavyo.
Kuendelea kuliongoza taifa kupitia sheria kandamizi na zile zinazotoa mianya ya kulididimiza taifa katika ‘umasikini wa kutupwa’ hakuna maana, manufaa wala tija kwa taifa.
Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana kupitia simu namba +255754691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com au mashaka.mgeta@guardian.co.tz.










