JUSTICE MAJABVI; Kadi nyekundu iliamua matokeo ya mchezo

07Mar 2016
Faustine Feliciane
Nipashe
JUSTICE MAJABVI; Kadi nyekundu iliamua matokeo ya mchezo

SIMBA wiki iliyopita imepoteza mchezo wake wa kwanza katika michezo saba waliyocheza chini ya Kocha Jackson Mayanja baada ya kukubali kipigo cha magoli 2-0 mbele ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

KIKOSI CHA SIMBA

Simba wamepokea kipigo hicho katika kipindi, ambacho mashabiki na wadau wa klabu hiyo waliamini timu yao itaibuka na ushindi kutokana na kiwango kizuri na matokeo ya ushindi walioupata katika michezo sita kabla ya kukutana na Yanga.

Mmoja wa wachezaji ambaye alikuwa muhimili kwenye mchezo huo, Justice Majabvi, ambaye pamoja na Simba kupigwa magoli 2-0 anasisitiza kuwa bado timu yao ipo kwenye mbio za ubingwa.

"Kwanini tukate tamaa...bado kuna michezo mingi mbele yetu, chochote kinaweza kikatokea," alisema Majabvi.
Nyota huyo raia wa Zimbabwe, alisema wataendelea kupambana hadi mchezo wa mwisho kupata ushindi.

"Hatujapishana sana kwa pointi kati yetu, Azama na Yanga. Bado tuna nafasi katika mbio hizi za ubingwa," aliongeza.
Alisema walijipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo, lakini mambo yalikwenda kinyume na matarajio.

UWEZO WA KUCHEZA NAFASI ZAIDI YA MOJA

Majabvi alisajiliwa Simba kama kiungo mkabaji na hata wakati anawasili aliweka wazi kufurahia kucheza nafasi hiyo.
Hata hivyo, ndani ya kikosi hiho cha Simba, Majabvi, amekuwa akitumika kwenye nafasi zaidi ya moja kulingana na mahitaji ya mwalimu.

Mwanzoni mwa ligi wakati timu ikiwa chini ya Kocha Muingereza, Dylan Kerr, Majabvi mara kwa mara alikuwa akitumiwa kama beki wa kati. Kiungo huyo anasema yuko tayari kucheza namba yoyote kati ya kiungo mkabaji na beki wa kati kulingana na mahitaji ya mwalimu.

KADI NYEKUNDU YA BANDA

Majabvi anasema Yanga ni kama walikuwa na bahati zaidi kwenye mchezo huo."Naamini kama tungekuwa tumetimia kama ilivyokuwa tangu mwanzo wa mchezo, Yanga wasingepata nafasi ya kushinda," anasema Majabvi.Anasema kuwa kadi ya pili aliyoonyeshwa Banda kwenye mchezo huo ndio iliyoamua matokea.

"Hakuna wa kulaumiwa kwa matokeo ya mchezo ule. Katika soka, makosa ni mambo yasiyokwepeka," anasema Majabvi.
Majabvi anasema kuwa wachezaji waliumizwa na matokeo ya mchezo huo, lakini wametiwa moyo na kocha na viongozi.

SIMBA NA YANGA NI ZAIDI

Akizungumzia upinzani uliopo kwenye michezo ya timu kubwa za Simba na Yanga (Derby), Majabvi anasema: "Inasisimua kwa kweli, niliwahi kusikia kabla kuja hapa (Tanzania) na hata wakati mchakato wa kusajiliwa Simba unaendelea kuwa timu hizo zina upinzani mkali."

Anasema kuwa msisimko na upinzani uliopo zinapokutana Simba na Yanga ni mkubwa na umezizidi 'Derby' nyingi Afrika.
"Moja ya mambo ya kusisimua ni mashabiki jukwaani pamoja na mbwembwe zao.

Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zimbabwe, anasema kuwa mbali na mambo yote, ligi kuu ina upinzani mkubwa.

"Hapa hakuna timu ndogo, unaweza kuona Simba, Yanga au Azam wanaweza wakafungwa na timu yoyote, hakuna uhakika wa ushindi."