Yafahamu mazoezi yanayoujenga ubongo

10Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Yafahamu mazoezi yanayoujenga ubongo

Hivi sasa imekuwa kama ‘fasheni’ kwa watu kufanya mazoezi. Nyakati za jioni katika siku za wiki hasa maeneo ya miji mikubwa kama Dar es Salaam, utakutana na watu wakikimbia kwenye njia za waenda kwa miguu wakifanya mazoezi.

Watu wakifanya mazoezi ya kukimbia, ambayo kiafya yanaelezwa kuwa na manufaa sana katika tija ya ubongo. (PICHA NA MTANDAO)

Wakati wa wikiendi, watu wengi huamka asubuhi kukimbia na pia nyakati za jioni. Pia kwenye miji mikubwa kumeanzishwa sehemu za kufanyia mazoezi (gym) na imekuwa kawaida kwa wafanyakazi wengi wanapotoka kazini kupita sehemu hizo kwa ajili ya kujenga mwili.

Hata hivyo, wataalam wanaeleza kuwa baadhi ya mazoezi yanazidiana faida kulinganisha na mengine katika kujenga ubongo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa kwa panya, wanasayansi wamebainisha aina ya mazoezi yanayojenga mishipa ya fahamu na ubongo kwa ujumla.

Kwa mujibu wa wanasayansi hao ni kwamba mazoezi ya kukimbia, kupunguza uzito na kuimarisha mwili; yana uwezo mkubwa wa kujenga ubongo.

Wanasayansi wanaeleza kuwa mazoezi yanabadilisha muundo na utendaji wa ubongo na kwamba utafiti uliowahusisha panya na binadamu umebaini nafasi ya mazoezi ya kukimbia katika maisha ya mwanadamu.

Utafiti huo umebaini kuwa, kukimbia kunaongeza uwezo wa ubongo na unaweza kupunguza idadi na ukubwa wa mashimo yanayohusiana na umri, kwenye seli nyeupe na za kijivu katika ubongo.

Pia, mazoezi hayo yanaweza kuzalisha seli mpya kwenye ubongo wa mtu mwenye umri mkubwa hivyo kupunguza mikunjo ya ngozi.

Kwamba mazoezi ya kukimbia yanatajwa kuongeza mara mbili hadi tatu, uwezo wa ubongo wa mbele unaotumika kujifunza na kutunza kumbukumbu.

Hata hivyo, wanasayansi wanaeleza kuwa mafanikio ya kujenga ubongo yanategemea umbali mtu anaokimbia.

Utafiti mpya uliochapishwa kwenye Jarida la Saikolojia la mwezi huu, unasema kuwa watafiti wa Chuo Kikuu cha Jyvaskyla nchini Finland na taasisi nyinginezo, wamekusanya madume ya panya na kuyadunga sindano zenye seli mahsusi kwenye ubongo. Kundi moja la panya lilifungwa magurudumu ya kukimbia miguuni na yalitakiwa kufanya mazoezi kwa maili kadhaa kila siku na kundi lingine liliachwa tu bila ya kufanya chochote.

Aidha, panya wengine walifanyishwa mazoezi ya kupanda ukuta wakiwa na vitu vizito kiasi kwenye mikia yao na makundi yote yalitakiwa kufanya mazoezi kwa dakika 15 kila siku.

Mazoezi hayo yalifanyika kwa wiki saba na kisha watafiti walichunguza tishu za ubongo katika kila kundi la panya hao na kubaini tofauti kubwa kati ya wale waliofanyiwa mazoezi na waliokaa tu.

Panya waliofungwa magurudumu ya kukimbia walibainika kuwa na viwango imara zaidi kwenye ubongo na kuzalisha seli mpya, ikilinganishwa na panya waliokaa tu na kwamba panya waliokimbia zaidi wakati wa majaribio walichochea zaidi uimara wa seli mpya kwenye ubongo.

Panya waliopewa mazoezi ya kupunguza uzito pamoja na kwamba walionyesha uimara wa seli kwenye ubongo ikilinganishwa na walivyokuwa wanaanza, lakini uimara upo zaidi kwa panya waliokimbia.

“Ni wazi, panya si watu. Lakini maana ya matokeo haya ni changamoto,” anasema Miriam Nokia, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Jyvaskyla ambaye aliongoza jopo la utafiti huo.

Anaongeza kuwa: “Mazoezi endelevu yanaweza kuwa na manufaa zaidi kwa ajili ya afya ya ubongo pia kwa binadamu.”
Watafiti hao wanaeleza kuwa kukimbia umbali mrefu kuna faida nyingi zaidi katika kukuza mishipa ya ubongo ikilinganishwa na mazoezi mengine, ingawa Dk. Nokia na wenzake wanabainisha kuwa mazoezi hayo yanachochea kuzalisha seli mahsusi katika ubongo na kwamba umbali zaidi mtu anaokimbia unachochea zaidi uzalishaji huo.

Aidha, mazoezi ya kupunguza uzito, kwa upande mwingine, yamebainika kuwa na manufaa zaidi kwa afya misuli.

Wataalam hao wanashauri kuwa kama ulikuwa kwenye mpango wa mazoezi ya viungo endelea, lakini jenga mazoea ya kukimbia au kuendesha baiskeli kwa ajili ya kujenga afya ya ubongo wako.