Mambo 10 yasikupite Azam vs Yanga

07Mar 2016
Sanula Athanas
Nipashe
Mambo 10 yasikupite Azam vs Yanga
  • Mechi 16 zilizopita za Ligi Kuu kati ya timu hizo hakikutoa mbabe kila upande ukishinda mara tano na kutoka sare mara sita.

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu huu ilitinga raundi ya 21 mwishoni mwa wiki, magoli 11 yakifungwa kwenye viwanja saba juzi huku Uwanja wa Taifa ukiendelea kuwa na idadi kubwa ya mabao.

Mchezaji wa Yanga, Amiss Tambwe akichuana na kipa wa Azam Aishi Manula

Majimaji walitoka suluhu ugenini dhidi ya African Sports sawa na matokeo ya Toto Africans dhidi ya Ndanda FC jijini Mwanza wakati Kagera Sugar wakilazimishwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Mgambo JKT.

JKT Ruvu waliyaanza vyema maisha mapya ya Uwanja wa Mabatini walipoichapa bao 1-0 Mwadui FC huku timu nyingine ya Shinyanga, Stand United ikipigwa 1-0 na Tanzania Prisons jijini Mbeya wakati Mtibwa Sugar wakiishindilia mabao 3-0 Coastal Union inayokabiliwa na mgomo wa wachezaji.

Shughuli pevu ilikuwa Dar es Salaam, mabingwa watetezi Yanga walipobanwa kwa sare ya 2-2 na mabingwa wa 2013/14 wa ligi hiyo, Azam FC.

Spotika inayofuatilia kwa kina ligi hiyo, leo inaletea rekodi na mambo 10 ambayo yaliyojitokeza katika mechi ya juzi ya Azam FC dhidi ya Yanga.

1. JUMA ABDUL
Katika dakika ya 12 ya mchezo wa juzi, Juma Abdul alitupia kwenye nyavu za timu yake wakati akijaribu kuokoa mpira wa krosi ya straika Kipre Tchetche.
Beki huyo wa pembeni kulia ambaye msimu uliopita aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu na wa mwisho wa Yanga kutolewa kwa kadi nyekundu, amekuwa mchezaji wa kwanza wa Yanga na wa tatu kwa timu zote 16 kujifunga msimu huu.

2. HIMID MAO
Juzi alionywa kwa kadi ya njano na refa Kennedy Mapunda katika sekunde ya 58 baada ya kujiangusha ndani ya boksi kusaka tuta. Kiungo huyo wa Azam FC ameweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyelambwa kadi ya mapema zaidi msimu huu.

3. BOCCO ANATISHA
Nahodha wa Azam, John Bocco 'Adebayor' alirushiwa chupa za maji na baadhi ya mashabiki wa Yanga baada ya kuisawazishia timu yake katika dakika ya 71 juzi.
Goli hilo lililokuwa la nane kwake msimu huu, lilikuwa la 10 kuitungua Yanga Ligi Kuu tangu msimu wa 2008/09 (msimu wa kwanza wa Azam FC Ligi Kuu) na kuendelea kuwa mchezaji aliyeifunga mabao mengi zaidi timu hiyo ya Jangwani katika kipindi hicho.

4. MECHI 5 KAPA
Matokeo ya mechi ya juzi pia yalimaanisha kwamba timu hizo zimeshindwa kufungana ndani ya dakika 90 katika mechi zote tano walizokutana msimu huu wakitoka sare robo-fainali ya Kombe la Mapinduzi, Ngao ya Jamii, mechi ya duru la kwanza Ligi Kuu na ile ya hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mwaka huu.

5. MABAO 45
Mabao manne yaliyofungwa juzi yaliifanya idadi ya magoli katika mechi za Ligi Kuu kati ya timu hizo kufikia 45. Yanga imetupia mara 23 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

6. MSIMU WA KIPEKEE
Sare ya juzi iliufanya msimu huu kuwa wa kwanza kwa mechi mbili baina ya timu hizo kutotoa mshindi katika ligi ya Bara tangu kikosi cha Wanalambalamba kianze kushiriki Ligi Kuu 2008/09. Misimu mingine saba iliyopita ilikuwa na vipigo na sare au vipigo katika mechi zote mbili za kila msimu.

7. ALI MUSTAFA 'BARTHEZ'
Yanga imefungwa mabao 11 katika mechi 20 ilizocheza Ligi Kuu msimu huu. Kipa Ali Mustafa 'Barthez' ambaye alipangwa katika mechi 11, amefungwa magoli saba, matatu dhidi ya Azam FC, mawili dhidi ya Mwadui FC huku JKT Ruvu na Toto Africans zikimtungua mara moja kila moja.

8. AISHI MANULA
Mechi ya jana iliweka rekodi ya kuwa ya tatu kwa kipa Aishi Manula wa Azam FC kufungwa mabao mawili katika mechi moja msimu huu. Kipa huyo (20) alipangwa katika mechi zote 20 zilizopita akifungwa mabao 13.
Manula alifungwa mabao mawili katika ushindi wao wa 4-2 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Karume na sare ya 2-2 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa. Mabao mengine saba alifungwa kwenye mechi zao (moja kila mechi) dhidi ya Prisons, Yanga (duru la kwanza), Majimaji, Mbeya City, African Sports, Mgambo na Coastal.

9. MECHI 16 BILA MBABE
Sare ya juzi pia ilizifanya mechi zote 16 zilizopita za Ligi Kuu kati ya timu hizo mbili kutotoa mshindi, kila timu ikishinda mara tano na kuambulia sare mara sita.

10. VITI VYA TAIFA
Mapema kipindi cha kwanza, kulitokea vurugu baina ya mashabiki wa timu hizo na kusabababisha kung'olewa kwa viti vya Uwanja wa Taifa. Ni tukio la kwanza kujitokeza kwenye uwanja huo mkubwa zaidi nchini tangu mashabiki wa Simba walipofura hasira na kung'oa viti baada ya Kagera Sugar kusawazisha kwa tuta katika dakika ya mwisho misimu miwili iliyopita.

REKODI ZA AZAM vs YANGA
Yanga vs Azam VPL
2008/09

1. Azam 1-3 Yanga (Oktoba 15, 2008)
2. Yanga 2-3 Azam (Aprili 8, 2009)

2009/10
3. Azam 1-1 Yanga (Oktoba 17, 2009)
4. Yanga 2-1 Azam (Machi 7,2010)

2010/11
5. Azam 0-0 (Okt 24, 2010)
6. Yanga 2-1 Azam (Machi 30, 2011)

2011/12
7. Azam 1-0 Yanga (Sept 18, 2011)
8. Yanga 1-3 Azam (Machi 10, 2012)

2012/13
9. Azam 0-2 Yanga (Nov 4, 2012)
10. Yanga 1-0 Azam (Feb 23, 2013)

2013/14
11. Azam 3-2 Yanga (Sept 22, 2013)
12. Yanga 1-1 Azam (Machi 19, 2014)

2014/15
13. Yanga 2-2 Azam (Des 28, 2014)
14. Azam 2-1 Yanga (Mei 5, 2015)

2015/16
15. Yanga 1-1 Azam
16. Azam 2-2 Yanga